25.5 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Ugaidi Tanga Siri nzito

OSCAR ASSENGA, TANGA
WAKATI nchi ikiwa bado kwenye taharuki ya mashambulio yanayodaiwa kufanana na ya kigaidi yaliyotokea katika Kijiji cha Mleni nje kidogo ya Jiji la Tanga, kumezuka madai mapya yanayowashutumu viongozi wa Jeshi la Polisi kwa kushindwa kutoa uamuzi wa haraka kudhibiti wahalifu hao.
Uzembe huo unadaiwa kufanywa na uongozi wa polisi makao makuu Dar es Salaam pamoja na Tanga na hivyo kutoa fursa kwa wahalifu kufanya mashambulio na baadaye kutoroka.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya jeshi hilo mkoani Tanga kimelieleza MTANZANIA kuwa urasimu na uzembe ulichangia kwa kiasi kikubwa hatua ya kuwakamata wahalifu hao kushindwa kutekelezwa kama ilivyotakiwa.
Inadaiwa kuwa baada ya askari kufika kwenye eneo walilokuwapo wahalifu hao, walijaribu kujibizana nao lakini baada ya muda walibaini kuwa wahalifu walikuwa na silaha nzito kuliko zile walizokuwa nazo wao.
Chanzo hicho ambacho tunakihifadhi kwa sababu maalum, kilisema viongozi wa juu wa jeshi hilo Tanga na Dar es salaam walikuwa wakiwasiliana na askari waliokuwa katika eneo la tukio na kuwataka wawakamate wahalifu wakiwa hai jambo ambalo liliwawia vigumu kulitekeleza.
“Katika utendaji kazi wa jeshi mambo ni tofauti, karibu kila kitu kinafanywa kwa amri, kuna silaha ambazo askari wanaruhusiwa kuzitumia endapo watakutana na watu wanaowashambulia.
“Silaha nyingine huwezi kuzitumia mpaka upate amri ya wakubwa wako, baadhi ya silaha hazitumiki kabisa bila amri ya rais wa nchi.
“Wale walivyofika pale walianza kushambuliwa na wao wakajibu mapigo lakini baada ya muda walijua wale wenzao wana silaha nzito kuliko wao.
“Wakajaribu kuomba kibali cha kutumia silaha nzito zaidi lakini walinyimwa wakaambiwa wahakikishe wanawakamata hao wahalifu wakiwa hai,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya jeshi la polisi.
Chanzo hicho kilisema kuwa baada ya askari kuzidiwa walilazimika kurudi nyuma ili kujipanga hatua ambayo ilitoa mwanya kwa wahalifu kutokomea kusikojulikana.
Haa hivyo tukio hilo linalodaiwa kuwa ni la kigaidi lilikanushwa na Kamishna wa Polisi Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja ambaye alisema juzi kuwa wahusika ni majambazi na si magaidi kama inavyovumishwa na baadhi ya wananchi jijini Tanga.
Wakati hali Tanga ikiwa hivyo, kuna video zinazosambazwa katika mitandao ya jamii ambazo inasikika sauti ya mtu akitamba kuwa yeye na kundi lake la ugaidi ndiyo wanahusika kuteka vituo vya polisi nchini.
Alipotafutwa jana kuzungumzia masuala hayo Mkuu wa Jeshi la Polisi, (IGP) Ernest Mangu hakuweza kuzungumza suala hilo badala yake alitaka mwandishi amfuate ofisini kwake.
“Nitajuaje kama wewe ni mwandishi na kama wewe ndiyo unayesambaza video hizo?” aliuliza.
Alipotakiwa kueleza alipo ili mwandishi aweze kumfuata alisema “mzee njoo kesho kwa msemaji wa jeshi atakupa taarifa.”
MTANZANIA lilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Fresser Kashai kuzungumzia taarifa hizo hakupokea simu yake na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu ya mkononi hakujibu.
Naye Msemaji wa jeshi hilo, Advera Senso alisema baada ya taarifa zilizotolewa juzi na Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi hilo, Paul Chagonja, hakuwa na taarifa nyingine tofauti.
Kuhusu video zinazosambazwa kwenye mitandao pamoja na usahihi wa kifo cha askari ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) anayedaiwa kuuawa na wahalifu hao, Senso alisema:
“Ndiyo maana nikakwambia taarifa yoyote ikipatikana tutatoa na wewe uwe kama mwana usalama na Mtanzania pia, ninavyokuambia hivi unielewe.”
Changoja kwa muda wote gazeti hili lilipojaribu kumtafuta kupitia simu yake ya kiganjani alikuwa hapokei simu yake.
JWZ haina taarifa ya kifo cha askari wake
Wakati taarifa zikieleza kuwa askari wa JWTZ aliuawa kwenye mashambulio ya kurushiana risasi na wahalifu huko Tanga juzi, Msemaji wa Jeshi hilo, Meja Joseph Masanja alisema hawana taarifa rasmi juu ya tukio hilo.
Alisema taarifa hizo naye amekuwa akiziona kwenye vyombo vya habari lakini jeshi hilo bado halina taarifa zozote.
“Kifo siyo jambo la siri, sisi zaidi ya kuona kwenye vyombo vya habari hatuna taarifa zozote juu ya kifo hicho, tukipata tutasema kama ambavyo tumekuwa tukifanya… hata pale askari wetu walioko Darfur walivyofariki dunia tulisema,” alisema.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Said Magalula, alisema atazungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio hilo leo.
Wananchi walikuwa wakionana na wahalifu hao kila siku
Baadhi ya wananchi wa eneo hilo ambao hufanya kazi za kupasua mawe, walisema kila siku walikuwa wakipishana na wahalifu hao lakini hawakuwa na wazo kama ni watu wabaya.
Akizungumza na MTANZANIA, mkazi wa eneo hilo, Mustapha Bakari, alisema kila siku asubuhi walipokuwa wakienda kwenye shughuli zao za kupasua mawe, walikuwa wakipishana na watu wawili waliokuwa wakitokea maeneo hayo.
“Ki ukweli kuna watu wawili ambao tulikuwa tukipishana nao kila siku wakati tukiwa tunakwenda kwenye shughuli zetu za upasuaji wa kokoto lakini sisi hatukujua wanafanya nini kwa sababu walikuwa ni watu wa kawaida tu ambao huwezi kuwadhani vibaya lakini tangu juzi hatujawaona tena,” alisema Bakari.

Wananchi, polisi wafanya doria
Habari zinasema kabla JWTZ hawajafika eneo la tukio, wananchi wanaoishi kwenye eneo hilo waliombwa kushirikiana na askari kuimarisha ulinzi.
Wananchi walisema polisi mmoja aliwafuata vijana wanaoishi karibu na eneo hilo na kuwaonyesha eneo wanaloweza kukaa na kuimarisha ulinzi.
Wananchi hao walifanya kazi hiyo hadi askari wa JWTZ walipofika.
“Baadhi ya watu wamekwisha kuhama maeneo haya kutokana na kukumbwa na hofu kubwa ya mashambulio ingawa sisi tupo hapa hatujui la kufanya,” alisema mwananchi mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Emanuel.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles