27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

Umejiandaaje na miezi ya matumizi?

shopping

Na ATHUMANI MOHAMED

LEO ni Novemba 12, siku zinakwenda kwa kasi sana. Bado takribani siku 18 kuufikia mwezi wa mwisho katika mwaka, Desemba ambao kwa kawaida una mfululizo wa sikukuu za mwisho wa mwaka.

Kumbuka kwamba Desemba kuna sikukuu ya Krismasi na baadaye panapo majaliwa Mwaka Mpya, kisha kufuatiwa na mambo chungu nzima ya kodi za nyuma, ada za watoto shule n.k.

Kimsingi ni miezi ya fujo za matumizi. Kwa wafanyakazi ni nyakati hatari zaidi. Kipindi hiki cha mwisho wa mwaka, wengi huchukua likizo zao.

Ukiacha sherehe hizo, pia huwa na sikukuu nyingine za watoto wanaopata kipaimara na mengine kama hayo. Kwanini kwa wafanyakazi ni hatari zaidi?

Ni kwa sababu maofisi mengi huamua kulipa mishahara mapema kwa lengo la kuwasaidia wafanyakazi kufurahia sherehe hizo.

Mara nyingi, kwa kampuni zinazochelewesha sana mishahara, hulipa si zaidi ya tarehe 20 ya mwezi Desemba. Kumbuka hapo, ukifanya matumizi yako mpaka kufikia tarehe Mosi mwaka ujao, utakuwa huna kitu.

Wakati ukiwa huna kitu mfukuni, kuna mambo ya ada za watoto wanaofungua shule na mahitaji mengine muhimu kama nilivyoeleza hapo juu.

Hapo sasa ndipo mwanzo wa kufungua mwaka na madeni kila kona. Ilivyo ni kwamba, ukifungulia madeni mwezi Januari, maana yake mwaka mzima utakuwa na kazi ya kulipa madeni.

Usisahau kuwa kwa sasa kama mshahara, unategemea wa mwezi huu (Novemba) na Desemba ambao huwahi, kisha utasubiri kwa siku takribani 45 (badala ya 30) ili kuufikia mshahara mwingine wa mwezi Januari.

CHANGAMSHA BONGO

Ndugu zangu, si kwamba sikukuu zimekuja kwa haraka au ghafla; la hasha! Kwa kawaida mwaka una miezi 12, hivyo lazima uanze wa kwanza hadi unapokutana tena na mwingine wa kwanza mwaka unaofuata.

Tulikuwa na Januari na sasa tuna Novemba, tukiutafuta Desemba. Hakuna ajali wala kushtukizwa hapo. Lakini inawezekana ulikuwa ukiishi mradi siku zinakwenda na hukujiandaa kabisa na miezi hii ya matumizi, mada hii itakufaa sana.

Pamoja na kwamba umebaki muda mdogo ili kufikia sikukuu hizo za mwisho wa mwaka, dondoo nilizokuandalia katika mada hii zinaweza kukupa mwanga wa nini cha kufanya.

Ukifuatilia kwa makini utajifunza vitu vya msingi.

ANDIKA MAHITAJI YAKO

Kitu cha kwanza kuzingatia ambacho kitaweza kukusaidia ni kujua mahitaji yako kwanza. Andika mahitaji yako yote muhimu.

Kama una familia ni vizuri kupanga na mwenzi wako; andika vitu vyote muhimu. Mfano vyakula, mavazi ya watoto, nauli za kwenda likizo, ada kwa ajili ya mwakani, vifaa vya shule nk.

Hili ni zoezi la kwanza lenye umuhimu. Wakati unaandika mahitaji yako hayo, ni vizuri kuanza na yale muhimu zaidi ambayo ni ya lazima.

 ANZA NA YA MUHIMU

Kuna vitu ambavyo ni muhimu na haviwezi kuharibika. Mfano mabegi ya watoto shule na steshenari (vitabu, madaftasi, kalamu nk), sare za shule na mengine. Anza kutekeleza hayo mapema.

Kama unazo pesa, hata leo unaweza kuamua kununua madaftari ya mtoto mmoja (kama unaye zaidi ya mmoja), kisha wiki ijayo ukanunua ya mwingine, hadi utakapowakamilishia wote.

Hii itakusaidia kutokuwa na presha ya kufanya mambo kwa haraka, hasa wakati ambao mfukoni utakuwa mkavu.

 

Somo letu litaendelea wiki ijayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles