Nora Damian – Dar es Salaam
WATOTO 17,000 wamefanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa mwaka 2017 huku matukio mengi yakifanywa na ndugu au jamaa wa karibu.
Katika kipindi hicho, maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi katika kundi la vijana yaliongezeka na kufikia asilimia 40, huku kwa mabinti pekee yakiwa ni asilimia 80.
Takwimu hizo zilitolewa juzi na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, baada ya kutembelea kijiji cha watoto kilicho chini ya shirika la kuhudumia watoto waliopoteza au walio kwenye hatari ya kupoteza malezi ya wazazi – SOS.
“Tumeanzisha kamati za ulinzi za watoto katika kila ngazi, lakini bado tuna changamoto kwa sababu wanaofanya matukio wengi wako ndani ya familia.
“Utakuta wanalipana faini, kupeana ng’ombe na wakati mwingine mtoto au mzazi anaweza kubadilisha maneno kupoteza ushahidi,” alisema Dk. Ndugulile.
Alisema watoto wengi hivi sasa ni yatima, na kwamba kuna ongezeko la watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani, hususan maeneo ya majiji kutokana na watu kuwatumia kama mtaji wa kupata fedha.
Kuhusu mimba za utotoni, alisema asilimia 27 ya mabinti wenye umri kati ya miaka 15 – 19 wana watoto au ni wajawazito.
“Mkoa wa Katavi ni asilimia 50, yaani ukiingia leba wodi utafikiri kwamba uko darasani, lakini hao ndio wazazi wetu,” alisema Dk. Ndugulile.
Naye Mkurugenzi wa SOS Tanzania, David Mlongo, alisema watoto 65 wamerejeshwa kwenye familia na jamii zao za asili kati ya mwaka 2017 na 2019 baada ya mazingira kuwa rafiki.
Alisema walirejeshwa kupitia programu ya malezi kwenye mfumo unaoshabihiana na familia ya kawaida, ambao hadi sasa watoto 612, kati yao wasichana 308 na wavulana 304 wanaendelea kupata malezi.
“Tumekuwa tukifanya utetezi wa haki za watoto wanaopata malezi nje ya mfumo wa familia ili kuhakikisha wale ambao hatua zote za kufanya wapate malezi ndani ya familia zimeshindikana ndiyo wapelekwe kwenye malezi mbadala,” alisema Mlongo.
Alisema pia kupitia programu ya kujenga uwezo wa familia, wamewafikia watoto na vijana 34,418 kuanzia mwaka 2015 hadi sasa, ambao wamenufaika na huduma za elimu, afya na kuboresha pato la familia kuziwezesha kumudu mahitaji ya msingi.
Mkurugenzi huyo alisema kijiji cha Dar es Salaam hadi sasa kinahudumia watoto 120 na kati yao wavulana ni 66 na wasichana ni 54 na kwamba kina kina mama 13 wanaosaidiwa na walezi nane.
Mlongo alisema kati ya watoto hao, sita wapo chini ya umri wa kuanza shule, 14 wako shule ya awali, 56 shule ya msingi, 50 sekondari na wengine 40 katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi.