25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Asilimia 95 ya wakazi wa kata moja Misenyi wahamiaji haramu

Mwandishi Wetu – Misenyi

MKUU wa Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera, Kanali Denis Mwila, amesema asilimia 95 ya wakazi wa Kata ya Kakunyu wilayani hapa ni wahamiaji haramu.

Kanali Mwila akizungumza mbele ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, alisema sababu kubwa ni kuletwa kwa wahamiaji hao kutafuta ajira na maeneo ya malisho ndani ya ranchi ya taifa.

“Tumekuwa na matukio ya kukamatwa kwa wahamiaji haramu katika wilaya yetu. Mfano katika Kata ya Kakunyu watu 6,630 walisajiliwa huku raia halali wakiwa 319 tu, hivyo asilimia 95 ya wakazi hao si raia au uraia wao una shaka.

“Wahamiaji hao ni gharama kuwahudumia, maana bado wana haki ya kuhifadhiwa na kupata mahitaji yote ya kibinadamu,” alisema Kanali Mwila.

Wakizungumza mbele ya Naibu Waziri, wahamiaji hao waliomba kupatiwa nauli ili warejee katika nchi zao, huku wengine wakitaja  sababu ya kuingia nchini kinyume na sheria ni kutafuta ajira na kukimbiwa na wenza wao.

Kutokana na hali hiyo, Masauni alitaka Idara ya Uhamiaji na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), kuongeza nguvu kazi katika Wilaya ya Misenyi.

 “Kuna haja ya kuleta nguvu kazi kubwa sana kutoka Idara ya Uhamiaji na Nida, lazima tuwe na takwimu halisi ya kila mtu aliyeko katika maeneo haya ambayo yana shaka.

“Nchi yetu inakaribia kufanya Uchaguzi Mkuu ndani ya mwaka huu, tunahitaji kuwa salama ili kuweza kufanya uchaguzi pasi na shaka yoyote ya uvunjifu wa amani.

“Tatizo hili ni kubwa, linahitaji utatuzi wa haraka ili kuepuka madhara huko mbeleni,” alisema Masauni.

Akitoa taarifa ya Idara ya Uhamiaji kwa kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka jana, Mkuu wa Wilaya ya Misenyi, Kanali Mwila, alisema ilitoa hati za dharura za kusafiria 1,276 zenye thamani ya Sh milioni 25.52 huku makusanyo hayo yakikisiwa kuwa ni wastani wa Sh milioni 2.12 kwa mwezi.

Alisema idara hiyo pia ilikamata wahamiaji haramu 206 kwa kipindi hicho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles