21.5 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

Ulimwengu, Sheikh Ponda, TLS, wagusia katiba, maelewano kwenye jamii

Na Clara Matimo, Dar es Salaam

Watu wa kada mbalimbali nchini wameendelea kujitokeza na kutoa maoni yao juu ya suala la umuhimu wa katiba  ambayo itaondoa malalamiko na changamoto tofauti tofauti  zilizopo  kwenye jamii na kuleta  maelewano ya kisiasa.

Baadhi ya wadau hao ni Katibu wa Maimamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda, Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS),Gloria Kalabamu, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Wakili Anna Henga na mwandishi nguli wa habari, Jenerali Ulimwengu, ambao walitoa ushauri wao juu ya suala la katiba mpya wakati wa mdahalo wa uchambuzi wa kitabu cha Rai ya Jenerali juzuu ya tatu na masuala ya Katiba.

Sheikh Issa Ponda.

Akizungumza katika Mdahalo huo uliofanyika Desemba 7, katika Ukimbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julias Nyerere jijini Dar es Salaam, kama miongoni mwa wazungumzaji, Sheikh Ponda alisema ukosefu wa mfumo wa masikilizano ni moja wapo ya changamoto zinazosababisha mgawanyiko kati ya wananchi na viongozi walioko madarakani.

“Kama kungekuwa na mfuno mzuri wa masikilizano isingefikia hatua watawala na raia kutofautiana, tumeshuhudia mara nyingi baada ya uchaguzi kunakuwa na malalamiko makubwa yanayosababisha watu kuuwawa na wanaouwawa ni raia na wanaopeleka majeshi kuwauwa raia ni watawala.

“Tume ya uchaguzi ni muhimu sana kwa sababu ni kiini cha uhalali wa utawala, lakini pia ni kiini cha vurugu zote, vurugu zote ambazo tunazisikia kama alivyozungumza Jenerali kwenye kitabu chake kwamba tusidhani yale mataifa ambayo yamefikia mahali kuna umwagaji mkubwa wa damu ni wapumbavu au wajinga ni watu waliosoma na wana busara kama kama sisi watanzania lakini kutokana na kutokuwa na mazingatio na makubaliano katika haya mambo ndiyo tatizo kubwa,”alisema Sheikh Pond na kuongeza.

“Hamuwezi mkapata maendeleo kama hampitii kazi zenu, tunapozungumza masuala ya katiba tafsiri yake ni kwamba tunapitia  kazi zetu na kufanya maboresho, hata wakati wa chama kimoja, ukiangalia kutoka walipoanza mchakato wa chama kimoja kuja kwenye vyama vingi kuanzia  mwaka 1992 hadi 1995 wamefanya mabadiliko ya katiba karibuni mara tano, ambayo tunasema ni kuziba vilaka hii inaonyesha umuhimu wa kuboresha na hapa ilikuwa ni chama kimoja,”amesema.

Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS),Gloria Kalabamu.

Makamu wa Rais TLS, Kalabamu alisema  lazima katiba ibadilike maana sasa kuna mambo mengi ambayo hayakuwepo wakati katiba  iliyopo ya mwaka 1977 ikiandaliwa kama utandawazi ambao ndiyo unaoendesha dunia.

“Tumeanza kushuhudia tofauti kubwa miaka ya karibuni ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo uhitaji wa katiba umezidi kushamili na kuzungumziwa na makundi mbalimbali nchini hii inadhihirisha kwamba wananchi wanahitaji katiba mpya,” amesema Kalabamu.

Kwa upande wake Ulimwengu ambaye ndiye Mwandishi wa Kitabu hicho kupitia makala zake mbalimbali alizoziandika katika gazeti la Rai tangu mwaka 1996 alisema “Katiba iliyopo  inamapungufu kwenye swala zima la mahusiano ya kimadaraka kwa sababu ambavyo chombo kimoja muhimu au muhimili mmoja muhimu umeingilia muhimili mwingine.

 “Suala la kujadili katiba ni  la kudumu wala halihitaji kupangiwa kipindi maana kila wakati kunanafasi ya kuboresha ni mjinga peke yake anayeweza kudhani kwamba kazi iliyofanyika mwaka 1977 inatosha inamaana kimawazo ni mfu ingawa anaonekana anatembea maana hata nguo nilizovaa leo inawezekana kesho nikaona hazifai nahitaji kubadilisha au gari nililonalo mwaka huu mwaka kesho nikaona silihitaji tena nahitaji kununua lingine,”alisema Ulimwengu ambaye pia ni mdau wa haki za binadamu nchini,” amesema.

Upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Wakili Henga, alitoa wito kwa serikali kutoa wigo mpana na uhuru kwa watu na taasisi mbalimbali kuzungumza na kuelezea elimu mahususi ya umuhimu wa katiba ili wananchi waelewe waweze kuhusisha na maisha yao ya kila siku kwani itasaidia kujenga jamii iliyotayari kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuandiaka katiba mpya.

“Tunatamani tuendelee kujadiliana na kuongea maana tukiendele kujadiliana tutapata namna bora ya kuipata katiba mpya toka mwaka 2014 tulipoishia,”alisema Wakili Henga.

Kwa mujibu wa wakili huyolengo la mdahalo huo ni kuwawezesha umma wa watanzania kufuatilia na kujihusisha kwa karibu na mambo yote yanayohusiana na utawala bora, utawala wa sheria na haki za binadamu ambavyo vyote msingi wake ni katiba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles