30 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

UMAKINI UNAHITAJIKA UJENZI JENGO LA TATU JNIA

WIKI hii Rais Dk. John Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza na kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la tatu la abiria (Terminal III) lililopo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Katika mradi huo unaogharimu kiasi cha Sh bilioni 560, Magufuli, aligundua kuna kasoro ikiwamo gharama za mradi kuwa kubwa ikilinganishwa na mradi wenyewe pamoja na kutolipwa kwa wakati mkandarasi wa Kampuni ya BAM kutoka Uholanzi inayojenga jengo hilo.

Kutokana na hilo, alimwagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, kuunda upya timu ya watu watakaofanya tathmini, kusimamia mradi huo pamoja na kuzungumza na mkandarasi ili kuangalia uwezekano wa kupunguza gharama hizo.

Tayari Mbarawa ametii agizo hilo na kuunda timu mpya ya wataalamu saba inayoongozwa na Mhandisi Julius Ndyamukama, wengine ni Mhandisi Godson Ngomuo, Mhandisi Humphrey Kanyenye, Mhandisi Abednego Lyanga, Mhandisi Mbila Mdemu na Mhandisi  Rehema Myeya.

Katika taarifa yake, Mbarawa, aliihakikishia Kampuni ya BAM kuwa Serikali itamlipa mkandarasi huyo katika kipindi cha wiki mbili kutoka sasa huku akiitaka timu hiyo kuhakikisha ujenzi wa jengo hilo unakamilika Desemba, mwaka huu kama ilivyopangwa.

Sisi wa MTANZANIA Jumamosi tuna imani kubwa kuwa timu hiyo yenye wataalamu mahiri, itasimamia ujenzi huo kwa umakini mkubwa, uzalendo na kwa masilahi mapana ya nchi hadi utakapokamilika kwa wakati kama ilivyokusudiwa na kuzingatia thamani ya fedha kama Mbarawa alivyosema.

Tuna imani pia kuwa hadi kufikia muda uliopangwa, ujenzi huo utakuwa umekamilika na kuufanya uwanja wetu wa ndege kuwa bora zaidi ya ulivyo hivi sasa na kusababisha idadi ya abiria kuongezeka.

Pia tuna imani kuwa kasi ya Serikali ya Magufuli inafahamika kwamba hataki uzembe, kwa hiyo tuna imani kila aliye katika timu ya kusimamia ujenzi huo atajituma na kuhakikisha kuwa unakamilika pasipo kuwepo tumbua tumbua tena.

Hatutarajii kusikia kuwa ujenzi huo umeshindwa kukamilika kwa wakati kutokana na sababu zilizo ndani ya uwezo wetu.

Tunaamini kila mmoja atajituma kulingana na mahali alipo na hata wale ambao wako katika miradi mbalimbali ya maendeleo kama hiyo, wakumbuke kuikamilisha kwa wakati badala ya kusubiri kuja kusukumwa au kutumbuliwa.

Tuna imani kuwa kila Mtanzania akisimama vyema katika nafasi yake na kutekeleza majukumu yake ipasavyo, nchi hii itafika mbali zaidi kiuchumi, viwanda na biashara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles