28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

SARAKASI SAKATA LA ROMA MKATOLIKI

Na Aziza Masoud, Dar es Salaam

TUKIO la kutekwa na hatimaye jana kupatikana kwa msanii wa Hip Hop hapa nchini, Ibrahim Mussa, maarufu kwa jina la Roma Mkatoliki, limeacha maswali mengi.

Roma ambaye anadaiwa kutekwa Jumatano wiki hii sanjari na wasanii wenzake, Moni Centrozone, Bin Laden na mfanyakazi wa mama mzazi wa mmiliki wa studio za Tongwe Records, Junior Makame, maarufu J Murder aliyejulikana kwa jina moja la Imma, taarifa za kuachiwa kwake zilianza kusambaa jana mchana baada ya kuonekana katika Kituo cha Polisi Oysterbay, Dar es Salaam.

MTANZANIA Jumapili ambalo lilifika katika kituo hicho muda mfupi baada ya kusambaa kwa taarifa hizo, lilidokezwa kuwa wasanii hao walikuwa wakihojiwa na hakuna mtu yeyote aliyeruhusiwa kuwaona.

Miongoni mwa watu ambao walifika kituoni hapo kumwona Roma na hawakufanikiwa, ni mke wake Nancy, J Murder na wasanii wengine.

Taarifa ambazo zilipatikana kituoni hapo, lakini hazikuweza kuthibitishwa mara moja na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Susan Kaganda, zilieleza kuwa wakiwa kituoni hapo wasanii hao walichukuliwa maelezo ya mdomo na kisha maandishi.

Baada ya kuchukuliwa maelezo, walichukuliwa na polisi na kisha kupelekwa katika Hospitali ya Mwananyamala.

MTANZANIA Jumapili lilishuhudia wasanii hao wakitolewa kituoni hapo kuelekea Mwananyamala, huku wakiwa wamebebwa katika gari aina ya Toyota Noah T 253 CEU yenye rangi ya fedha.

Safari ya kuwapeleka Hospitali ya Mwananyamala ilianza saa 1:15 usiku.

Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo saa 3:00 usiku, baada ya kuchukua muda mrefu kwa vipimo, Roma alisema yupo salama na anawashukuru Watanzania wote kwa kumpa sapoti.

“Sijapata muda wa kuingia kwenye mtandao, lakini najua Watanzania wamenipa sapoti, kwa sasa sitaweza kuongea chochote kwa sababu ya taratibu za uchunguzi, nitaongea yote kesho,” alisema Roma ambaye alionekana akichechemea na mwenye majeraha.

Kabla Roma hajazungumza, awali mtu aliyejitambulisha kuwa ni ndugu yake, alidai kuwa msanii huyo amejeruhiwa kwenye mkono na pia anatembea kwa kuchechemea.

Ndugu huyo wa Roma ambaye hata hivyo alikataa kutaja jina lake, aliliambia gazeti hili kuwa hadi anafikishwa hospitalini hapo, msanii huyo hakuwa katika hali nzuri.

“Huo ndio ukweli ingawa hatujaruhusiwa kushuhudia mahojiano yao, lakini tumeambiwa kapelekwa… kwa kumwangalia ana mikwaruzo, wengine wapo vizuri, lakini Roma kaathirika zaidi, amehojiwa kama shahidi na si mtuhumiwa, polisi ndio wana taarifa zaidi,” alisema.

Hata hivyo, Kamanda Kaganda hakuwa tayari kuzungumza lolote kuhusu tukio hilo zaidi akisema kuwa hadi watakapotoka hospitali.

 Wakili wa Roma aliyejitambulisha kwa jina la Jebra Kambole, alisema mteja wake alikuwa anachechemea na ana majeraha mkononi hali iliyomfanya ashindwe kusalimiana naye.

Wakili huyo wakati akisema hayo naye alikuwa hajapata fursa ya kuzungumza naye.

Zaidi alisema Roma na wenzake walianza kuhojiwa saa nane mchana hadi saa moja usiku kabla ya kupelekwa hospitali.

“Hali ya Roma si nzuri, anatetemeka, wenzake wana afadhali kidogo… amehojiwa kama mtu wa kawaida na si muhalifu ili awasaidie polisi katika upelelezi, hadi sasa hakuna shtaka lililofunguliwa dhidi yao, wakimaliza kuangaliwa afya zao wataachiwa huru kwenda nyumbani,” alisema.

Wakati wakili huyo akisema hayo, ofisa mmoja aliyefika kituoni hapo ambaye hakutaka kutaja jina lake gazetini, aliliambia MTANZANIA Jumapili kuwa kuna vitu vimemshangaza kuhusu tukio hilo na kwamba alikuwa akilifuatilia kwa ukaribu.

“Nimetoka humo ndani, lakini kuna vitu sijavielewa, tunataka kuangalia kama ni michezo imechezwa au kweli wanahitaji msaada… tumefanya juhudi nyingi, lakini kuna vitu vimenitia wasiwasi,” alisema ofisa huyo pasipo kuvitaja vitu hivyo.

Ofisa huyo aliliahidi kulipatia gazeti hili taarifa za kina pale atakapokamilisha kulifuatilia jambo hilo kwa kina.

Taarifa zisizo rasmi zilizolifikia gazeti hili, zinaeleza kuwa Roma na wenzake walionekana tangu asubuhi katika mahali ambako hapakuwekwa wazi.

Inaelezwa mtu wa kwanza kupigiwa simu kujulishwa taarifa za kupatikana kwa akina Roma, alikuwa ni Mkurugenzi wa Vipindi wa Clouds Media, Ruge Mutahaba.

Hata hivyo, Ruge ambaye alikuwapo kituoni hapo na baadae katika Hospitali ya Mwananyamala, alilitaka MTANZANIA Jumapili kumuuliza suala hilo Roma mwenyewe na si yeye.

Majira ya saa 3:00 usiku, Roma na wenzake wakiwa hospitalini hapo kuchukuliwa vipimo, askari nao walikuwa wakisubiri majibu yake ili kuyawasilisha kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni.

Pamoja na hayo, baadhi ya watu wameanza kuhoji tukio zima la kutekwa hadi kupatikana kwa wasanii hao, wengine wakidai kuwa huenda ni mchezo uliochezwa na kiongozi mmoja.

Wengine wamekwenda mbali na kuhoji uwezekano wa kugongana kwa matukio matatu tofauti yakimuhusisha msanii wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul maarufu Diamond, Meneja wake, Babu Tale na kiongozi mmoja ambaye anataka kurejesha ushawishi wake.

Wanaohoji hilo, wanatilia shaka kitendo cha Diamond kukutana na kiongozi huyo siku mbili baada ya tukio la utekaji kufanyika na kisha kutoa wimbo mpya siku moja kabla ya wasanii hao kuachiwa huru.

Watu hao wamekwenda mbali na kuhoji hatua ya Babu Tale kuhamasisha wasanii kuungana kuwasaka wenzao na zaidi akidaiwa kuwashawishi wakutane na kiongozi huyo ambaye alikaririwa akisema watapatikana kabla ya Jumapili.

Hisia za namna hiyo zilikwenda mbali na kulihusisha tukio hilo na njama za kufifisha nguvu ya mkutano wa hadhara wa aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye, uliofanyika jana jimboni kwake Mtama mkoani Lindi.

Wenye mawazo ya namna hiyo, wanaona ni jambo lisiloingia akilini kwa wasanii hao kutekwa siku moja mara baada ya Nape kuandika kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa atakwenda kuzungumza kila kitu jimboni kwake Mtama na kisha kuachiwa siku hiyo hiyo ambayo mwanasiasa huyo alikuwa akifanya mkutano wake.

Awali jana asubuhi kabla akina Roma hawajapatikana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, alilizungumzia tukio hilo akisema walikuwa wanaendelea na uchunguzi.

Alipoulizwa juu ya kauli ya kiongozi ambaye alisema wasanii hao hadi kufikia kesho watakuwa wamepatikana, Sirro aliwataka waandishi wa habari kumuuliza hilo kiongozi huyo huku akisisitiza kwa upande wake hadi upelelezi utakapokamilika.

Kabla ya Sirro, Waziri Kivuli wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Joseph Mbilinyi, maarufu Sugu, alimtaka kiongozi aliyesema wasanii hao watapatikana kabla ya kesho, kuwaachia jana.

Akizungumza na waandishi wa habari Dodoma jana, Sugu alisema kiongozi huyo amwachie Roma na kwamba hakuna sababu ya kusubiri Jumapili, vinginevyo aseme majukumu aliyopewa huko.

“Jana (juzi) tumeona kiongozi wa Dar es Salaam akisema hadi kufikia Jumapili Roma atakuwa amepatikana. Mimi namtaka amwachie leo (jana) kwanini iwe mpaka Jumapili? Amempa kazi gani huko, anafanywa nini huko?” alihoji Sugu.

Sugu ambaye aliambatana na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa na Frank Mwakajoka wa Tunduma, alisema msanii huyo aachiwe ili arudi kwa familia yake.

Alisema ni haki ya kila msanii kutoa maoni yake kupitia muziki kwa sababu Katiba inaruhusu.

“Kama wasanii tunao uhuru wa kutoa maoni yetu kupitia muziki, kwanza aliyekuwa amemkamata Ney wa Mitego alitakiwa ashtakiwe na Basata nao wanatakiwa washtakiwe kwa kufungia wimbo wake kwa sababu walivunja utaratibu,” alisema.

Roma na wenzake walitekwa Jumatano wiki hii wakiwa katika studio za Tongwe Recods jijini Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles