27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Umejiandaaje na miezi ya matumizi? – 2

atmcardpicha

Na ATHUMANI MOHAMED

TUNAKARIBIA mwisho wa mwaka, mambo mengi sana. Kimsingi tunahitaji kuwa na fedha lakini pia mahitaji yakiwa mengi zaidi pengine kuliko kipindi chochote katika mwaka.

Mwishoni mwa mwaka huwa na sikukuu nyingi, wakati huohuo mahitaji mengi muhimu. Watu hulia na miezi ya Desemba na Januari kama vile imekuja kwa ghafla.

Habari nzuri kwako ni kwamba, ikiwa utakuwa umejipanga vizuri, kipindi hicho kinaweza kupita vizuri bila kukuachia adha kubwa kwenye matumizi yako.

Ilivyo ni kwamba, ikiwa utafanya matumizi yasiyo na hesabu katika kipindi hiki, ni rahisi kuanza mwaka mpya ukiwa mwenye madeni na misukosuko mingi na mwisho wake ni kwamba mwaka wako hautakuwa na chochote cha kujivunia.

Ni muhimu sana kuandika mahitaji yako muhimu na kupanga namna ya kuyafanyia kazi moja baada ya jingine. Kuandika kutakusaidia kujua nini uanze nacho na kipi kifuatie huku ukilinganisha umuhimu wa mahitaji husika.

BANA MATUMIZI

Katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye sikukuu za mwishoni na mwanzoni mwa mwaka, inakupasa uwe mwangalifu zaidi na matumizi yako.

Kumbuka siku za usoni utakuwa na uhitaji mkubwa zaidi wa fedha hivyo jitahidi kutunza fedha; fanya matumizi ya muhimu tu. Mfano kama ulikuwa unajiachia kwa matumizi makubwa sana, basi acha vile ambavyo si muhimu sana kama viburudisho nk.

WEKA MIPANGO YA FEDHA

Unapaswa kufanya mipango yako ya fedha vizuri. Je, hadi kufikia mwishoni mwa Desemba utakuwa na kiasi gani? Mfano kama ni mwajiriwa, lazima ujue kuwa utakuwa na mishahara ya miezi miwili tu (Novemba na Desemba) kwa sasa.

Ikiwa ni mfanyabiashara ni tofauti kidogo, ingawa pia ni rahisi kufanya makadirio. Pamoja na kujua kuhusu fedha zako, ni vizuri pia ukafikiri namna ya kupata kipato cha ziada kwa kipindi hiki.

Kama hujawahi kufikiria jambo hili huko nyuma, hiki ni kipindi unachotakiwa kufikiria jambo hilo zaidi kuliko wakati mwingine, maana uhitaji wako wa fedha ni mkubwa zaidi.

Ikiwa una mpango wa kusafiri kwa ajili ya mapumziko, fanya utafiti juu ya bidhaa zinazopendwa katika eneo unalokwenda, nenda zako.

Mfano labda kwenu ni vijijini huko, unaweza kutafiti na kwenda na nguo za watoto au simu za bei nafuu, ikakusaidia kuongeza kipato wakati huu ambao una mahitaji makubwa zaidi.

TENGENEZA BAJETI

Mali bila daftari hutumika bila habari. Ni muhimu sana kuwa na bajeti ya mahitaji yako yote. Ujue fedha gani utatumia kwenye kitu gani.

Ni hatari sana kufanya matumizi ya zimamoto, wanaotumia fedha bila mpangilio hujikuta ghafla wakiwa hawana kitu na tayari sikukuu zinakuwa mlangoni au zimeisha lakini majukumu mengine ya muhimu yakiwa mbele yao.

KUWA MAKINI NA MATUMIZI

Heshimu mipango yako, tumia fedha zako kwa makini ukihakikisha kila ulichopanga kinakwenda vilevile bila kubadilisha kitu.

Nidhamu ya matumizi ni kati ya vitu muhimu ambavyo vitakusaidia sana kupita katika kipindi kigumu vema bila kupata usumbufu wowote kifedha.

Nakutakia maandilizi mema ya sikukuu za mwisho na mwanzo wa mwaka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles