22.2 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

Ronaldo mti wenye matunda unaopigwa mawe

Cristiano Ronaldo
Cristiano Ronaldo

ADAM MKWEPU NA MITANDAO,

KWA muda mrefu Cristiano Ronaldo amekuwa suluhisho la mafanikio ya timu ya Real Madrid licha ya kukumbana na  changamoto mbalimbali ikiwamo kukosolewa na baadhi ya mashabiki wa timu hiyo.

Tangu uanze msimu huu nyota huyo ameonekana kutokuwa katika kiwango bora hali ambayo imesababisha kuitwa mzigo pia chanzo cha timu hiyo kufanya vibaya sambamba na kupata matokeo ya sare katika michezo minne mfululizo ya Ligi Kuu ya Hispania ‘La Liga’.

Kucheza bila mipango huku wakiwa chini ya kiwango tangu msimu uanze, ndio sababu ya kocha wa zamani wa timu hiyo, Fabio Capello kudai kuwa Ronaldo ni tatizo na chanzo cha timu hiyo kufanya vibaya.

Licha ya kauli ya Capello kuonekana kuwa kali kwa nyota huyo ambaye msimu uliopita alikuwa mfungaji bora, huenda ilikuwa ikimaanisha kuwa kuna tatizo kubwa la kimbinu ndani ya kikosi cha kocha Zinedine Zidane na wachezaji wake.

Kikosi hicho kwa sasa kimekosa mbinu mbadala uwanjani na kumfanya nyota huyo kushindwa kung’aa licha ya kuonekana bado anasumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu aliyopata katika michuano ya Euro 2016.

Lakini hiyo haitoshi kutomshushia lawama nyota huyo ambaye ndio hubeba mafanikio ya timu hiyo katika mabega yake, haikushangaza kumuona Capello akisema nyota huyo huenda akarejea upya baada ya michezo ya kimataifa.

Siku mbili baada ya maneno ya Capello nyota huyo amemjibu kocha huyo kwa kufunga mabao manne katika ushindi wa mabao 6-0 wa timu ya Ureno dhidi ya timu ya taifa ya Andora.

Kiwango alichokionesha katika mchezo huo kinawapa matumaini mashabiki wa timu yake wakiamini kuwa huenda akarejesha ubora wa timu ya Real Madrid watakapokutana na vijana wa Gus Poyet, Real Betis wiki ijayo.

Ronaldo ana mabao matatu katika michezo sita ya La Liga msimu huu ambao umeonekana kuwa mbaya kwake uliomfanya kuanza kwa lawama kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo.

Mbali na mambo mengine, kitendo cha nyota huyo kuonesha kuchukizwa kutolewa uwanjani katika mchezo dhidi ya Las Palmas labda ni ishara kwamba amekuwa katika msongo wa mawazo kutokana na kushindwa kuibeba timu hiyo kama ambavyo Zidane anavyomtaka kufanya.

Kwani Madrid walifanikiwa kushinda bila ya Ronaldo na kupoteza pointi mbili katika michezo miwili kati ya minne ambayo hawakuwa na matokeo mazuri.

Lakini Ronaldo alirejea katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya timu ya Borussia Dortmund, ambao alifanikiwa kufunga bao na kutoa pasi ya bao licha ya kushindwa kulinda ushindi huo na kusababisha kutoa sare ya mabao 2-2.

Hatua ya kupata sare katika michezo minne inamaanisha kwamba kocha wa timu hiyo Zidane yupo katika presha.

Mkurugenzi wa ufundi wa timu hiyo, Emilio Butragueno, amedai kuwa tayari baadhi ya watu ambao wapo karibu na rais wa klabu hiyo, Florentino Perez wameanza kumfanya rais huyo awe na presha kutokana na mwelekeo wa timu hiyo.

Zidane anahitaji kiwango cha Ronaldo kurejea haraka kwa kuwa anajua umuhimu wa nyota wakati akiwa katika ubora wake.

Ronaldo pia anahitaji Zidane kufanya aliwezalo kutumia mbinu zake kuboresha safu ya ushambuliaji Gareth Bale, Karim Benzema, ili kupata matokeo mazuri.

Lakini Zidane aliwahi kusema kwamba kama wachezaji wake wa safu hiyo ya ushambuliaji wakiwa katika ubora wao hakuna wa kuwazuia.

Kusuasua huko kunamfanya Zidane  kukiri kuwa ipo siku atatupiwa virago kama hajafikia malengo ya klabu hiyo.

Nyota huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa aliiongoza Madrid kutwaa taji lao la 11 Ligi ya Mabingwa msimu uliopita akiwa kocha wa timu hiyo kwa mara ya kwanza, amesisitiza kuwa haogopi kutupiwa virago na Los Blancos.

“Nafurahia vilivyo kile nikifanyacho nina fursa ya kipekee. Naipenda kazi yangu ambayo si rahisi mara zote, lakini nataka kujifunza kuwa bora zaidi.

“Najifunza kila siku kufanya kazi na wachezaji bora. Nina kikosi cha kipekee, iwe tunashinda au kushindwa bado ni wachezaji wema,” anasema Zidane.

Madrid hawajawahi kutoa sare mechi nne mfululizo kwa kipindi cha miaka 10 kabla ya hili kutokea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,415FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles