28.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

KUFANYA VIDEO ZA NUSU UTUPU NI KUTOJIAMINI

Na RAMADHANI MASENGA

MHESHIMIWA Rais, Dk. John Pombe Magufuli ameonesha kuchukizwa na hali ya kinadada wanavyovaa wakiwa katika video za muziki.

Ameshangaa ni kwanini wanaume mara nyingi wanavaa mavazi ya staha huku wanawake wakivaa mavazi ya kuanika maungo yao.

Tamko la Rais ni agizo. Bila shaka mamlaka zinazohusika zimelibeba suala hilo katika akili zao na litazifanyia kazi. Baada ya tamko hilo la Rais nimefuatilia kwa karibu mwitikio wa wananchi.

Wengi wanaonekana kumuunga mkono. Wengi wanasema hali ilikuwa ni mbaya sana. Baadhi wakafika mbali zaidi na kusema ilifikia hatua walikuwa wakitaka kuwazuia watoto wao kuangalia muziki wa Tanzania kwa sababu mavazi ya kinadada wengi yalikuwa yakifanya watoto wao nao watamani kuvaa vile wakati ni kinyume kabisa na maadili.

Ni kweli muziki unahitaji ubunifu. Ila ni kwanini ubunifu huo uwe katika kuweka maungo ya kinadada wazi? Hakuna ubunifu mwingine katika video za muziki?

Miaka kumi iliyopita wazazi walikuwa hawataki watoto wao watazame muziki wa Kimarekani kwa hofu ya kuharibika kimaadili kwa sababu ya mavazi na mashairi yao. Ila sasa tunaenda kufikia hatua kuogopa muziki wa Kitanzania kuliko wa Kimarekani.

Sikiliza mashahiri ya vijana wa sasa. Angalia mavazi na aina ya maigizo wanayofanya katika video zao za muziki. Ni uchafu mtupu.

Muziki ni njia nyepesi sana kueneza chochote. Kupitia muziki ukitaka kusaficha maadili, utafanya hivyo. Ila pia kupitia muziki ukitaka kuchafua maadili utafanikiwa.

Leo mavazi ya wasichana wengi mtaani yanatia aibu. Sababu  ya yote hayo inajulikana. Akina Vanessa Mdee na wenzao wamefanya maadili ya mavazi kwa kinadada yakose muelekeo.

Hili suala halitakiwi kwenda mbali zaidi. Hongera mheshimiwa Rais kuonesha kuwa unafuatilia kila kitu na kweli unahitaji Tanzania mpya kwenye kila idara.

Taifa lisilo na maadili ni taifa mfu. Kama Watanzania, kwa faida ya maendeleo ya muziki wetu na vizazi vijavyo ni lazima tuzingatie suala la maadili.

Tathimini inaonesha kuanika maungo hakuna uhusiano wowote na uzuri wa video. Kuna nyimbo nyingi tumewahi kuzisifia kwa sababu ya video nzuri ila ndani yake hakuna mavazi ya kumfedhehesha mwanamke.

Nyimbo kama My Number One wa Diamond Plutnumz na Pacha Wangu wa Rich Mavoko ni nyimbo nzuri na video zake zimesifiwa sana, ndani yake maadili yamezingatiwa.

Unapofanya video ya wimbo ambao ndani yake kuna uvunjifu mkubwa wa maadili, unagawa watazamaji. Utafanya wastaarabu na walinzi wa maadili waikwepe na kuachia wale wa oyaoya pekee ndiyo waitazame.

Ila kufanya video za nusu utupu unaifanya jamii ijikite zaidi katika imani kuwa muziki ni shughuli za wahuni na makahaba.

Kuna haja kubwa wasanii kukaa na kujitafakari. Inabidi wasanii wajitafakari kwa manufaa ya muziki wao na taifa lao. Japo baadhi wanajiona tayari ni wasanii wakubwa wa kimataifa ila wajue thamani na ubora wao ulianzia nyumbani hivyo basi wanapaswa kuheshimu maadili ya taifa lao.

Yemi Alade na wasanii kutoka nchini Mali ni baadhi ya wasanii wanaofanya vizuri sana katika soko la kimataifa huku wakiwa bado wanauhifadhi utu wao.

Kufanya video za nusu utupu mbali na mambo mengine ni ishara ya kutojiamini. Wanaona mashairi na matendo mengine mazuri ya video hayatavuti hisia za watazamaji mpaka wapambue nguo zao na kuweka wazi yanayofaa kuwa siri.

Tubadilike!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles