27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Ulimwengu azindua kitabu, atoa wito kwa vijana

Na Clara Matimo, Mwanza

Mwandishi nguli wa habari na mdau wa haki za binadamu nchini, Jenerali Ulimwengu, amezindua kitabu chake kinachobeba dhima ya udadavuzi katika masuala mbalimbali ikiwemo siasa, utawala bora na  haki za binadamu huku akitoa wito kwa vijana kupigania haki.

Uzinduzi wa kitabu hicho kilichopewa jina la Rai ya Jenerali umefanyika hivi karibuni jijini Mwanza  kwa ufadhili wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC) ambapo watu kutoka kada tofauti tofauti walihudhuria wakiwemo wanasiasa, wanasheria, Wahadhiri wa vyuo vikuu, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT) Dayosisi ya Karagwe Mkoa wa Kagera, Dk.Benson Bagonza na waandishi wa habari.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Ulimwengu alisema tatizo kubwa linalowakabili watanzania wengi wakiwemo vijana ambao ndiyo tegemeo kwa taifa  ni kutaka kujua bila kujifunza hali  hiyo imechangiwa na mfumo wa elimu ambao unamfanya mwanafunzi akariri badala ya  kumpa ujuzi hivyo wanashindwa hata kudai haki zao.

 “Kitabu hiki ni makala zangu mbalimbali ambazo niliziandika kwenye gazeti la Rai na Mtanzania kuanzia mwaka 1996  kuhusu mambo yaliyokuwepo kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 ikiwa ndiyo uchaguzi wa kwanza kufanyika hapa nchini chini ya vyama vingi ambapo nimeeleza kulikuwa na mambo gani katika masuala ya haki za binadamu, usawa wa kijinsia na nafasi walizopewa wagombea kunadi sera zao kwenye vyombo mbalimbali vya habari.

“Mfumo huo wa elimu umesababisha kiongozi anapoteuliwa  kuongoza wizara fulani anakuwa anajua kila kitu hata kama hakusomea fani hiyo, madaraka ya Tanzania yanampa kiongozi uwezo wa kujua kila kitu huu ndiyo muujiza wa elimu yetu, nimetoa kitabu hiki lengo langu nataka  hata ambao hawakuwepo miaka hiyo wakikisoma wajifunze ingawa kwa mtazamo wangu naona tangu uchaguzi huo hadi leo bado tuko vile vile lakini bado tuko hapo hapo hivyo kazi kwenu vijana kuchakata binafsi najia  pekee ya kutunza mambo ni kwa kuyaweka kwenye maandishi,”alisema Ulimwengu.  

Mratibu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC), William Mtwazi, aliiambia MTANZANIA Digital kwamba  wameamua kushirikiana na Ulimwengu katika uzinduzi wa kitabu chake kutokana na dhima yenyewe ya kitabu  maana masuala anayoyazungumzia ikiwemo  haki za binadamu, utawala wa sheria na utawala bora ni kazi wanazozifanya.

“Ulimwengu ni  mchechemuzi ukisoma kitabu hiki utaona namna alivyokuwa mwalimu katika nyanja za ufundishaji, uelimishaji  na udadavuzi katika masuala mbalimbali Sisi kama wadau wa sheria na watetezi wa haki za binadamu tunaamini tukishirikiana naye ni fursa nzuri kwetu ili kuhakikisha ujumbe uliomo ndani ya kitabu chake unaifikia jamii Kikubwa tunachotaka watanzani wajifunze wawe na moyo wa uthubutu katika kutafuta haki na maarifa kisha wayaishi  hayo maarifa ambayo wanayapata.

“Ukizingatia Ulimwengu ni mwandishi nguli wa habari pia amefanya kazi serikalini na amewajenga vijana wengi imani yetu yote ambayo ameyazungumzia ndani ya kitabu chake yanaenda kuwafikia wananchi wengi na kadri yanavyowafikia ndivyo wanavyopata uelewa na ufahamu ili wayaishi pia wajue jinsi ya kuenenda katika misingi ya utawala wa sheria na utafutaji wa haki za binadamu,”alisema Mtwazi.

 Mwanasiasa John Heche, alisema ulimwengu ni mwandishi ambaye alikuwa akichambua kwa kina mambo mbalimbali yaliyokuwa yakitokea tangu mwaka 1996 hivyo  kitabu hicho ni urithi kwa kizazi kilichopo na kijacho ambacho kitatumika kushape maisha yao.

“ Tunapozungumzia dhana ya uhuru wa watu tunakumbuka  kipindi cha wakoloni walitujengea shule, reli, vyuo vikubwa na  hospitali  lakini watu walikataa kwa sababu hakuna kitu kikubwa kama uhuru, leo baadhi ya viongozi wanataka watupimie uhuru mambo ambayo tumekuwa tukiyapinga na tunayakataa hivyo kwa kitabu hiki kitasaidia kutunza, kuonya na kuelimisha viongozi wanaokuja wasije wakafanya mambo kama hayo kwa sababu wanataka waturudishe kule tulikotoka,”alisema Heche.

Mhadhili wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine(SAUT), Shukuru Paulo, aliwataka watanzania kusoma kitabu hicho maana ni shibe na afya ya akili kwa sababu kinakithi mahitaji hayo vilevile kitamwezesha msomaji kufikili, kujenga hoja na kuwaza sawasawa.

 “Ni muhimu kusoma kwa sababu mfuko uliyotupu hausimami wima ili usimame lazima uujaze bidhaa na ndivyo ilivyo kwa akili,  akili iliyotupu haiwazi, haifikili pia  haijengi hoja.Unafanya nini sasa kwa akili iliyotupu?  Unaishibisha maarifa na uelewa kwa kusoma vitabu kama hiki,”alisema mhadhili huyo huku akionyesha kitabu hicho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles