28.6 C
Dar es Salaam
Saturday, January 28, 2023

Contact us: [email protected]

‘BRAND’ ZETU TUTAZIJENGA KWA KUCHAPA KAZI TU

NA CHRISTOPHER MSEKENA

MOJA ya kazi kubwa ambayo inatumia muda, fedha, kutokukata tamaa na wakati mwingine kipaji, juhudi na kumwomba Mungu bila kuchoka, ni pale unapotaka kujenga jina kwenye jamii inayokuzunguka. Kutengeneza ‘Brand’ si kitu kidogo, kwani huu ndio wakati ambao usipojitambua, ukajitoa basi safari yako itaishia njiani.

Unaweza kuwa mwanasiasa ila usiwe na jina kubwa. Itakulazimu kufanya siasa safi, kuibua mambo na changamoto kadha wa kadha ambazo zitakuza jina lako miongoni mwa wanajamii, hivyo kuwa na ‘brand’ yako pekee isiyofanana na mtu mwingine yeyote.

Hali kadhalika unaweza kuwa mwanamichezo, mfano unacheza soka ili ujitengenezee ‘brand’ yako ni lazima uwe na aina ya uchezaji utakaokutofautisha na wacheza soka wengine, ndiyo maana leo hii soka analolicheza Messi huwezi kulifananisha na lile la Ronaldo au Mbwana Samatta halilingani na la Thomas Ulimwengu, japo kuwa wote ni wakali na wana heshima kubwa kwenye soka.

Tukirudi kwenye burudani pia kuna wasanii ambao wanajulikana harakati zao za kujitengenezea ‘brand’ kabla hawajawa walivyo hivi sasa. Kwenye muziki kuna watu kama kina Diamond Platnumz ambaye ana utambulisho wake pia na muziki wa kipekee.

Hivyo hivyo kwa Ali Kiba, ni msanii mkubwa mwenye muziki wa kipekee ambao haufanani na yeyote, hiyo yote ilikuja baada ya kutambua ni namna gani wajitengenezea ‘brand’ zao. Na wote walishawahi kutoa jasho ili tu kutafuta nafasi walizonazo hivi sasa kwenye muziki wa Bongo Fleva.

Nani ambaye hajui jinsi marehemu Steven Kanumba alivyosota mpaka kufanikiwa kuipa heshima tasnia ya filamu? Si yeye tu, jaribu kufuatilia historia za kina JB, Ray, Johari, Lulu, Monalisa, Richie Richie na wengineo utabaini kuwa kutengeneza jina kwenye jamii si rahisi kama wengi tunavyofikiri.

Unahitaji uwekeze muda na nguvu katika kazi yoyote unayoifanya. Nimesema hivyo kwa sababu ‘brand’ ya mtu ndiyo inayomwezesha kupata dili kwenye kampuni mbalimbali. Kama unafuatilia vyema burudani utabaini hapa mjini kuna mastaa wakubwa ila hujawahi kuwaona kwenye tangazo hata moja.

Lakini utashangaa staa mmoja anafanya matangazo ya kampuni nyingi kwa wakati mmoja wakati mastaa wenzake hawana hata tangazo moja. Hapo ndipo linapokuja suala zima la kufanya kazi kwa bidii ili kujenga ‘brand’ inayouzika kirahisi kwenye ulimwengu huu uliotawaliwa na biashara kila sehemu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles