28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Ulaya yamfungia  milango Dk Shein

Pg 3Elizabeth Hombo na Evans Magege, Dar es Salaam

UMOJA wa Ulaya (EU), umevunja uhusiano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kwa kukiuka mkataba wa utawala bora, ukandamizaji wa demokrasia na uchaguzi mkuu kutokuwa huru na haki.

Kwa sababu hiyo, EU imesema haitapeleka Zanzibar ripoti yake ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana kwa sababu hata taasisi zote za umoja huo haziitambui serikali hiyo.

Msimamo huo ulitolewa  na Mwangalizi Mkuu wa   Waangalizi wa Uchaguzi wa Umoja wa Ulaya (EU EOM), Judith Sargentini, alipozungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana.

Hatua hiyo inaweza kutafsiriwa kama   msimamo rasmi wa kutoutambua uongozi wa Rais Dk. Shein.

Sargentini alisema kwa sasa EU haifanyi kazi na SMZ, hivyo haoni umuhimu wa kuwasilisha ripoti hiyo visiwani humo.

“Naomba niliseme hili wazi kwamba ripoti hii sitaiwasilisha Zanzibar kwa sababu EU kwa sasa haishirikiani na SMZ kwa kuzingatia kuwa hatuutambui uchaguzi wa marudio.

“Nazungumza hili najua nipo ndani ya mipaka ya Tanzania lakini samahani…. sitakwenda Zanzibar.

“Pia hata baadhi ya nchi wanachama kwa kiasi fulani wamekata misaada kwa SMZ kwa sababu mkataba wa kusimamia utawala bora umekiukwa,” alisema Sargentini.

Sargentini ambaye ni Mbunge wa Bunge la Ulaya, katika ripoti hiyo alielezea mambo mengi ambayo yalitawala duru za siasa  nchini kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu.

Upungufu huo ni pamoja na mifumo ya uchaguzi wa Tanzania kwamba haiko huru na uendeshaji wake ni wa kutojiamini na   hata yanayoendelea bungeni hivi sasa ni matokeo ya mifumo hiyo.

Katika muktadha huo, alishauri jitihada za makusudi zifanyike   kupunguza uhusika wa taasisi za utawala za serikali kwenye masuala ya upangaji na utekelezaji wa mchakato wa uchaguzi.

Sargentini alisema uteuzi wa makamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) upitiwe upya  kuongeza imani na uhuru miongoni mwa wadau.

“Hatua ya kujenga mfumo huru wa kudumu wa NEC katika mikoa pia uangaliwe pamoja na mfumo wa muda kwenye ngazi ya jimbo wakati wa uchaguzi.

“Mfumo huu uachane na utegemezi wake wa sasa kwa vyombo vya utawala vya mkoa na wilaya,”alisema.

Mwakilishi huyo wa EU alisema Katiba zote za Muungano na Zanzibar kwa sasa zinanyima haki ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais mahakamani, hivyo lazima sheria irekebishwe.

“Katika nchi zote hii sheria ipo isipokuwa Tanzania…Juzi tulikuwa bungeni mjini Dodoma nimeuliza kuhusu Katiba Mpya lakini sijapewa jibu la kueleweka.

“Hivyo lazima hili liwekwe ili iwepo  sheria ya kupinga matokeo ya rais kwa mujibu wa misingi ya kimataifa ya uendeshaji wa uchaguzi wa demokrasia,”alisema Sargentini.

EU pia inapendekeza kuwapo   haki ya vyama vya siasa kuungana na kuandikisha umoja wao kwa mujibu wa sheria na kusimamisha wagombea.

“Hili lazima lielezwe kwenye sheria, hususan kwenye suala la uchaguzi wa Rais wa Muungano ambako wagombea wawili wanasimamishwa kwa pamoja kugombea nafasi ya rais na makamu wa rais,”alisema Sargentini.

Ili kuongeza imani katika mchakato wa uchaguzi, hatua thabiti za uwazi kama vile ruhusa kwa wawakilishi wa vyama vya siasa   na waangalizi kujionea hatua zote kuanzia kujumlisha matokeo, zinahitajika.

Pia alisema nafasi ya vyombo vya usalama siku ya uchaguzi iangaliwe upya kwa sababu idadi kubwa ya jeshi kama ilivyokuwa Zanzibar inaongeza hatari za vitisho kwa wananchi.

“Mamlaka ya polisi kwenye uchaguzi lazima ielezwe kwa uamilifu kwenye sheria na wapiga kura wafahamishwe. Wingi na mwonekano mkubwa wa  polisi siku ya uchaguzi kunaongeza hatari ya vitisho,”alisema .

Alisema uamuzi wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu lazima utekelezwe kwa wagombea binafsi kugombea nafasi yoyote kwenye uchaguzi.

“Wagombea binafsi wanatakiwa kuwa na haki ya kugombea nafasi yoyote kwenye uchaguzi wa Muungano na Zanzibar kama ilivyoelezwa kwenye Mkataba wa Kimataifa ya Haki za Uraia na Siasa na Hati ya Afrika ya Haki za Binadamu.

Sheria ya Mtandao

Awali alizungumzia Sheria ya Makosa ya Mtandao   akisema   kanuni za utekelezaji wa sheria hiyo zianzishwe ili ziendane na aina ya makosa.

“Utekelezaji wa vifungu fulani vya Sheria ya Makosa ya Mtandao unaweza kubana uhuru wa kujieleza na kusababisha watu kukamatwa holela.

“Wanaofunguliwa mashtaka kwa mujibu wa sheria hiyo wasinyimwe haki ya kujitetea mbele ya mahakama, kama ilivyo sasa ambako ombi kwa mahakama hufanyika kwa kusikiliza upande mmoja tu na kwa siri,”alisema Sargentini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles