23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

WATOTO WALIOTEKWA WAKUTWA WAMEKUFA

Na JANETH MUSHI

-ARUSHA

JIJI la Arusha limekumbwa tena na simanzi, baada ya watoto wawili kati ya wanne waliotekwa hivi karibuni, kukutwa wakiwa wamefariki dunia.

Watoto Maureen David (6) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Lucky Vincent na Ikram Salim (3), miili yao ilikutwa jana kwenye kisima cha maji katika Mtaa wa Olkerian, Kata ya Olasiti jijini hapa.

Tukio hili, linakuja ikiwa ni miezi mitano tangu Mei 6, zaidi ya watoto 30 wa shule hiyo kufariki kwa ajali ya gari huko Karatu.

Maureen alitekwa Agosti 21 na Ikram, Agosti 25.

Babu wa Ikram, Kassim Hassan, alituma Sh 300,000 kwa watekaji kati ya Sh milioni 3 alizoambiwa atume ili mjukuu wake aachiwe, lakini hakuachiwa.

Jana mtuhumiwa wa utekaji, Samson Peter, aliongozana na polisi hadi kwenye eneo hilo na kuonyesha kisima cha maji kilicho nje ya nyumba moja eneo hilo ambacho alidai kuwa aliwaweka watoto hao.

Hata hivyo, haikufahamika kama aliweka watoto hao kwenye kisima hicho wakiwa hai ama la.

Mara baada ya mtuhumiwa kuwaonyesha polisi eneo hilo, wananchi walitaka kumvamia na kumpiga hatua iliyofanya aondolewe haraka.

Baada ya hatua hiyo, wananchi na waandishi wa habari walitolewa eneo hilo na kubaki askari polisi.

Lakini baadaye MTANZANIA lilishuhudia miili hiyo ikiwa imepakiwa kwenye gari la polisi na kuondoka eneo hilo, huku msafara ukiongozwa na gari la zimamoto.

Askari polisi mmoja, alilieleza gazeti hili kuwa miili hiyo ni ya watoto waliokuwa wametekwa, lakini hakuwa tayari kueleza kwa kina kwa kuwa yeye si msemaji.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alitafutwa kuthibitisha taarifa hizo, lakini simu yake iliita muda wote bila kujibiwa.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Olkerian, Kata ya Olasiti, Daudi Safari, ambaye awali ndiye aliyemdokezea mwandishi habari za miili ya watoto hao kukutwa kwenye eneo hilo, baada ya polisi kuondoka hakupatikana kutoa ufafanuzi.

Hata hivyo, awali kabla ya kupatikana kwa taarifa za miili hiyo kukutwa eneo hilo, aliliambia MTANZANIA kuwa  askari wawili wa upelelezi walienda katika chumba cha Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Masorogo Msibha, ambaye alikuwa akiishi na Samson na kufanya upekuzi.

“Polisi wakati mwingine wanashindwa kutoa ushirikiano,  kwa mfano jana (juzi), tuliwaeleza kuwa dari la chumba alichokuwa analala mtuhumiwa limetobolewa na hatujui kule ndani kumewekwa nini.

“Wakaja wapelelezi wawili na yule askari wa FFU, badala ya kutushirikisha sisi, wakaenda kwenye ile nyumba, hatujui kama kuna kitu kilifichwa kule au vipi, tuliwahoji lakini hawakutupa majibu, ilifika mahali hadi lugha kati yetu na wao zilitofautiana, walitakiwa kutupa ushirikiano ili tujiridhishe wenyewe kuona kama kuna kitu kilikutwa au la,” alisema.

 

KABLA TAARIFA ZA VIFO

Awali David Njau, mzazi wa Maureen, aliliambia gazeti hili kuwa alipata matumaini ya kumpata mtoto wake baada ya kukamatwa kwa mtuhumiwa wa utekaji, Peter, lakini yalipotea baada ya kushindwa kuwaonyesha polisi alipo.

Mtuhumiwa huyo alikamatwa na polisi mkoani Geita mwanzoni mwa wiki.

“Tukafikiri mtuhumiwa amepatikana anaweza akasema watoto wako wapi, sasa alivyoshindwa tukapoteza matumaini, inaonekana kabisa watoto hawapo hai tena.

“Kwa kweli sisi kama wanaume tulijikaza, nikiwa na babu yake Ikram, tukasema basi hebu ngoja tushirikiane na polisi tuone wanatuambia nini na tutapokea taarifa hizo kwa namna gani.

“Kwa sasa mtuhumiwa ameshakamatwa, jambo la msingi aseme tu watoto wako wapi, hata kama wamekufa au amewafukia mahali, sisi tuambiwe tu kwamba watoto wapo au wamekufa, tuone kama wazazi tutachukua hatua gani nyingine,” alisema.

 

MAWASILIANO NA WATEKAJI

Kuhusu mawasiliano kati yao na watekaji, alisema mara ya mwisho kuwasiliana nao ni Agosti 27, kabla hawajatumiwa Sh 300,000 na babu wa Ikram na kuanzia hapo, simu zao hazipatikani tena na wakitumiwa ujumbe mfupi wa maandishi haufiki.

“Hatujawahi kuwasiliana nao tena, ukipiga simu haipatikani, hata tukituma ujumbe mfupi wa maandishi haufiki, hatujui kama wanatumia mitandao mingine au la, tunaendelea na sisi kuwatafuta hatukai kuwasubiri tu polisi, tunawasiliana pia na watu tofauti tofauti kuona kama wameona mtoto wetu,” alisema Njau.

Alisema juzi mtuhumiwa huyo akihojiwa na polisi, alidai kuwatelekeza watoto hao katika eneo la Njiro, lakini walipoenda nae hawakufanikiwa kuwaona jambo lililowaongezea hofu.

“Utekaji ni kitu ambacho kinapaswa kukemewa na ninyi vyombo vya habari, wazazi, Jeshi la Polisi na kuzungumzia ni namna gani watu (watekaji) wakamatwe kwa uharaka.

“Huyo kijana anayetuhumiwa kuteka watoto kiukweli sijawahi kumfahamu, sijui ni vipi alijua mtoto anakaa wapi na wazazi wake ni kina nani? Kiukweli tunashindwa kuelewa anafanya peke yake au nyuma yake kuna watu. Huyo kijana ni hatari sana kwa kweli,” alisema Njau.

 

BABU WA IKRAM

Naye babu wa Ikram, Hassan, alisema: “Polisi walienda na mtuhumiwa wakarudi, tulipowauliza walisema tuwaachie kazi wenyewe, wanasema wanaendelea kumhoji. Lakini licha ya kwenda huko (Njiro) hawajapata watoto, polisi wanaendelea kupambana naye.

“Kwa kweli hali ni ngumu, leo (jana) ni siku ya 11 mtoto hajapatikana, tuna majonzi, wazazi wana majonzi tunawazuia nyumbani hata kuja polisi kwa maana ni vilio. Inabidi nishughulikie suala hili mwenyewe.

“Licha ya polisi kusema wanaendelea kuwatafuta watoto, hata sisi tunawatafuta mitaani, maeneo ya huku kwetu Njiro, tunawatafuta kwa kupiga simu, kwingine tunalazimika kwenda kujaribu kuangalia kama tutawapata,” alisema.

 

 

TAARIFA YA POLISI
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Mkumbo alithibitisha jeshi hilo kushikilia watuhumiwa watatu na kudai taarifa kamili ya tukio hilo atatoa wiki hii.

Katika matukio hayo ya utekaji, watoto wanne walitekwa.

Watoto wawili; Ayub Fred (3) na Bakari Selemani (3) ambao wazazi wao wanaishi Mtaa wa FFU, Kata ya Muriet jijini hapa, walipatikana Agosti 28, baada ya watekaji kuwasiliana na wazazi wao kupitia balozi wa eneo hilo na kuwarudisha kwa pikipiki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles