27 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Ujenzi wa vyumba vya madarasa Jiji la Dodoma wafikia asilimia 90

* Madarasa kukabidhiwa kesho

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

UJenzi wa Vyumba vya madarasa katika Jiji la Dodoma kwa kutumia fedha za Uviko-19 umefikia asilimia 90 huku Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Antony Mtaka akiutaka uongozi wa Jiji hilo kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana.

Aidha, ameagiza kukamilika kwa ujenzi wa vyumba hivyo kwa wakati ili wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza waweze kusoma.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru, amesema wanatarajia kukabidhi madarasa hayo kesho (Oktoba 24, 2021) yakiwa yamekamilika.

Itakumbukwa, hivi karibuni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu aliwaagiza Wakuu wa Mikoa kote nchini kuhakikisha mpaka ifikapo Desemba 30, ujenzi wa vyumba hivyo uwe umekamilika.

Kutokana na hali hiyo Jumatano Desemba 22, 2021 Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dodoma ilifanya ziara ya kukagua ujenzi wa vyumba hivyo katika Jiji la Dodoma ikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Antony Mtaka.

Kamati hiyo ilitembelea shule za Sekondari za Miyuji, Umonga, Kiwanja cha ndege, Viwandani, Itega na Dodoma Sekondari ikiwa ni pamoja na kukagua karakana zinazotengeneza Madawati.

Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo, Mtaka amesema ujenzi wa vyumba hivyo umefikia asilimia 90, hivyo amewataka wazazi na walezi ambao watoto wao wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kuhakikisha ifikapo Januari 17 mwaka 2022 wanakuwa shuleni.

“Hili sio ombi nasisitiza kwa jinsi mradi wa ujenzi wa vyumba hivi vya madarasa unavyoendelea, mmenihakikishia mmefikia asilimia 90 ya ujenzi nataka Januari 17, 2021 watoto wote waripoti shuleni ili wapate haki yao ya msingi kwa maslahi yao na taifa kwa ujumla,”amesema Mtaka.

Aidha, Mtaka amesema ni vyema ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa ukazingatia suala zima la upandaji miti ili kuweza kutunzaji mazingira.

“Sasa nipende kuwaagiza kuwa lazima ujenzi huu uendane na thamani ya pesa kama Mheshimiwa Rais ambavyo amekuwa akisistiza kila siku lengo hapa ni kuona watoto wetu wananufaika na miradi hii,” amesema Mtaka.

Hata hivyo, ameutaka Uongozi wa Jiji la Dodoma kuhakikisha wanakamilisha ujenzi huo wa vyumba vya madarasa kwa wakati  ili watoto wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza waweze kusoma.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Fatma Mganga, amesema Dodoma ilikuwa na upungufu wa madarasa ya sekondari 601, hivyo ujenzi wa madarasa hayo utasaidia kupunguza tatizo la vyumba vya madarasa katika mkoa huo.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Jabir Shekimweri, amesema wanatarajia kupokea wanafunzi 10,755 wa kidato cha kwanza mwaka 2022 ambapo watahakikisha wote wanapata haki yao ya msingi ya kusoma.

Mstahiki Meya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe amesema Jiji litaendelea kutenga bajeti ya ujenzi wa madarasa lengo likiwa ni kukabiliana na tatizo la uhaba wa madarasa.

Awali, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru, ameihakikishia Kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Dodoma kuwa hadi ifikapo Desemba 24, Mwaka huu watakabidhi Madarasa hayo.

“Sisi kama Jiji tunajitahidi katika kutekeleza mradi huu na tunamshukuru sana mheshimiwa Rais kuona umuhimu wa watoto ambao walikuwa wanakosa nafasi kuweza kusoma,”amesema Mafuru.

Naye, Kaimu Afisa Elimu Sekondari wa Jiji la Dodoma, Fredrick Mwakisambwe akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa madarasa 147 yanayotekelezwa kupitia Mradi huo wa uviko 19 katika Halmashauri hiyo amesema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imefanya juhudi kubwa ya utekelezaji wa miradi hiyo.

“Miradi hii inafanyika kwa kuzingatia kiwango cha ubora na thamani ya fedha inaonekana  ambapo ujenzi huo unaenda sambamba na utengenezaji wa madawati,”amesema

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles