28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Matokeo kidato cha nne Wanafunzi wamefaulu, wamefaulishwa?

dk-charles-e-msondeNA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM
WAKATI maelfu ya wanafunzi waliohitimu Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2014 wakiwa wanasherehekea matokeo yao, baadhi ya wadau wa elimu wameonyesha wasiwasi wao juu ya kuongezeka kwa ufaulu huo wakati hali ya shule na changamoto zake zikiwa zinaongezeka.
Kwa mujibu matokeo yaliyotangazwa juzi na Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani (Necta), Dk Charles Msonde, ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 58.25 mwaka 2013 mpaka 68.33 mwaka 2014.
Wadau hao walisema baada ya serikali kuona elimu imekuwa ikishuka kila mwaka, badala ya kuweka mikakati ya kuinua elimu, walianzisha mipango mbalimbali ambayo tangu mwaka juzi imekuwa ikionyesha matokeo yanapanda.
Walisema mipango hiyo ni pamoja na kubadilisha madaraja ya ufaulu.
Malengo ya BRN

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa katika hotuba aliyoitoa kwenye warsha ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) katika sekta ya elimu ya watendaji wa elimu ngazi ya kanda, mkoa na wilaya, aliainisha malengo ya kupandisha ufaulu.

Alisema kwa mwaka, ufaulu kwa shule za msingi ulitakiwa kupanda kutoka asilimia 31 mpaka 60 huku kwa sekondari ukitakiwa kupanda kutoka asilimia 43 hadi 60.

Wizara hiyo ilijipangia pia kufikisha ufaulu huo asilimia 70 mwaka 2014 na 80 kwa mwaka 2015.

Haki ya Elimu
Meneja Utafiti Uchambuzi wa sera, Boniventure Godfrey kutoka HakiElimu, alisema wanashtushwa na ongezeko la matokeo lililotokea kwa kasi katika miaka miwili ya hivi karibuni.
Alisema kwa picha iliyotolewa inaonyesha kwamba matokeo yamepanda kwa asilimia 10 ikilinganishwa na mwaka 2013 ambao yalikuwa asilimia 58 na sasa imepanda na kuwa asilimia 68.
“Nadhani kwa sababu sisi tumekuwa tukiyafuatilia matokeo kuanzia mwaka 2005 hadi 2006 na tumebaini namna ambavyo hali ya elimu ilivyokuwa ikishuka na shule kuwa na changamoto mbalimbali, sasa haya yanayokuja yanashtua kidogo.
“Katika miaka hii miwili tumeelezwa mabadiliko mengi, mara ya GPA (mfumo wa upangaji wa wastani kwa kutumia Pointi), mabadiliko ya E; kwa hiyo yana changamoto nyingi sana na hatujui kinachokuja na tunaona kabisa ni mitego ya uchaguzi ili wazazi wafurahie matokeo,” alisema Godfrey.
Alisema hakuna chochote kikubwa kwa ajili ya uwekezaji wa elimu chenye nia ya kuhakikisha matatizo yanaondolewa.
“Ilitakiwa matokeo yasieleze kwa ujumla jumla ila yaeleze hasa wangapi ambao wanaelekea kidato cha sita na wala si kusema kwa ujumla waliofaulu kwani hata wanaopata ‘division four’ wanahesabika kama wamefaulu ingawa hawawezi kwenda kidato cha tano,” alisema Godfrey.
Alisema serikali imekuwa ikipambana kuonyesha yamepatikana mafanikio katika mpango wake wa BRN ambako mwaka jana walijipangia kupata asilimia 60 na hivyo walipata asilimia 58.25 na mwaka huu walijipanga asilimia 70 na wametangaza kupata asilimia 68.33.
Profesa Sylvester Kajuna
Msomi wa Chuo Kikuu cha kumbukumbu ya Hubert Kairuki, Profesa Sylvester Kajuna akizungumzia matokeo hayo, alisema Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) hauwezi kuokoa elimu ya Tanzania.
Alisema mtindo unaotumika unakuwa tatizo kutokana na ulipuaji wake kwa sababu unashindwa kuwasaidia wanafunzi kufika mbali na kupata wanafunzi wenye uwezo mzuri.
“Mambo haya yanafanywa kisiasa kwa nia ya kuonyesha kwamba tunaendeelea katika elimu huku ukweli ni tofauti na dhamira hiyo inachangia kuwa na wanafunzi wasiokuwa bora katika vyuo vikuu,” alisema.

TAMONGSO
SHIRIKISHO la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyo vya Kiserikali (TAMONGSO), Benjamin Nkonya, alisema ubora wa elimu hautokani na wingi wa ufaulu bali hutokana na ushindani katika soko la ajira.
“Maana yangu kuwa ubora wa elimu unatokana na soko la ajira ni kwamba hatutarajii kuona wasomi wetu hawathaminiwi kama inavyotokea hivi sasa viongozi wanapougua wanakwenda kutibiwa nje ya nchi,” alisema.
Nkonya alisema elimu itakapokuwa nzuri itawezesha wataalamu nchini kutumika bila ya kuwahofia kama inavyotokea sasa kwa kutowaamini.
“Limetokea suala la Escrow limepelekwa Uingereza kwa kutoaminiwa majaji wa kwetu…wahandisi bado wanaaminiwa kutoka nje,” alisema.
Alifananisha ufaulu wa mwaka huu sawa na kupanua magoli kwa nia ya kila mchezaji kufunga. Hivyo ndivyo ilivyotokea kwa kupunguza alama ili watahiniwa wengi waweze kushinda, alisema.
“Mipango hiyo mingi ambayo imekuwa ikitumika itakwisha baada ya kumalizika uchaguzi mkuu, serikali imeshindwa kutoa motisha kwa walimu wake na kubaki na mipango ambayo haina tija na kuinua kiwango cha elimu iweze kwenda sawa na shule za binafsi,” alisema.

DK. SLAA
Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilibrod Slaa aliyaponda matokeo hayo na kusema kuwa serikali imepanga kuzalisha taifa la wajinga.
“Hivi unaweza kupata matokeo makubwa sasa wakati shuleni hujapeleka daftari, mwalimu hujamlipa mshahara, hujapeleka chaki, hujapeleka vifaa vya maabara, walimu hawajalipwa malimbikizo yao, hilo haliwezi kufanikiwa eti kwa sababu una Matokeo Makubwa Sasa,” alisema Dk. Slaa.
Alisema inakuwa vigumu kuhusishwa kwa BRN na matokeo haya kwa sababu tangu kutangazwa kwa mpango huo hadi sasa bajeti imebaki kuwa ile ile, nyumba za walimu hazijajengwa, vitabu havijapelekwa.
“Kilichotokea ni serikali kushusha alama za ufaulu, hiyo iliwezesha watoto wengi kufaulu wakati uhalisi hawajafaulu hivyo tunatengeneza taifa la wajinga na mbumbumbu na wazazi wanafurahia kwa sababu hawajui kinachoendelea.
“Huu ni udanganyifu wa ajabu ambao utasababisha taifa kuangamia wakati wenzetu wanatengeneza wanasayansi, sisi tunatengeneza taifa la wajinga.
“Wenzetu wanapeleka watu mwezini na kwenye sayari mbalimbali sisi tunatengeneza wajinga, halafu bado tunashangilia watu wamefaulu hivyo inatubidi tuamke na kujiuliza maana ya alama hizo,” alisema.

Wizara ya elimu
Alipotafutwa msemaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzi ya Ufundi, Ntambi Bunyanzu alisema hayuko tayari kuzungumzia suala hilo kwa sababu kwa miezi mitatu hakuwapo kazini kutokana na kukabiliwa na ugonjwa.
“Sitaweza kuzungumzia suala hilo kwa sababu limetokea nikiwa nje ya ofisi kwa muda wa miezi mitatu lakini unaweza kuzungumza na kamishna wa elimu wa wizara anaweza kukusaidia,” alisema.
MTANZANIA lilipomtafuta Kamishna wa Wizara ya Elimu, Profesa Eaustelia Bhalalusesa, alisema hakuwa na nafasi ya kulizungumzia hilo kwa sababu alikuwa akiendesha kikao cha harusi hivyo ingekuwa bora kutafutwa leo wakati akiwa kazini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles