24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, April 14, 2024

Contact us: [email protected]

UMEJIPANGAJE KUUKABILI MWEZI WA MIKIKIMIKIKI?

Na ATHUMANI MOHAMED

KWA kawaida mwishoni mwa mwaka huwa na shamrashamra za kila aina. Wengi mifuko yao huwa imetuna! Hawana wasiwasi na fedha.  Ni mwezi wenye matukio mengi ya sherehe.

Huyu anafunga ndoa, wengine watoto wanapata kipaimara, wengine wako likizo kwa mapumziko nk. Kifupi ni mwezi uliochangamka sana. Nazungumzia mwezi wa mwisho katika mwaka – Desemba.

Kwa waajiriwa ni mwezi ambao mishahara huwaishwa. Wapo wanaopokea tangu tarehe 15 au zaidi ya hapo lakini ni kabla ya Krismasi. Hata hivyo kwa kuwa fedha zinatoka mapema, matumizi huwa mengi, Januari huwa ni kilio!

Hata wale wanaojiajiri na wafanyabiashara, miezi miwili mpaka mitatu ya mwisho wa mwaka, biashara huchanganya. Katika kuchanganya huko, pia matumizi yao hubadilika hasa kwenye kipindi cha sikukuu (zaidi Krismasi na Mwaka Mpya).

Kasheshe ni Januari ambayo ratiba hubadilika, badala ya kupata fedha mwisho wa mwezi Desemba, majukumu mengi yanakuwa mbele yake. Kuna ada za watoto shule, mitaji ya biashara, kusafirisha wageni na mengineyo.

Hata hivyo, zipo mbinu nzuri kabisa, ambazo zitakusaidia kuvuka salama mwezi Januari na kuendelea na mipango ya maisha yako sawasawa.

Hakuna kitu kipya kinachotokea katika mwezi huo, bali ni utaratibu na mazoea ya kusahau au kuacha mambo yajipeleke yenyewe, jambo ambalo kamwe haliwezekani.

Hebu tuangalie japo kwa dodoso tu, namna ya kuishi vyema mwezi Januari na kuweka mipango yako sawasawa.

JIFUNZE MAKOSA YA DESEMBA

Kama nilivyotangulia kusema, wengi hutumia fedha vibaya mwezi Desemba na kusahau majukumu au ukata ambao atakutana nao Januari. Kwako iwe funzo. Hata kama uliharibu fedha nyingi kwa ajili ya anasa tu, tulia.

Usijiumize, achana na mambo yaliyopita lakini iwe fundisho kwa miaka mingine inayofuata ukianza na huu, kama ukijaaliwa. Acha kutumia fedha zote mwezi Desemba kama vile hutakuwa na matumizi ya muhimu Januari.

Kama nilivyosema, hapa ni kukumbushana na kujifunza kwa ajili ya sasa na wakati ujao.

ANGALIA VIPAUMBELE

Kwa kawaida ukitaka kuvuka salama mwezi Januari, kuwa na vipaumbele. Angalia mambo ya msingi ambayo lazima uyashughulikie haraka. Mfano ada za watoto nk.

Hayo ni mambo muhimu ambayo hayawezi kusubiri. Andika mahali ili ujue namna ya kuanza kushughulikia moja baada ya lingine.

BANA MATUMIZI YAKO

Bana matumizi yako kabisa. Kama nilivyotangulia kusema hapo awali, katika kubana huko ni pamoja na kuangalia vipaumbele vyako. Usitumie fedha kwenye mambo ambayo si ya lazima.

Kwa mfano kama ulikuwa na mazoea ya kukodi taksi – acha, panda daladala ili uweze kwenda na kasi ya matumizi na fedha kidogo ulizonazo.

Achana na kukodi bodaboda, bajaji au taksi kwenye sehemu fupifupi – tembea kwa miguu. Kumbuka huna fedha na mahitaji yako ni makubwa. Kuruhusu matumizi wakati huingizi tafsiri yake ni kushindwa kuvuka salama mwezi Januari.

Si lazima ule hoteli, safari hii jifanye hohehahe, nenda kwa mama lishe. Usiogope macho ya watu. Kwa bahati nzuri, watu wala huwa hawana haja ya kufuatilia maisha yako. Ishi kama wewe, usiongozwe na macho ya watu.

Wako katika mafanikio, naitwa Athumani Mohamed, wiki ijayo tutamalizia mada yetu, USIKOSE! Wasalaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles