25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

UKAWA YATOA MASHARTI KUSHIRIKI UCHAGUZI

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


VYAMA vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), vimetishia kususia uchaguzi mdogo uliopangwa kufanyika Januari 13, mwakani endapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), haitausogeza mbele ili kutoa nafasi ya kufanya tathmini ya uchaguzi uliopita.

Uchaguzi huo unatarajiwa kuhusisha majimbo ya Longido, Singida Kaskazini, Songea Mjini na kata sita.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, baada ya kikao cha pamoja, Mwenyekiti wa  Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, alisema uchaguzi mdogo uliofanyika Novemba 26, mwaka huu, ulikuwa na kasoro nyingi

“Umoja wetu umetafakari sana na kuona uchaguzi wa Januari 13 hauna sifa ya kuendelea. Kuendelea kushiriki chaguzi za kuumiza watu hakujengi bali kunaliumiza Taifa.

“Waite meza ya mazungumzo, vyama, msajili wa vyama vya siasa,tume, vyombo vya ulinzi na usalama tukae tujadili mustakabali wa nchi yetu tulipotoka, tulipo na tunakoelekea. Kama watakataa waendelee wenyewe na uchaguzi lakini sisi hatutashiriki,” alisema Mbowe.

Alisema uchaguzi unapokosa kuwa na uhalali, huru na wa haki unajenga chuki na mfarakano mkubwa katika Taifa.

“Vyama vya siasa hujengwa na kuimarika pale ambapo vina uhuru wa kufanya kazi za siasa, wanataka tukashiriki uchaguzi wakati wametufunga mikono kwa miaka miwili…wanataka tukashindane lakini sisi haturuhusiwi kujenga vyama vyetu,” alisema.

Alisema pia wataendelea kudai katiba mpya na kupigania utawala unaoheshimu katiba, sheria na haki za binadamu.

CUF

Naye Julius Mtatiro, alisema busara ni kushiriki majadiliano ya pamoja ili kuondoa kasoro zilizojitokeza katika uchaguzi uliopita na kuhakikisha uchaguzi ujao unakuwa huru na wa haki.

“Palikuwa na matatizo mengi sana katika uchaguzi wa juzi, Nec iahirishe uchaguzi ujao halafu iite wadau mezani tujadiliane tunayatuaje yale yaliyotokea,” alisema Mtatiro.

CHAUMMA

Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Eugene Kabendera, alisema uchaguzi uliopita walishiriki lakini kasoro zilizojitokeza zimewasukuma kuungana na wenzao ili kudai haki.

“Miaka 25 tangu mfumo wa vyama vingi urejeshwe, sasa unarudishwa nyuma kwa kasi ya ajabu, ndio maana tumeona tuunganishe nguvu na wenzetu kudai madai ya msingi,” alisema Kabendera.

NLD

Katibu Mkuu wa Chama cha National League for Democracy (NLD), Tozzi Matwanga, alisema vyama ambavyo havina wabunge vinanyimwa haki yao ya msingi ya kufanya siasa suala ambalo ni kinyume cha Katiba.

“Kuzuia mikutano ni dhambi ya kikatiba na sheria iliyoruhusu kuwepo kwa mfumo wa vyama vingi. Sisi ambao hatuna wabunge tunanyimwa haki yetu ya msingi ya kufanya siasa,” alisema Matwanga.

NCCR-MAGEUZI

Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Juju Danda, alisema anashangaa kuona Msajili akipita kukagua uhai wa vyama wakati majukumu muhimu ameyazuia.

“Tunachokidai kiko wazi, katiba inatupa haki ya kufanya kazi zetu, sheria ya vyama vya siasa na jeshi la polisi lakini leo msajili anapita kukagua uhai wa vyama wakati majukumu muhimu ameyazuia,” alisema Danda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles