28.7 C
Dar es Salaam
Thursday, February 22, 2024

Contact us: [email protected]

UKWELI, UZALENDO VILIVYOTIBUA KIBARUA CHA MKWASSA STARS

Na ZAINAB IDDY, DAR ES SALAAM


mkwasa1MAPEMA wiki hii, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitangaza kuachana na aliyekuwa nahodha wa zamani wa timu ya soka ya taifa ‘Taifa Stars’, Charles Boniface Mkwassa na kumpa majukumu hayo, mzawa mwingine Salumu Mayanga.

Ukiacha na suala hilo, Spotikiki leo inaziangalia dakika 990 za Mkwassa akiwa na kikosi hicho cha Stars.

Tangu kupewa majukumu ya ukocha, baada ya kutimuliwa kwa Mholanzi Mart Nooij, Mkwassa ameweza kuiongoza Stars katika michezo 11, huku akishinda mmoja,  akatoa sare nne na  kupoteza mara sita.

Mkwassa alianza kibarua cha kuinoa Stars  katika mchezo wao dhidi ya Malawi,  ukiwa ni mtanange wa awali  wa kusaka tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2018 zitakazofanyika nchini Urusi.

Katika mchezo huo, Stars ya Mkwassa iliweza kuitoa Malawi kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1, kabla ya kutoa sare ya mabao 2-2 na Algeria.

Matokeo hayo yaliwafanya Watanzania kuendelea kuwa na imani na timu yao kusonga mbele, licha ya Algeria kuonyesha wazi kuizidi uwezo Stars.

Hali ikaanza kuwa mbaya, baada ya Stars kujikuta ikipokea kipigo cha aibu cha mabao 7-0   katika mchezo wa marudiano nchini Algeria.

Kipigo hicho  ndicho kilichoanza kuzua maneno mengi  kwa wadau wa soka na kusahau kuwa moja ya sababu, iliyosababisha hilo ni kamati zilizoundwa ambazo hazikuwa na malengo ya kuwanufaisha wachache.

Thamani ya Mkwassa iko wapi?

Kuvunjika kwa ndoa ya Mkwassa na TFF, imeonekana kuzua maswali mengi yasiyo na majibu. Lakini wapo wanaodai kuwa huenda kusema kwake ukweli ndiko kulikosababisha  kuondolewa katika nafasi hiyo.

Itakumbukwa kuwa Mkwassa aliingia kubeba majukumu ya Nooij, akitakiwa kulipwa dola za Marekani 12,500 (zaidi ya Sh. milioni 25) kwa mwezi, lakini kwa mujibu wake kiasi hicho cha fedha kililazimika kupungua, baada ya TFF kudai hawana fedha  hizo, jambo ambalo limejulikana pindi alipotangazwa kuondolewa katika nafasi hiyo.

Kwa mujibu wa Mkwassa mwenyewe, alikubali kupunguza kiwango cha fedha za mshahara wake ikiwa ni moja ya uzalendo kwa taifa lake.

Licha ya kupunguza kiwango hicho, lakini  mara ya mwisho mkwassa kulipwa mshahara ilikuwa Oktoba mwaka jana na hivyo kubakiwa na miezi minne anayodai pamoja na marupurupu mengine.

TFF imetangaza kumlipa kwa awamu mbili, kabla ya kufika tarehe za kumalizika kwa mkataba walioingia naye Februari mwaka huu.

Hakuna anayepinga kuondolewa kwa Mkwassa kwenye benchi la ufundi la Stars, lakini suala linalozua maswali, ni je, Mayanga ataweza kutimiza ndoto za Watanzani na siasa zilizopo katika soka la Bongo?

Mashabiki wa soka hapa nchini watalazimika kuzitazama Fainali za Mataifa Afrika za mwaka huu ‘Afcon 2017’ kupitia televisheni, huku majirani zetu Uganda wakitinga kwenye michuano hiyo.

Kwa utaratibu wa timuatimua ya makocha huku wakiwekwa kwa kubahatisha ni ngumu kutabiri kuwa siku moja Taifa Stars itafika huko.

Alikuwepo kocha Mart Nooij aliyekuwa akiinoa Stars kwa kusaidiana na Mayanga, lakini walitimuliwa ghafla baada ya kufanya vibaya katika michuano ya COSAFA, mechi zakuwania kufuzu Afcon 2017 na kuvurunda katika michuano ya CHAN.

Sasa ni zamu ya Mkwassa aliyekuwa akisaidiwa na Hemed Moroco, ambaye amecheza mechi 12 , Je ni wapi  amechemsha hadi ikaonekana  ameshindwa kutimiza majukumu yake na kusababisha  mabadiliko yafanyike kwake tu ilihali upande wa timu yasiwepo.

Mkwassa aliwahi kuanika baadhi ya changamoto zinazokwamisha timu kufanya vizuri, ikiwamo ile ya kutopewa mishahara yake kwa wakati.

Lakini pia, taasisi inayoongoza na kusimamia soka hapa nchini ilishindwa kumuwezesha  kuzunguka mikoani kuangalia vipaji.

Tukio la wachezaji kusota na kulala katika mabenchi katika Uwanja wa Ndege nchini Ethiopia ni miongoni mwa mambo yaliowekwa wazi na Mkwassa.Ukweli huo umeonyesha kuwakera mabosi wa TFF.

Ni dhambi kumhukumu Mkwassa katika mazingira kama haya. Ukichunguza tu uteuzi wake wa kikosi mara kadhaa utabaini  ulitokana na uzoefu binafsi wa kocha huyo, kwani wengi aliowateua ni wale aliokuwa akiwajua kutokana na kuwafundisha katika timu yake ya Yanga  na hili limetokana na kushindwa kupata nafasi ya kuzunguka mikoani.

Ukweli utabaki kuwa kiini cha matatizo ya Taifa Stars kipo ndani ya TFF, lakini pia shirikisho hilo limeshindwa kutambua thamani ya Mkwassa katika dakika 990 alizokuwa na kikosi cha timu ya taifa na hii inadhirisha ule usemi unaosema ‘Shukrani ya punda mateke’ na ‘Tenda wema uende zako usingoje shukrani’.

 

WASIFU WAKE

KUZALIWA: 10 Aprili 1955 (Miaka 60)

ALIPOZALIWA: Morogoro, Tanzania

NAFASI: Beki/Kiungo

TIMU: Tanzania (Kocha Mkuu)

KLABU ALIZOCHEZEA: Mseto FC,Tumbaku ya Morogoro,Yanga SC na Taifa Stars.

TIMU ALIZOFUNDISHA:Super Stars,Yanga SC,Sigara, Al Khaboura. (Oman, Kocha Mkuu),Tanzania Prisons,Yanga SC,Coastal Union,Tanzania Prisons,Moro United,Miembeni,African Lyon,Ruvu Shooting, Al Shoolai (Saudi Arabia) na Yanga SC, kwa upande timu za taifa ni Tanzania Bara B ‘Kakakuona’,Tanzania timu ya vijana U17, Taifa Stars (Msaidizi wa Syllersaid Mziray)Timu ya taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’, na ‘Taifa Stars’ .

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles