24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Kocha Pluijm: BDF hawatoki Taifa leo

PluijmNA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM

KOCHA wa timu ya Yanga, Hans van Pluijm, amewaondoa shaka mashabiki wa timu hiyo kuelekea mchezo wao dhidi ya BDF XI ya Botswana utakaofanyika leo na kueleza kuwa timu yake itawafunga Wabotswana hao.

Yanga itachuana na BDF kwenye mchezo wa hatua ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni leo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana mbele ya waandishi wa habari kwenye mkutano wa makocha wa pande hizo mbili, Pluijm alisema atahakikisha anaiongoza vizuri timu yake kwa kuifunga BDF ili kuipeperusha vema bendera ya Tanzania.

“Najua mchezo utakuwa mgumu, lakini nataka kushinda na kuwafurahisha mashabiki wetu na Watanzania kwa ujumla kwani hatuiwakilishi Yanga pekee bali Tanzania nzima.”

“Timu tunayokutana nayo ni ya jeshi, hivyo najua timu za hivyo huwa wanatumia nguvu kubwa mchezoni, lakini nimewaandaa wachezaji wangu kukabiliana na hali hiyo na pia nitatumia staili ya kucheza kwa kushambulia tu na kucheza kwa nidhamu,” alisema.

Pluijm alisema wachezaji wake wote wako fiti kwa ajili ya mchezo huo, huku habari njema zaidi ni kupona kwa nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliyekuwa mgonjwa.

“Cannavaro yupo fiti asilimia 100 kucheza pambano hilo,” alijibu Pluijm baada ya kuulizwa kama hali ya mchezaji huyo imetengamaa.

Naye kocha wa BDF, Meja Letang Kgengwenyang ‘Rasta’, alisema wamekuja Tanzania kama timu dhaifu ‘underdog’ na kudai kuwa malengo yao ni kuhakikisha wanapata mabao mawili ya ugenini au moja ili kujiweka vizuri kwenye mchezo wa marudiano.

“Tunaingia kwenye mchezo huo tukiwa na maandalizi ya wiki sita, ambapo tulikuwa tukiiandaa timu kwa mazoezi ya nguvu, saikolojia pamoja na mbinu za mchezo, hivyo hatujaja Tanzania kujilinda zaidi bali tumekuja kushambulia na kupata mabao mawili au moja ya ugenini.”

“Hiyo itatusaidia kwenye mchezo wetu wa marudiano, vilevile tutacheza staili yetu ya uchezaji ya ‘total football’ yaani tunashambulia wote na kuzuia wote ila hatutacheza mchezo wa kujilinda zaidi,” alisema Rasta.
Kikosi cha BDF kinaundwa na wachezai sita wanaocheza timu ya Taifa ya Botswana akiwemo nahodha wao, Apache Thuma, huku pia wakiwa na wachezaji watatu wa kigeni wakitokea nchini Zimbabwe.

Yanga inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) ikiwa na pointi 25 sawa na vinara Azam FC, ilitupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita na timu ya Al Ahly ya Misri katika raundi ya pili.

Yanga ilitolewa baada ya kufungwa kwa mikwaju ya penalti 4-3 kufuatia mechi zote mbili kuisha kwa matokeo ya jumla ya bao 1-1, kila timu ilishinda bao 1-0 kwenye mchezo wa nyumbani.

BDF yenyewe itakuwa ni mara ya pili kucheza na timu ya Tanzania baada ya mwaka 2003 kufungwa na Simba kwa jumla ya mabao 4-1 kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba ilishinda bao 1-0 nyumbani na kuifunga tena 3-1 ugenini.

Mechi ya marudiano ya Yanga na BDF itafanyika jijini Gaborone, Botswana Februari 27, mwaka huu na kama Yanga itafanikiwa kuwatoa basi itakutana na mshindi wa jumla wa mechi itakayowahusisha Sofapaka ya Kenya na Platnum ya Zimbabwe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles