28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

WATENDAJI SERIKALINI WASIMTAFSIRI VIBAYA RAIS MAGUFULI

Na Dk. GEORGE KAHANGWA


MIEZI ya hivi karibuni, hususan baada ya Serikali ya Awamu ya Tano nchini Tanzania kuingia madarakani, chini ya Rais Dk. John Magufuli, umeibuka utaratibu wa uendeshaji ofisi za umma na taasisi za Serikali, ambao ni wa namna ya kipekee sana. Utaratibu huu, wapo walioutambua upekee wake na kuupatia jina la Magufulification (kwa tafsiri yetu, Umagufuli).

Pamoja na mambo mengine Umagufuli unajumuisha kubana matumizi, kudhibiti ujanja wa kujipatia kipato kwa njia zisizofaa (kupiga dili), kuondoa wafanyakazi wasio na sifa stahiki za kitaaluma, kuondoa watumishi hewa, kuwawajibisha papo hapo wanaoshindwa kutimiza wajibu wao ipasavyo au kuwa waadilifu (kutumbua majipu), kurejesha mikononi mwa umma mali zilizobinafsishwa bila kuendelezwa na kusitisha shughuli za kisiasa za hadharani hususan muda wa watu kuwa kazini.

‘Umagufuli’ huu unaonekana kuwa na dhumuni la kuimarisha utendaji wa Serikali ili lengo kuu la kujenga Tanzania ya viwanda na kuipeleka nchi katika uchumi wa kati lifanikiwe.

Hakuna shaka kwamba kusudio la rais ni jema na kama utaratibu wake ukifuatwa vizuri lengo litafikiwa. Hata hivyo, ni bahati mbaya kwamba wapo watu kadhaa wenye nyadhifa serikalini ambao ama kwa maksudi au kwa kutouelewa Umagufuli wanautekeleza vibaya na wanautumia kukandamiza haki za wafanyakazi walioko chini yao na raia ambao taasisi zao zinapaswa kuwahudumia.

Kwa kuiona hatari inayolikabili taifa kutokana na upuuzi huu, kwa niaba ya jumuiya ya wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, natoa wito kwa watu hao waache mara moja kumtafsiri vibaya rais na wakome kutumia kisingizio cha Umagufuli kuminya na kudhulumu haki za watu na kuharibu kazi za ujenzi wa Taifa, kwa kuvunja morali wa watumishi ambao ndio chachu ya kuiletea Tanzania maendeleo yaliyolengwa na Serikali.

Kwa sasa katika Taifa hili, tumekuwa mashuhuda wa vituko vya viongozi, watawala na mameneja wa kada mbalimbali (baadhi yao wateule wa Rais) wanavyowadhalilisha Watanzania kwa matusi na kejeli hadharani, wakidhani kwa kufanya hivyo wanaendana na Umagufuli wa kutumbua majipu.

Wanafanya hayo bila kutambua kwamba vitendo hivyo vinavunja haki za binadamu na ni kinyume na misingi ya uadilifu ya nchi hii iliyojengwa kwa muda mrefu na inayozingatia kuwa kila mtu anastahili heshima, kuthaminiwa, kusikilizwa na kutambuliwa utu wake.

Wakati hayo yakionekana hadharani, yapo mabaya mengine yanayoendelea chini kwa chini ndani ya ofisi za umma. Mathalani, kwa kutumia kisingizio cha kusafisha kada ya utumishi wenye nyadhifa wanaminya haki mbalimbali za wafanyakazi, zikiwemo kupandishwa vyeo kazini, kutambua hatua za kujiendeleza kwao kitaaluma, kupata nyongeza za mishahara, kutengewa malipo yao ya pensheni na kuyawasilisha kunakostahili, kupewa stahiki za kuajiriwa kwa mara ya kwanza, stahiki za safari na nyinginezo.

Watu hawa kila mara wanapodaiwa kutoa haki hizo, wanakimbilia haraka kusema, Rais Magufuli bado anaendelea na zoezi la kusafisha kada ya utumishi na hivyo stahiki hizo zimesimama. Kisingizio hiki sasa kinaonekana kuwa endelevu na sugu.

Wenye nyadhifa hawa hawajali kwamba kuminya haki za watumishi kunatayarisha mgogoro mkubwa kati ya mwajiri na mwajiriwa. Baadhi ya hawa wanaosingizia Umagufuli, wamekuwa na tabia hiyo hiyo ya dhuluma na wivu hata kabla Rais Magufuli hajaingia madarakani. Ushahidi wa hili, ni madai lukuki ya wafanyakazi ambayo mengine ni ya zaidi ya miaka kumi nyuma. Wakati ule walitengeneza visingizio mbalimbali, sasa hivi wamepata kisingizio kikuu; Umagufuli.

Wapo pia ambao sasa wametunga sera mpya mbalimbali za kuwaongezea watumishi makato kedekede kwenye mishahara yao kwa kisingizo kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imewaagiza wasitegemee sana ruzuku ya Serikali/OC na wala wasilalamike kwamba haitoshi, bali wabuni vyanzo mbadala vya fedha za ndani. Kwa kutumia akili isiyoweza kuona madhara hasi ya wanachokifanya, wabaya hawa wamebuni kwa mfano, kuongeza kodi ya nyumba wanazokalia watumishi na kuongeza ada ya kazi za ushauri wa kitaalamu wanaoutoa watumishi.

Licha ya kodi hizo mpya za nyumba kutoendana kabisa na hali ya nyumba zenyewe, zimepangwa bila kuhusisha utaalamu wa wakala wa majengo na zinathibitisha tafsiri yao mbaya ya kanuni za utumishi wa umma (standing orders) za mwaka 2009.

Kadhalika, wakijua kuwa utoaji wa ushauri wa kitaalamu kutoka katika taasisi wanazoziongoza umeshuka na wakiwa wanafahamu fika jinsi ada au kodi kubwa zilivyo na kawaida ya kukimbiza/kufukuza uwekezaji, kushusha utoaji huduma na kusababisha ukwepaji kodi, wameongeza ada hizo kiukaidi.

Kana kwamba haitoshi, mabingwa hawa wa kuutumia Umagufuli vibaya, wamekuwa wakiwakata watumishi kiasi fulani katika mishahara yao wakidai ni wa ajili ya kulipia deni la mikopo ya elimu ya juu. Makato hayo hayawasilishwi katika bodi ya mikopo na wanapobainika hawana maelezo ya kulidhisha kwanini walifanya hivyo, na wala hawana mipango ya kurejesha fedha zilizokatwa. Hakika Umagufuli sana unatumiwa hadi kwenye wizi wa mapato ya wafanyakazi.

Katika harakati zao potofu zinazotokana na kisingizio cha kubana matumizi, mabosi hawa ni mabingwa wa kuunganisha idara zilizoko katika ngazi za chini, ilihali wakibuni vyeo na madaraka mapya katika ngazi za juu wanakopatikana wao.

Wamekuwa wepesi kuziambia ngazi za chini zisifanye matumizi mbalimbali, ilihali wao wanaendelea na matumizi makubwa, yakiwemo posho kubwa za vikao na utumiaji wa magari ya kifahari/ yenye gharama kubwa za uendeshaji.

Licha ya kwamba wanajinasibu kuwa watekelezaji wa utaratibu wa ugatuaji madaraka, linapokuja suala linalohusu fedha, chochote kinachozalishwa ngazi za chini wamejiwekea mamlaka ya kukitawala kana kwamba ngazi zinazokizalisha hazina uwezo wa kupanga kitumikeje.

Baadhi ya wapotoshaji hawa wa Umagufuli, waliitumia nafasi ya kuwaondoa kazini watumishi wasiokuwa na vyeti halali kuwaonea na kuwakomoa wafanyakazi ambao walikuwa na visa nao, vingi vikiwa visa binafsi. Miongoni mwa walioonewa ni wale waliokata rufaa baada ya kuondolewa kazini. Bahati mbaya zaidi kwa baadhi yao, hawajaweza kurudi kazini hata baada ya kuthibitisha wanavyo vyeti halisi na halali.

Hata Umagufuli wa kutumbua majibu na kunyamazisha siasa kuna baadhi ya mabosi wamegeuza rungu la kutishia yeyote anayehoji chochote au anayedai haki yake. Imekuwa kawaida yao sasa kuwatamkia/kuwatishia wafanyakazi kwa kauli ya ‘nitakutumbua’.

Tunasisitiza wito wetu kwamba, visingizio hivi vikome mara moja. Umagufuli si unyanyasaji wala upindishaji wa haki. Mabosi, viongozi na wakuu wa taasisi watimize wajibu wao, watende haki na wawapatie wafanyakazi stahiki zao.

Endapo wapotoshaji hawa hawatakoma, wanataaluma tutakuwa tayari kufanya pamoja na mambo mengine, yafuatayo; kutangaza mgogoro na wao; kuwaanika mmoja mmoja kwa majina, vyeo na taasisi wanazoziongoza na kuunga mkono jitihada halali za kuhakikisha wanatumbuliwa wao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles