ALLY BADI, KILWA
UMASIKINI wa kipato,kilimo cha kuhamahama kwa baadhi ya wazazi na walezi kudaiwa kunachangia watoto wasiandikishwe shule na uwapo wa maendeleo duni ya ufaulu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi.
Hayo yamesemwa wakati wa  utafiti uliofanywa na Shirika la Action Aid na kuwasilishwa mtafiti, Jacob Kateri katika kikao kazi na wadau wa elimu kilichofanyika Kilwa masoko,chini ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Christopher Ngubiagai.
Akiwasilisha ripoti hiyo juzi, Kateri alisema utafiti uliofanywa kati ya shirika hilo na Mtandao wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali la Wilaya ya Kilwa (KINGONET),umebaini uwapo wa changamoto mbalimbali zikiwemo za umasikini wa kipato.
Alisema kitendo cha wazazi na walezi kutotambua na kuthamnini umuhimu wa elimu,kunachangia washindwe kuchangia kuinua kiwango cha elimu, ikiwemo pamoja na kujitokeza kushiriki,kujenga nyumba za kuishi walimu,vyumba vya madarasa na vyoo.
Alisema umasikini wa kipato kwa baadhi ya wazazi na walezi kunachangia wanafunzi wanaosoma shule mbalimbali, zikiwamo za msingi na sekondari washindwe kuwapatia vijana wao mahitaji muhimu kama vile chakula na gharama zingine.
Alisema sababu nyingine kuendelea kwa adhabu ya viboko kwa wanafunzi ni changamoto zilizopo katika shule z wilaya humo, kwani kati ya Shule (15) zilizokuwa zimefanyiwa utafiti (14) zimeelezewa ni suala la kawaida,shule tatu zimetaja uwapo ukatili wa kingono na ukatili wa kimwili.
Alisema  upungufu wa walimu na wengine kuishi mbali na maeneo yao ya kazi,nalo ni tatizo walilobaini na kuomba uongozi husika kulifanyia kazi.