27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Ummy: Msiwatenge wagonjwa wa ukoma

Ramadhan Hassan – Dodoma

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu,  ameitaka  jamii kutowatenga watu wenye ugonjwa wa ukoma kwani hupata sonona, huzuni na wasiwasi kutokana na mtazamo hasi uliopo katika jamii.

Pia amezitaka halmashauri nchini kutenga fedha kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la ugonjwa huo.

Kauli hiyo aliitoa juzi, katika kijiji Samaria Kata ya  Hombolo Bwawani mkoani Dodoma wakati akikabidhi msaada wa chakula na viatu kwa wazee wenye ukoma kuelekea kumbukumbu ya watu wenye ukoma duniani ambayo huazimishwa kila Jumapili ya mwisho ya Januari.

Msaada alioutoa ni mchele kilo 100, maharage kilo 50, unga wa sembe kilo 50 na viatu jozi 48.

Waziri Ummy alisema asilimia  50 ya watu wenye ukoma hupata sonona na huzuni na wasiwasi kutokana na mtazamo hasi uliopo katika jamii juu ya watu hao.

Hivyo alitaka jamii kutowabagua ikiwa ni pamoja na kufanya kazi na kushirikiana nao katika mambo mbalimbali ambapo alidai kwamba  huwezi kuupata ugonjwa huu kwa kushikana mkono,au kula.

“Ukoma sio laana hivyo unyanyapaa juu yao ndio hufanya wajifiche na kutoenda hospital kupata matibabu hivyo kuambukiza wengine,” alisema.

Aidha, Waziri Ummy alisema ugonjwa huo sio wa kurithi wala kurogwa ambapo wizara yake itaendelea kuchukua hatua kuahakikisha ukoma unatokomezwa pamoja na kutoa dawa kwa wale ambao wanaumwa.

“Dalili za ugonjwa huu ni kutoka mabaka ya rangi ya shaba mwilini, ambayo hayaumi wala kuwasha na yanaweza kujitokeza sehemu yoyote mwilini kuanzia kichwani mpaka miguuni,” alisema Waziri Ummy.

Alisema ugonjwa huo huambukiza kwa njia ya hewa kwa mgonjwa ambaye hajaanza tiba katika maeneo ambayo yana hewa finyu.

Waziri Ummy pia alisema lengo la siku ya ukoma duniani ni kuwakumbusha watu juu ya ugonjwa huo ambao husababisha ulemavu wa kudumu,upofu,vidonda sugu,kukatika vidole vya miguu vya mikono,pua na masikio.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles