Na ASHA BANI
WANAHARAKATI, wanasheria na taasisi mbalimbali za Serikali zimesema tatizo la ukeketaji bado kubwa nchini.
Dk. Natujwa Mvungi kutoka Taasisi ya Mafunzo ya Wanasheria Tanzania alikuwa akizungumza hayo Dar es Salaam jana baada ya mkutano wa wadau hao.
Lengo la mkutano huo lilikuwa ni kupinga ukeketaji nchini.
Alisema kuna haja ya kubadilisha baadhi ya vifungu vya sheria ambavyo vitamsimamia mwanamke na mtoto wa kike katika kupinga ukeketaji.
Dk. Mvungi alisema kuna sheria mbalimbali zinazungumzia ukeketaji lakini zinaangalia mtoto wa kike chini ya umri wa miaka 18 na si zaidi ya hapo.
‘’Kuna watoto walio chini ya miaka 18 na hata wanawake waliozidi umri huo wote wanaathirika kutokana na mila hizo hivyo ni vema kukafanyika mabadiliko sheria iwe kwa wanawake na watoto,” alisema.
Alisema suala la ukeketaji katika katiba ya mwaka 2011 ya Kenya na ile ya 2010 Uganda limewekwa na linafanya kazi kwa watoto na wanawake.
Pia alisema katika nchi za Afrika ya Mashariki ni ajenda kubwa kwa mwaka 2017 kupinga ukeketaji kwa mtoto wa kike na mwanamke.
Alisema ni jambo la kushangaza katika Tanzania hakuna kipengele kwenye Katiba kinachozungumzia suala la kupinga ukeketaji.
Alisema sheria ya watoto ya mwaka 2009 na ile ya makosa ya jinai ya mwaka 2002 imekuwa ikikinzana kwa baadhi ya adhabu zake jambo ambalo si zuri.
“Ombi letu kwa wadau na kwa serikali ni kwamba sheria hizo zisipingane maana sheria ya watoto inasema kwamba ukikutwa na kosa la ukeketaji ni kifungo cha miaka 15 au faini Sh milioni mbili huku sheria ya jinai faini yake haizidi Sh 300,000,’’alisema.
Wakili kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Naemy Silayo alisema hadi sasa utafiti unaonyesha mikoa inayoongoza kwa ukeketaji ni Dodoma asilimia 47. Arusha asilimia 41, Singida asilimia 31 na Mara asilimia 32.