Ramadhan Hassan -Dodoma
SHIRIKA la Umeme nchini (Tanesco) linatekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Kinyerezi, Dar es Salaam hadi Dodoma kupitia Chalinze mkoani Pwani.
Wizara ya Nishati ililiambia Bunge jijini hapa jana wakati ikijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Mary Muro (Chadema), ambaye alihoji ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi wa Kibaha mkoani Pwani waliopisha ujenzi wa umeme wa msongo wa KV 400.
“Serikali ilishafanya uhakiki kwa wananchi wa Kibaha waliopisha ujenzi wa umeme wa msongo wa KV 400,” alisema mbunge huyo.
Wizara hiyo ilifafanua mradi huo unahusisha pia ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Kibaha hadi Zinga Bagamoyo.
Ilieleza kuwa mradi huu unalenga kuimarisha mfumo wa kusafirisha umeme nchini ikiwa ni pamoja na kusafirisha umeme kutoka mradi wa umeme wa megawati 2,115 – Mwalimu Nyerere (JNHPP).
“Mheshimiwa Spika, mradi huu unahusisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 400 yenye urefu wa takribani kilometa 600 kutoka Kinyerezi – Chalinze kilometa 100, Chalinze – Rufiji kilometa 160 na Chalinze – Dodoma kilometa 340,” ilisema wizara hiyo.
Ilisema mradi unahusisha pia ujenzi wa kilometa 40 njia ya umeme msongo wa kilovoti 220 kutoka Kibaha hadi Zinga Bagamoyo. Mradi huu utaenda sambamba na ujenzi wa vituo vya kupoza umeme vya Chalinze na Zinga.
Wizara ya Nishati ilibainisha kuwa mwaka 2015 hadi 2016 kazi ya uthamini wa mali za wananchi kutoka Kisarawe, Kibaha hadi Chalinze ilifanyika ili waweze kulipwa fidia na kupisha ujenzi wa mradi.
Ilisema hadi kufikia mwezi Machi, 2020 taratibu zote za uandaaji taarifa na majedwali ya fidia zilikamilika. Jumla ya fidia kwa maeneo kati ya Kiluvya (Kisarawe) hadi Chalinze ni Sh bilioni 21.569.