25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

MASTAA WALIOAGA UKAPERA 2017

Na BADI MCHOMOLO

KATIKA maisha ya kawaida kila mwaka watu wanajiwekea mikakati juu ya vitu vya kufanya kabla ya mwaka kumalizika, wapo ambao wanafanikiwa na wengine wanashindwa kutokana na mambo yaliyo nje ya uwezo wao.

Kesho ni siku ya mwisho kwa mwaka 2017, leo katika safu hii tunaangalia baadhi ya mastaa waliofanikiwa kukamilisha mipango yao ya kuuaga ukapera.

GUCCI MANE, KEYSHIA

Wawili hao walikuwa kwenye uhusiano kwa kipindi kirefu, lakini mipango ya kufunga ndoa iliwezekana kabla ya kumalizika kwa mwaka 2017.

Ilikuwa Oktoba 17, wawili hao waliweza kutimiza ahadi waliyopanga kwa kipindi cha uhusiano huo kwa kufunga ndoa katika Hoteli ya Four Seasons, iliyopo Miami nchini Marekani.

Kitu cha kushangaza kwenye harusi hiyo ni kwamba Gucci Mane ambaye ni msanii wa muziki wa Hip Hop, hakuweza kutoa mwaliko kwa mama yake mzazi na hata familia yake kwa ujumla, ila mwaliko alitoa kwa baadhi ya wasanii wa muziki huo.

Mama na kaka wa msanii huyo walitumia mitandao ya kijamii kumlalamikia msanii huyo kwa kitendo alichokifanya na inadaiwa harusi yake haikuwa na watu wengi sana.

STEVIE WONDER, TOMEEKA

Stevie ni staa wa muziki nchini Marekani mwenye umri wa miaka 67, mbali na kufanya vizuri katika muziki lakini ni kipofu wa macho kwa muda mrefu.

Aliwahi kufunga ndoa mara ya kwanza mwaka 1970 na mpenzi wake Syreeta Wright, lakini walikuja kuachana mwaka 1972.  Baadaye mwaka 2001 Stevie akafunga ndoa na mpenzi wake Kai Millard, kabla ya kuachana mwaka 2015.

Julai 19, mwaka huu aliamua kuachana tena na ukapera kwa kufunga ndoa na mpenzi wake Tomeeka Bracy, hivyo amekuwa kwenye maisha ya ndoa mara tatu.

TYESE, SAMANTHA LEE

Tyrese ni miongoni mwa wasanii wa muziki nchini Marekani ambao wana ngozi nyeusi na wamekuwa na mvuto mkubwa kwa wasichana.

Hakuna ambaye alikuwa anaamini kuwa msanii huyo anaweza kufunga ndoa kwa miaka ya hivi karibuni kutokana na hali yake ya kutotulia na msichana mmoja, amekuwa akibadilisha wasichana mara kwa mara, lakini aliweza kunasa katika penzi la mrembo huyo Samantha Lee.

Hata hivyo ndoa hiyo ilikuwa ya siri sana hadi pale alipoweka wazi kuwa tayari amefunga ndoa na kusambaza picha zao kwenye mitandao ya kijamii.

Picha hizo zilisambazwa mwezi mmoja baada ya ndoa hiyo iliyofungwa Februari 14, ikiwa ni Sikukuu ya Wapendanao duniani kote.

MORGAN EVANS, KELSEA

Hao ni nyota wa muziki kutoka nchini Marekani, walianza kuweka wazi uhusiano wao tangu siku ya Krismasi mwaka jana.

Mapema mwaka huu waliamua kutangaza kuwa wapo kwenye mipango ya kufunga ndoa, hivyo Desemba 2 kabla ya kumalizika kwa mwaka 2017 waliamua kutimiza ahadi yao kwa kufunga pingu za maisha.

JORDIN SPARKS, ISAIAH

Jordin ni nyota wa muziki nchini Marekani, aliweza kujizolea umaarufu wake baada ya kutwaa taji la American Idol mwaka 2006, lakini awali alikuwa anashiriki mashindano mbalimbali, ila shindano hilo liliweza kumtoa na kuwa msichana mdogo kushinda kwa mara ya kwanza akiwa na miaka 17.

Awali alikuwa kwenye uhusiano na nyota wa muziki Jason Derulo, lakini baada ya kuachana akaamua kutoka na Dana Isaiah na hatimaye mwaka huu wakafanikiwa kufunga ndoa.

Wawili hao kwa sasa wanatarajia kupata mtoto wao wa kwanza mapema mwakani. Hao ni baadhi ya mastaa walioagana na ukapera mwaka 2017 majuu.

Nawatakieni nyote Heri ya Mwaka Mpya 2018

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles