24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

Umeya waivuruga CCM, Chadema

DSC_0373-FILEminimizerNa Waandishi Wetu

UCHAGUZI wa umeya katika manispaa mbalimbali umedaiwa kuanza kukivuruga Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Kutokana na kuvurugwa huko, vyama hivyo vimeanza kulazimisha kutumia mbinu mbadala kuhakikisha vinashinda uchaguzi huo unaofanyika nchi nzima.

Moja ya mbinu wanazodaiwa kutumia ni kulazimisha wabunge wa viti maalumu kwenda kujisajili katika manispaa za mikoa mingine kama madiwani ili waweze kupiga kura katika uchaguzi wa umeya.

Kitendo cha vyama hivyo kulazimisha wabunge hao kupelekwa katika manispaa nyingine kimeibua utata na kusababisha baadhi ya uchaguzi huo kutofanyika.

Miongoni mwa wabunge wanaotajwa kuibua utata huo ni wale waliotoka Zanzibar na kuja Dar es Salaam kutaka kushiriki uchaguzi wa meya na naibu meya.

Baada ya utata huo kuibuka, Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) umemtaka Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, awape majibu ya uhalali wa wabunge hao kwenda kupiga kura za umeya na unaibu meya katika maeneo ambayo si yao.

Akitoa tamko Dar es Salaam jana, Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara, alisema kabla ya kikao kijacho wanamtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala apeleke kanuni na sheria zinazowaongoza.

Alisema wanahitaji vitu hivyo ili kufahamu uhalali wa ushiriki wa wabunge kutoka Zanzibar wanaofanya idadi ya wabunge kuongezeka na kusababisha uchaguzi wa umeya na unaibu umeya kuvunjika.

“Tunaomba mwongozo na kanuni za ushiriki wa wabunge hawa wa viti maalumu kwa kuwa wamechangia kuvunjika kwa uchaguzi,” alisema Waitara.

Aliwataja wabunge wa CCM kutoka Zanzibar walioshiriki katika baraza hilo kuwa ni Angelina Malembeka, Amina Ally, Mwantumu Haji na Asha Abdallah.

Alisema wabunge hao waliungana na wenzao wa viti maalumu Bara na kusababisha idadi ya wabunge wa CCM kufikia tisa na wale wa Ukawa kutoka Bara kuwa watano.

Hata hivyo, alisema baraza lililovunjika juzi lilikuwa na kasoro kwa kuwa wajumbe hawapewi uhuru wa kuchagua.

 

Wakati huohuo, mwandishi wetu kutoka mkoani Rukwa anaripoti kuwa kikao cha Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kimevunjika baada ya madiwani wanaotokana na Chadema kupinga wabunge wa viti maalumu wa CCM kutoka nje ya mkoa huo kuwa wajumbe na kushiriki uchaguzi wa kumchagua meya.

Katika kikao hicho, CCM kiliwasilisha kwa uongozi wa halmashauri ya manispaa hiyo majina mawili ya wabunge wawili wa viti maalumu ambao ni Anna Lupembe kutoka Katavi na Mwanne Nchemba kutoka Tabora, huku Chadema wakiwasilisha jina la Lucy Mlowe kutoka Njombe.

Kikao hicho kilichofanyika ukumbi wa manispaa hiyo, kilivunjika jana saa sita mchana baada ya mvutano wa zaidi ya saa tatu kati ya madiwani wa CCM na Chadema, huku kila upande ukitaka matakwa yao yatimizwe.

Madiwani wa Chadema wakiongozwa na mbunge wa viti maalumu kutoka Rukwa, Aida Khenan, walihoji ni kanuni zipi zimetumika kuwapokea na kuwahalalisha wabunge wa viti maalumu wanaotoka nje ya mkoa huo kuwa wajumbe wa kikao hicho kisha waruhusiwe kupiga kura.

Akijibu hoja ya mbunge huyo wa Chadema, Mwanasheria wa Halmashauri hiyo, Tulelemwa Mwenda, alisema viti maalumu ni wabunge wasio na jimbo, hivyo majina yakishatolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), chama husika humpanga mbunge wake katika eneo la kwenda kufanya kazi kwa kipindi cha miaka mitano.

Mwanasheria huyo alikwenda mbali zaidi kwa kueleza kuwa baada ya kupokea jina la Lucy iliwalazimu kuhoji uhalali wake wa kuhudumia Jimbo la Sumbawanga Mjini wakati yeye ni mbunge anayetokea Njombe na ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ilieleza kuwa sheria inampa uhalali wa kuchagua halmashauri yoyote atakayodumu kama diwani kwa kipindi cha miaka mitano, hivyo hata wabunge wa viti maalumu wa CCM wako sahihi kuhudumia katika halmashauri hiyo.

Kauli ya mwanasheria huyo ilipokelewa kwa mtizamo tofauti na Diwani wa Chadema, Vitalis Ulaya, aliyetaka meza itumie busara kuwatoa wabunge wote wa viti maalumu kutoka nje ya mkoa huo ili wajisajili na waweze kupiga kura.

Hata hivyo, Ulaya alipingwa na Mbunge wa Sumbawanga Mjini (CCM), Aeshi Hilaly, aliyedai Chadema walikuwa wa kwanza kumleta mbunge kutoka nje ya mkoa huo wakifikiri wataizidi kete CCM.

Pia Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Himidi Njovu, alitoa ufafanuzi wa kisheria na kanuni mbalimbali, lakini wajumbe (madiwani) wa Chadema wapatao 16 waligoma kujisajili na kusababisha akidi ya wanaopaswa kupiga kura kutotimia na kutangaza kuahirisha kikao hicho hadi atakapokiitisha tena ndani ya siku saba.

Naye Mwandishi Wetu kutoka Arusha anaripoti kuwa madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Karatu wamegoma kuapishwa kutokana na kitendo cha NEC kuongeza jina la ziada la diwani wa viti maalumu kupitia CCM.

Inadaiwa kuwa Emilian Titus ndiye aliyeongezwa kinyemela na NEC na hatua hiyo imeibua mgogoro uliosababisha kikao hicho kuvunjika.

Akizungumzia kitendo hicho, Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Chadema, Cecilia Pareso, alisema kwa mujibu wa sheria idadi ya viti maalumu vya madiwani ni moja ya tatu ya idadi ya kata katika halmashauri husika.

Alisema kutokana na hesabu hizo, Chadema Wilaya ya Karatu ilishinda jumla ya kata 14 na hivyo ina haki ya kupata  madiwani watano wa viti maalumu.

Alisema NEC iliandika barua ya kwanza ikiwa na majina matano kwa maana ya  mchanganuo wa Chadema nafasi tatu na CCM nafasi mbili.

“Tulipinga barua hiyo, kisha wakaleta barua ya pili iliyoteua madiwani watano kwa maana ya CCM mmoja na Chadema.

“Juzi wameleta barua tena ya kufanya uteuzi upya yenye jumla ya majina sita, ambapo sasa wamepanga Chadema wanne na CCM wawili, hatua hii bado tunaipinga kwa kuwa NEC inavunja taratibu na sheria. Hivyo tumekataa kuapishwa hadi sheria itakapofuatwa kwa kupata haki ya nafasi tano na siyo sita,” alisema Pereso.

Akizungumzia hatua ya kuvunjika kwa kikao hicho, Mkurugenzi wa Manispaa ya Karatu, Moses Mabula, alisema:

“Kikao kimeahirishwa baada ya madiwani wa Chadema kulalamikia kuongezwa kwa jina la diwani wa viti maalumu wa CCM. Kwa sasa nasubiria uamuzi kutoka NEC, wao ndio watakaonipa mwongozo wa nini kifanyike.”

Habari hii imeandikwa na Christina Gauluhanga (Dar es Salaam), Eliya Mbonea (Arusha) na Walter Mguluchuma (Rukwa).

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles