22.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

Ukitaka kujua tabia ya mtu, angalia anavyowatendea wengine

Businessman Irritated with Loud Coworker

MJEMA anaandika ripoti inayohitajiwa na mkuu wake wa kazi. Wakati muda wa kukabidhi ripoti hiyo ukikaribia, anapigiwa simu na mtu asiyemfahamu. Mjema hajui ni nani hasa anayemtafuta hivyo anaamua kuipokea. Bahati mbaya aliyempigia simu hasikiki vyema. Mjema anaamua kuikata mara moja.

Baada ya dakika moja, namba ile ile inampigia tena. Mjema anapokea simu. Kwa mara nyingine anayeongea hasikiki vyema. Mjema anaona anasumbuliwa na anakasirika. Anakata simu kwa hasira.

Mara ya tatu, namba ile ile inaita tena. Mjema anaudhika na kupandwa na hasira. Anaipokea na kutukana matusi ya nguoni kwa hasira. Baada ya dakika tatu, Mjema anapokea ujumbe mfupi wa maandishi wa kujitambulisha na kuomba msamaha kutoka namba hiyo hiyo. Mjema anagundua kumbe aliyemsumbua alikuwa ni mkurugenzi wa kitengo chake. Mjema anachanganyikiwa. Huku akijutia kitendo cha kumtukana mkuu wake wa kazi bila kujua, anaamua kupiga simu haraka kuomba msamaha kwa kitendo chake hicho.

Kwanini Mjema anasikitika kumtukana mkuu wake wa kazi bila kujua? Je, kama Mjema angegundua kuwa huyo aliyemtukana bila kujua alikuwa ni mtu asiye na hadhi yoyote katika jamii, angesikitika kwa kiwango hicho hicho, kwanini?

Tukio kama hili hutukuta wengi wetu karibu kila siku. Tunapokuwa na watu tunaowaheshimu, kama wazazi wetu, wapenzi wetu, viongozi wa dini, wakuu wa kazi, tunajiweka katika sura inayoheshimika. Tunafanya jitihada za kuonekana wanyenyekevu ili kupata heshima yao. Tunaogopa kudharauliwa na watu hao na hivyo tunajitahidi kuwa na hadhi wanazozitarajia kwetu.

Wakati mwingine tunafanya kinyume. Tunapokuwa na watu tunaodhani ni wa hadhi ya chini, hatuoneshi heshima. Kwa mfano, tunapozungumza na wahudumu wa migahawa ya chakula tunaonesha dharau ambazo kwa hakika tusingethubutu kuzionesha kwa watu tunaowaheshimu. Tunafanya hivyo kwa sababu tunajua hata wanapojisikia vibaya, hatupati madhara yoyote.

Vile vile, tunapokuwa peke yetu mara nyingine tunafanya tofauti na yale tunayoyafanya pindi tunapokuwapo wengine. Uwepo wa watu wengine hutulazimisha kubadili tabia zetu ili kukidhi matarajio ya watu hao. Wakati mwingine tunavuka mipaka na kujikuta tunaigiza tabia zisizo halisi ili tuonekane tunazidi vile tulivyo. Tunalazimika kujibadilisha badilisha kama kinyonga kama jitihada za kutengeneza hadhi bandia tunazozihitaji kwa wengine.

Hadhi, hata hivyo, si jambo baya wakati wote. Tunapokwenda kukutana na watu wengine tunajitazama kwenye kioo kuhakikisha tunaonekana vyema. Tunavaa mavazi ya kupendeza ili kukidhi hadhi tunazotaka kuwa nazo katika jamii. Ndio kusema kusoma mazingira yanataka nini ili tutende yapasayo ni sehemu ya busara ya kawaida ya kibinadamu.

Kwa upande mwingine, kudhibiti namna watu wanavyotuona kwa mbinu ya kuwafanya waone uzuri tusiokuwa nao yaweza kuwa tatizo. Sababu ni kwamba kubadilika badilika ili kuendana na mazingira yaweza kuwa dalili ya kutokujikubali. Mtu anayejikubali halazimiki kubadilika kilaghai kukidhi matarajio yasiyokuwapo. Hujiamini na kuongozwa kwa misingi inayoongoza matendo yake bila kujali yuko wapi na nani.

Ili kupima tabia zetu halisi na kujitambua kwetu, ni muhimu kuangalia tunavyowatendea watu wasioheshimika. Tunavyozungumza na watu tusiowafahamu. Tunavyowajibu makondakta wa daladala. Tunavyowasemesha wahudumu wa migahawa. Ukitaka kujua tabia ya mtu, angalia anavyowatendea watu wa chini. Kwa sababu kujitambua ni kuelewa kwamba binadamu wote wanastahili heshima yetu ya dhati bila kujali nafasi walizonazo.

Mwandishi ni mwalimu wa Saikolojia katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Anapatikana kwa [email protected], 0754 870 815.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles