27.1 C
Dar es Salaam
Monday, September 25, 2023

Contact us: [email protected]

BANDARI DAR KULETA SURA MPYA USAFIRISHAJI NCHINI

Na Shermarx Ngahemera

BANDARI ya Dar es Salaam inafanyiwa ukarabati na ujenzi mkubwa kuliko, kwa kupanua njia ya kuingilia na kuongeza kina, ujenzi wa gati na maghala ya mizigo na uboreshaji mkubwa pamoja na ununuzi wa vifaa vya kufanyia upakizi na upakuzi.

Upanuzi huo utahusu vilevile kujenga gati 0 ambayo itashughulikia shehena ya magari pekee.

Ni mradi mkubwa unaofadhiliwa kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia (WB) na DFID wa Sh bilioni 336 na kujengwa na Kandarasi ya China Harbour Construction Engineering, Shipping and Port Services Engineering.

Serikali ya Tanzania kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), imetiliana saini na Kampuni ya China, mradi uliosuasua kwa miaka mingi.

Kutokana na kauli za wahusika, mkataba huo ni wa kimkakati  kwani Sheria ya Manunuzi hutaka mkataba timilifu, lakini huo uliosainiwa ulikuwa bado kuna vipengele havijakamilika.

Kwa mujibu wa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, mkataba  huo wa Sh bilioni 336 ni kwa ajili ya kuongeza kina cha mlango wa Bandari ya Dar e Salaam na kuboresha na kupanua gati  namba 1-7 kwa huduma zinazotolewa .

“Hatima hiyo ni matokeo ya majadiliano ya muda mrefu na yatakuwa bado yanaendelea kujadiliwa kwani bei ya mradi ni ya juu na Serikali inataka ipunguzwe na kufikia bei ya uhalisia kamili na kutoa nafuu kwake na vilevile kutazama uwezekano wa kupunguza muda wa ujenzi kupungua kutoka miezi 36 ya makisio ya awali.

“Lakini Serikali inaendelea na mazungumzo na kampuni  hiyo iliyopata zabuni ili kupunguza  bei na kukamilisha mapema kabla ya muda uliokadiriwa awali,” anasema Waziri Mbarawa.

Swali kuu kwa wadau na wahusika ni kwanini watu wasaini mkataba ambao si kamilifu?

Haraka ndio iliyomuumiza chura kwani hakuna  la dharura katika hilo. Kufuatana na maelezo ya Waziri Mbarawa, haraka hiyo ni ili kupata uwezo wa ‘panamax’,  lakini katika taaluma ya usafiri wa meli,  meli kubwa au panamax  hutaka  kina cha zaidi  ya mita 20 kwa kile kinachoitwa ‘mothership’. Mradi wa Dar unatoa kina cha mita 15 tu na hivyo kaitafikia lengo lililokusudiwa.

Uboreshaji huo ni pamoja na ujenzi wa bandari  kavu Mkoa wa Pwani  katika Kijiji cha Ganta, karibu na stesheni ya Ruvu kilomita nane ndani upande wa kushoto wa kutoka barabara ya Morogoro kutokea Vigwaza kama unatoka Jiji la Dar es Salaam kuelekea Morogoro.

Shirika la Ujenzi la Jeshi la Suma JKT  ndio kandarasi ambapo mizigo ikishushwa kwenye meli  bandarini Dar, itawekwa kwenye mabehewa na kusafirishwa hadi Ganta, ambapo ndipo mizigo itakuwa inahifadhiwa na kuchukuliwa kwenda bara na nchi za jirani.

Maendeleo hayo yataua biashara ya Internal Container Depots (ICD) iliyo shamiri sana kwa miaka  zaidi ya kumi na kukoma kutokea pale Rais Magufuli alipotibua mnyororo wa wizi wa bandarini. Hadi sasa hakuna mizigo toka bandari inayopelekwa huko (ICD) na hakuna anayehuisha upya leseni kwa kukosa mzigo, kwani  bandari kavu hizo zinachofanya sasa ni kumalizia kuzitoa gari zilizopo kwa wenyewe na hakuna dalili ya kwenda kuchukua leseni ya Wakala wa Forodha kwani hakuna mizigo yoyote ya maana .

Serikali inalaumiwa kwa kufanya biashara yote yenyewe kwani  kama ilivyotakiwa na Kamati ya Makinikia ya Prof Osoro, Serikali imekubali kutekeleza  mapendekezo yote ikiwamo kufanya mabadiliko makubwa bandarini na hivyo iko mbioni kuirudisha Kampuni ya Wakala wa Meli (NASACO) ili kuleta utendaji bora kama mdhibiti  na mipango ya mzigo yaani ya Central Freight Bureau itarejeshwa ili nchi  idhibiti mwenendo wa mizigo kwa ile inayoingia na kutoka.

CFB itarudi ili kuweza kuweka mambo sawa yaliyopotoshwa na ubinafsishaji ambao  umeifanya nchi isiwe na kauli juu ya mwenendo na usafirishaji wa mizigo.

Inasikitisha kuona kazi zote  zimepokonywa na wenye  meli ambao wanazifanya  kama wakala kwa wenyewe na kwa hasara na matatizo mengi kwa Serikali na nchi kuiibia mapato  kwa kutoza huduma zisizotozwa kama kumkabidhi mwenye mali mzigo wake, anatozwa dola 50 hadi 100  kwa kila hati ya mzigo (bill of lading). Bandari inapoteza mapato kwa kufanya bei ndogo kwa mizigo yote  kutozwa bei moja ya kontena wakati makontena yanatofautiana (CBM).

“ TPA  na Sumatra zimelala na watu wenye meli wanafanya watakavyo, kwani hakuna mtu wa kuwaonesha kidole kwani NASACO ndio ilikuwa macho ya Serikali kimapato na kiusalama,” anasema Renatus Mkinga, Mjumbe wa Bodi  Mpya ya TPA na  mdadisi mkubwa wa masuala ya biashara ya bandari na usafirishaji.

Anasema wenye malori Dar es Salaam inabidi watafute biashara  nyingine kwani mzigo wote umehamia Ruvu na hivyo inabidi kutafuta muundo mwingine wa kufanyia kazi  kwani malori yatazuiwa kuingia jijini ili kupunguza msongamano wa magari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,717FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles