27.9 C
Dar es Salaam
Monday, June 24, 2024

Contact us: [email protected]

UKAWA WASUSA, CCM WALA

Na MAREGESI PAUL – DODOMA

USEMI wa waswahili usemao ‘ukisusa wenzio wala’, ulijidhihirisha jana bungeni, baada ya wabunge wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kuwasusia wenzao saba wa CUF, waliokuwa wakiapishwa, huku wale wa CCM wakijitokeza kuwalaki kwa kuwaingiza katika ukumbi wa Bunge kula kiapo.

Hali hiyo ilijitokeza jana asubuhi kwenye kikao cha kwanza cha mkutano wa nane wa Bunge.

Wakati wa kula kiapo, wabunge wa upinzani hawakuingia isipokuwa watatu wa CUF, wanaomuunga mkono Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba.

Wabunge saba wa CUF walioapishwa jana, ni wale walioteuliwa na Lipumba baada ya kutengua uteuzi wa wengine wanane wa viti maalumu. Mbunge mwingine, Hindu Hamis Mwenda alifariki dunia wiki iliyopita.

Walioapishwa jana na Spika Job Ndugai ni Alfredina Kahigi, Kiza Mayeye, Nuru Bafadhili, Rukia Kassim, Shamsia Mtamba, Sonia Magogo na Zainab Amir.

Wabunge wa CUF waliokuwa ukumbini wakati wenzao wakila kiapo ni Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya, Maulid Mtulia (Kinondoni) na Maftaha Nachuma (Mtwara Mjini).

 

HALI ILIVYOKUWA

Wakati kiapo kikiendelea, wabunge wa CCM walikuwa wakiwashangilia na wengine kuwasindikiza kuingia bungeni kuelekea katika eneo la kuapishwa alikokuwa amesimama Spika Ndugai.

Wakati viapo na shamra shamra vikiendelea, wabunge wa upinzani wanaounda Ukawa, hawakuwamo bungeni na badala yake walikuwa nje wakiwa wamevalia nguo nyeusi walizosema zinaonyesha masikitiko kwa yanayoendelea bungeni.

Katibu wa Wabunge wa Ukawa ambaye pia ni Mbunge wa Momba, David Silinde (Chadema), aliwaambia waandishi wa habari kwamba hawatatoa ushirikiano kwa wabunge wapya walioapa.

“Kama mnavyojua, hatukuingia bungeni wakati wabunge wapya wakiapa kwa sababu hatukubaliani na uteuzi wao na tunapinga Bunge kutumiwa. Kwa hiyo, hatutawapa ushirikiano hadi pale kesi ya msingi ya kuwapinga iliyoko mahakamani itakapomalizika.

“Katika hili, tunataka Bunge liwe huru kama zilivyo mahakama za Kenya.

“Kuhusu mavazi meusi tuliyovaa leo, tumefanya hivyo ili kuonyesha hisia zetu na masikitiko ya kuapishwa kwa wabunge hao wakati wamepingwa mahakamani,” alisema Silinde.

 

SPIKA AFUNGUKA

Akizungumza baada ya ratiba ya kiapo kukamilika, Spika Ndugai alisema wabunge walikula kiapo baada ya taratibu zote kukamilika.

“Kwanza kabisa, napenda kuwapongeza wabunge wote wapya ambao awali mlikuwa wabunge wateule na sasa mmekuwa wabunge kamili. Bunge litawapa ushirikiano wote na naomba leo wapewe fomu za kuchagua kamati wanazotaka ili waanze kazi leo leo.

“Lakini pia, nawaomba wabunge msome Katiba ya nchi, kwani inaeleza namna ya kuwapata wabunge na nawahakikishia wabunge hawa wapya wamepatikana baada ya taratibu zote kukamilika,” alisema Ndugai.

Katika hatua nyingine, Spika Ndugai alionyesha kutoridhishwa na gazeti moja nchini ambalo hakulitaja jina, kwamba liliwahi kuandika yeye ni dhaifu ndiyo maana amekubali kuwaapisha wabunge hao wapya.

“Kuna gazeti moja liliwahi kuandika katika ukurasa wake wa katikati, kwamba ‘Spika huyu ni dhaifu’, lakini kama una akili zako, maneno kama hayo huwezi kuyafuata kwa sababu mimi si dhaifu,” alisema Spika Ndugai.

 

UTATA WALIOVULIWA UANACHAMA

Tofauti na ilivyozoeleka kuona chama cha siasa kikitangaza kumvua uanachama mbunge, hata mwaka hupita bado akiwa bungeni, safari hii kwa wabunge wa viti maalumu wa CUF hali ilikuwa tofauti kwani mchakato wote ulichukua siku nne pekee.

Hali hiyo ilizua minong’ono mingi ambayo hata hivyo haikuzaa matunda.

Julai 24, mwaka huu, Profesa Lipumba alitangaza kuwavua uanachama wabunge hao wanane na Julai 25, Spika Ndugai akatangaza kupokea barua ya kiongozi huyo.

Siku moja baadaye – Julai 26, Ndugai alitoa taarifa iliyoeleza kuridhia kufutwa uanachama kwa wabunge hao na Julai 27, Tume ya Taafa ya Uchaguzi (NEC), ikatangaza majina manane ya wabunge wapya kuziba nafasi za waliondolewa.

 

WABUNGE WALIOFUKUZWA

Wabunge wanane waliotangazwa kuvuliwa uanachama na Profesa Lipumba, ni Severina Mwijage, Saumu Sakala, Salma Mohamed Mwassa, Riziki Shahari Mngwali, Raisa Abdallah Mussa, Miza Bakari Haji, Hadija Salum Ally Al-Qassmy na Halima Ali Mohamed.

Pia wamo madiwani Elizabeth Sakala na Layla Madiba.

Miongoni mwa makosa yanayodaiwa kufanywa na wabunge hao na madiwani hadi kufukuzwa, ni pamoja na kukihujumu chama katika uchaguzi wa marudio wa madiwani wa Januari 22, 2017 na kumkashifu na kumdhalilisha Profesa Lipumba.

Makosa mengine ni kumkashifu Naibu Katibu Mkuu na Mbunge wa Kaliua, Sakaya na wakurugenzi wa chama hicho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles