24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

UKIWA HIVI, MWANAMKE HABANDUKI! – 2

USISHANGAE kuwaona akina fulani wanadumu kwenye uhusiano wao kwa muda mrefu huku kwa upande wako mambo yakiharibika. Usije kujiuliza ni vipi kwao tu, kwako mambo hovyo?

Ni kwamba wenzako wanawekeza kwenye uhusiano, wakati wewe ukienda ilimradi siku zinakwenda. Kwa hakika hamuwezi kuwa sawa.

Ndiyo sababu tunajifunza somo hili. Ni mada iliyoanza wiki iliyopita na leo tunamalizia sehemu ya mwisho. Tunaangalia ni mambo gani wanawake wanavutiwa zaidi kwa wanaume. Au niseme vitu gani ukivifanya kwa mwanamke wako hatafikiria kukuacha.

Tuendelee na mada yetu.

 

KUMSIFIA

Wanaume wengi hupuuzia hili, huona kama ni jambo lisilo na maana sana kwao na wenzi wao. Hali ni tofauti sana kwa wanawake ambao hupenda kuwasifia wanaume zao.

Kumsifia mwanamke kuna nafasi kubwa sana kwake. Jenga utamaduni wa kumsifia mpenzi wako, unamuweka katika kilele cha upendo.

Anajiona kamili, peke yake na mwenye nguvu kwako. Anajiamini na unamfanya azidi kukupenda kwa kuwa anaamini yupo na mwanaume ambaye anajivunia kuwa naye.

 

MALENGO

Wanaume wengi wana ulemavu mmoja; hawapendi kuwashirikisha wanawake katika mambo yao. Wanapenda kufanya mambo yao kwa siri na wakati mwingine ikilazimika kumwambia mwenzi wake basi kwa mshtukizo baada ya kukamilisha jambo husika.

Hii si sahihi. Mwenzako anapaswa kujua mambo yako, ndiye mtetezi wako nambari wani. Mweleze juu ya malengo yako, wakati mwingine anaweza kukusaidia sehemu ambayo hukutarajia.

Hata hivyo, kumshirikisha katika malengo yako, kunampa nguvu na nafasi ya kujiona mwanamke kamili katika penzi lenu.

 

MPE KIPAUMBELE

Kuna wakati wanawake huwa na mambo yao binafsi. Kazini au kifamilia. Inawezekana akatatizika katika eneo fulani ambalo kwa namna moja ama nyingine atahitaji usaidizi wako. Ikitokea akawa katika hali hiyo, msikilize.

Mathalani ana tatizo la kifamilia, amekuambia mmoja wa wazazi wake anaumwa, msaidie. Si lazima kifedha, lakini kuonesha kujali kwako tu, kutampa matumani kwamba yupo na mtu sahihi.

Acha kupuuza mambo yake; hata yale madogo. Msikilize, mshauri panapofaa kufanya hivyo na ukiweza msaidie hata kifedha. Katika upande wa pili ni hivyo hivyo. Labda una tatizo binafsi, kazini kwako au kifamilia, mshirikishe.

Unaweza kushangaa jambo ambalo uliamini unaweza kulimaliza peke yako, kwa kumshirikisha likawa jepesi zaidi na mambo yakaendelea vyema. Kipaumbele kwa namna yoyote ile, kunaongeza mapenzi zaidi kwa mwanamke.

 

TENDO LA NDOA

 

Hiki ni kipengele nyeti, kinachohitaji lugha nzuri ya kirafiki kukifafanua. Hakuna siri, tendo la ndoa ni moja ya kiwakilishi cha ndoa. Maana hata maandiko yanasema: “Mwanamke ataacha wazazi wake na kwenda kwa mumewe, nao watakuwa mwili mmoja.”

Kimsingi tendo la ndoa lina nafasi yake. Ni muhimu likaheshimiwa na kutengewa muda maalum wa kufurahia. Si papara. Kwa bahati mbaya wanaume huwa si wafuatiliaji sana wa kujua namna ya kuwafurahisha zaidi wenzao. Wenyewe wanajiwazia wenyewe. Wanafikiria namna ya kuwakomoa wenzao.

Tendo la ndoa halina maana ya kukomoana. Jenga mazoea ya kufanya maandalizi kamili kabla ya tendo. Sikiliza hisia za mwenzako. Ukiweza kumjulia mke wako katika eneo hili, ni wazi kwamba utazidisha upendo wake kwako, lakini pia atakuwa katika kuta za uaminifu. Akatafute nini nje wakati wewe ndiye mganga wake unayeweza kumtibu barabara?

Kuna kitu nimesahau? Kama kipo nitafute pembeni, kwa hapa haya yatoshe kukufanya uelewe nilichotaka kukuelekeza. Nikuache na neno moja; uamuzi wa kuijenga ndoa yako upo mikononi mwako.

Jiandae kupata kitabu changu kipya cha SIRI ZA MAISHA YA NDOA YENYE FURAHA kitakachokuwa mitaani hivi karibuni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles