23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

YANGA NI MWENDO WA KIJESHI

ADAM MKWEPU Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

WAKATI Yanga ikiendelea kujifua vikali  ikisubiri kuivaa Njombe Mji Jumapili, habari njema kwa mashabiki wa timu hiyo ni kutoka kifungoni kwa kiungo wao, Pius Buswita.

Kiungo huyo alifungiwa kucheza soka kwa kipindi cha mwaka mmoja baada ya  kubainika kusaini timu mbili kwenye dirisha la usajili la msimu huu.

Hukumu hiyo ilitolewa na Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji baada ya kujiridhisha kuwa Buswita alisaini mikataba miwili tofauti ya kuzichezea timu za Simba na Yanga.

Kamati hiyo iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Richard Sinamtwa, ilimtia hatiani mchezaji huyo kwa kukiuka kanuni ya  66 ya Ligi Kuu  Tanzania Bara ambayo  adhabu yake ni kifungo cha mwaka mmoja.

Hata hivyo, Yanga ndiyo iliyowasilisha TFF jina la Buswita katika orodha ya wachezaji iliowasajili kwa ajili ya msimu huu wa ligi kuu kabla ya Simba kulilalamikia shirikisho hilo likidai kutapeliwa na mchezaji huyo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji, Elias Mwanjala, alisema klabu hizo mbili zimekubaliana Buswita airejeshee Simba kitita cha Sh milioni 10 alizopewa baada ya kusaini mkataba na baada ya hapo aendelee kuichezea timu yake ya sasa ya Yanga.

“Simba walileta malalamiko ya kutapeliwa na mchezaji Buswita Sh milioni 10, kitu kizuri Buswita mwenyewe alikubali jambo hilo ambalo lilirahisisha kazi yetu.

“Baada ya klabu hizo kukutana, zimekubaliana Yanga ilipe kiasi hicho cha fedha ambacho Buswita alichukua ili awe huru Simba,” alisema Mwanjali.

“Wakati wowote fedha hizo zikilipwa Buswita ataruhusiwa kucheza, tumeona tutumie njia hii ili mchezaji arejee uwanjani ukizingatia umri wake ni mdogo,” aliongeza.

Katika hatua nyingine, kikosi cha Yanga kiliendelea kujiweka fiti kwenye Uwanja wa Uhuru ili kuikabili Njombe Mji katika pambano la ligi kuu litakalopigwa Jumamosi hii.

Katika mazoezi hayo, kocha wa kikosi hicho, George Lwandamina, aliwahenyesha vilivyo wachezaji wake huku akitoa adhabu zinazofanana na mazoezi ya kijeshi kwa wale walioonekana kuwa goigoi.

Baadhi ya wachezaji walioonja joto ya jiwe baada ya kufanya uzembe ni pamoja na kiungo Thaban Kamusoko, beki Nadir Haroub ‘Cannavaro na mshambuliaji Donald Ngoma.

Adhabu walizokutana nazo kwa nyakati tofauti wachezaji hao ni kupiga ‘push up’ pamoja na kuruka juu mara tano.

Zoezi ambalo lilionekana kuwa changamoto kwa wachezaji wengi ni lile la kukimbia huku wakizunguka koni.

Lwandamina pia alionekana akiwaandaa wachezaji wake kukabiliana na timu ambayo ina safu ya ulinzi isiyopenyeka kirahisi, kwa kuwataka kupiga mashuti kwenda golini wakiwa nje ya kumi na nane.

Katika zoezi hilo, kiungo wa timu hiyo, Papy Tshishimbi ndiye aliyekuwa kivutio  kutokana na kupiga mashuti makali, hali iliyosababisha kushangiliwa na mashabiki waliohudhuria mazoezi hayo.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa, alisema wanaendelea kuipika safu yao ya ushambuliaji ili iwe na uwezo wa kufunga mabao ya kutosha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles