Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, ameagiza barabara zote zinazoingia Dodoma kulindwa kuanzia sasa wakati uchunguzi wa tukio la kupigwa risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), ukiendelea.
Amesema ameagiza Jeshi la Polisi kuimarisha ulinzi katika njia na barabara hizo ili ikiwezekana wahusika wakamatwe.
Aidha, akizungumzia tukio hilo nje ya Hospitali ya Mkoa wa Dodoma leo Septemba 7, Nchemba amesema tukio hilo halikubaliki kwa namna yoyote na limechafua nchi taswira ya nchi kwani Lissu anajulikana kama mwanasiasa mahiri.
“Naambiwa tayari ameshapatiwa huduma ya kwanza kuzuia damu isiendelee kuvuja tumboni na wamefanikiwa, kinachofuata sasa ni kuendelea na upasuaji,” amesema Nchemba.
Naye Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema madaktari wanaendelea kupambana na uwezo wanao wa kumtibu hapa nchini.
“Niwahakikishie tu anaendelea kupata matibabu na mmoja wa madaktari wanaomtibu ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, kama ikitokea dharura au sababu maalumu ndiyo tunaweza kumpeleka hospitali nyingine,” amesema Mwalimu.
Kwa upande wake Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema Ofisi ya Bunge itatoa ushirikiano na huduma yoyote pale itakapohitajika.