*Spika kupangua kamati, vigogo watano kupoteza nyadhifa zao
*Ndassa kuhojiwa Takukuru
NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
KAMATI za Kudumu za Bunge zinatarajiwa kufanyiwa mabadiliko makubwa ya viongozi na wajumbe wake wakati wowote kuanzia sasa, baada ya ripoti ya uchunguzi wa mwenendo wa wabunge kuwatuhumu baadhi yao kujihusisha na vitendo vya rushwa kutua mezani kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai.
Taarifa za uhakika zilizolifikia MTANZANIA kutoka ndani ya Ofisi ya Bunge, zinaeleza kuwa Spika Ndugai atawang’oa katika nyadhifa za uenyekiti na makamu wenyeviti wa watano wa Kamati za Bunge kutokana na tuhuma hizo za rushwa.
Hatua hiyo ni pamoja na kuhawamisha baadhi ya wabunge kutoka kamati moja hadi nyingine, kutokana na majina yao kutajwa na wengine kuhusishwa moja kwa moja na tuhuma za rushwa.
Imeelezwa kwamba, Spika Ndugai amelazimika kuchukua uamuzi huo baada ya kufikishiwa mezani ripoti ya uchunguzi uliofanywa na taasisi za kiuchunguzi za Serikali, kuhusu mwenendo usioridhisha wa baadhi ya wabunge hususan waliopewa dhamana ya kuongoza Kamati za Bunge.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge wanaotajwa kuvuliwa nyadhifa zao wakati wowote kutokana na tuhuma hizo ni Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Martha Mlata ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM).
Wengine ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji na Mitaji (PIC), Richard Ndassa, ambaye pia ni Mbunge wa Sumve (CCM) na Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, Dk. Mary Mwanjelwa ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM).
Makamu wenyeviti wanaotajwa kuwamo katika orodha ya kuondolewa katika nyadhfa zao ni Dk. Raphael Chegeni (Kamati ya Huduma za Maendeleo ya Jamii) ambaye pia ni Mbunge wa Busega (CCM), Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).
Vyanzo vya habari vya gazeti hili kutoka ndani ya Ofisi ya Bunge vimeeleza kuwa Spika Ndugai baada ya kufikishiwa ripoti yenye tuhuma dhidi ya baadhi ya wabunge, aliwaita ofisini kwake, wenyeviti wa kamati watatu ambao ni Mlata, Ndassa na Dk. Mwanjelwa pamoja na makamu wenyeviti wawili ambao ni Lugola na Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aeshi Hilaly (CCM), ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC).
Wabunge kadhaa wamelieleza gazeti hili kuwa sakata hilo limelitikisa Bunge kiasi cha kumlazimu Spika kuwaonya wenyeviti na makamu wenyeviti aliokutana nao ofisini kwake kuhusu nyendo zao baada ya majina yao kutajwa kwenye ripoti hiyo wakidaiwa kujihusisha na rushwa, huku Aeshi ambaye jina lake halimo kwenye orodha ya watuhumiwa akitakiwa kuwa makini yeye mwenyewe pamoja na wajumbe wake, kwa sababu kamati anayoingoza imekuwa ikikumbwa na tuhuma za namna hiyo kila mara.
Taarifa zaidi kutoka ndani ya Ofisi ya Bunge zimeeleza kuwa katika ripoti aliyokabidhiwa Spika Ndugai, kuhusu mwenendo usioridhisha wa baadhi ya wabunge, zimetajwa baadhi ya taasisi za umma ambazo zimekuwa zikiombwa au kushinikizwa kutoa rushwa.
Taasisi zilizotajwa ni Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).
Ofisa mmoja wa juu wa Bunge (jina tunalifadhi) amelieleza gazeti hili kwamba uchunguzi umebaini kuwa, Mlata akiwa na mmoja wa wajumbe wa kamati yake anatuhumiwa kupokea kiasi cha Sh milioni nane kutoka Ewura.
Huku akilionyesha gazeti hili ripoti hiyo, alisema uchunguzi umeonyesha kuwa Kamati ya Huduma ya Maendeleo ya Jamii ilimtuma katibu wake ambaye ni mtumishi wa Bunge kwenda kuchukua mzigo wa kamati hiyo katika ofisi za NHIF, lakini alipofika alikabidhiwa mfuko uliojaa fedha ambazo alikataa kuzipokea.
Alisema, ofisa huyo alirudi na kuitaarifa kamati hiyo ameshindwa kuchukua mzigo huo kwa sababu ni fedha jambo ambalo haruhusiwi kwa mujibu wa tararibu za kazi zake.
Ofisa huyo alisema, baada ya taarifa hiyo katibu huyo alishambuliwa na baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo kwa kuwaangusha, huku wakimuapiza asiseme jambo hilo na kwamba watazifuata wenyewe.
“Hawa jamaa sasa wanaomba rushwa wazi wazi na kwa nguvu, wanatumia kamati hizo kuwabana na kuwatisha watendaji ili wawape chochote, ripoti hii inamtaja Mlata kuwa alipokea shilingi milioni nane akiwa na mbunge mwenzake na kamati ya Chegeni nayo ilimtuma katibu wake ambaye ni ofisa kwenda kuchukua mzigo, lakini alipofika huko akakuta ni furushi la hela.
“Yule kijana alikataa kuzichukua kwa sababu maadili yake ya kazi yanamzuia, akarudi akawaambia ameshindwa kuchukua mzigo wenyewe kwa sababu ni furushi la hela, wakamfokea huku wakimwapiza asitoe siri hiyo na kwamba watazifuata wenyewe, yeye alipotoka hapo akaenda kuripoti kwa mabosi wake,” alisema ofisa huyo wa Bunge.
Spika Ndugai alipotafutwa kuthibitisha taarifa hizo hakuweza kupatikana. Hata hivyo, Katibu wake, Said Yakub aliliambia gazeti hili kwamba bosi wake anao utaratibu wa kuacha milango wazi kwa wabunge kukutana naye mara kwa mara kwa ajili ya kujadiliana mambo ya kibunge na yale yanayohusu utawala.
Alisema ni kweli kulikuwa na kikao hicho baina ya Spika na wabunge hao lakini hawezi kuzungumza kilichojadiliwa isipokuwa Spika mwenyewe ambaye ana mamlaka ya mwisho kuhusu uendeshaji wa shughuli za Bunge.
“Swali lako bwana mimi siwezi kulizungumzia sana, unajua Spika ana utaratibu wa kuacha milango kwa wabunge wake ambao hukutana naye mara kwa mara kwa ajili ya kujadiliana mambo ya kibunge yakiwemo ya kiutawala.
“Sasa ni kweli wabunge hao unaowataja ambao ni viongozi wa kamati walikutana na kufanya kikao na Spika lakini mimi siwezi kukuambia kilichoongelewa humo ndani isipokuwa yeye mwenyewe kwa sababu ndiye mwenye mamlaka ya mwisho ya kuhusu uongozaji wa Bunge,” alisema Yakub.
Alipoulizwa Dk. Mwanjelwa kuhusu jina lake kutajwa kwenye tuhuma hizo alisema ni tuhuma ambazo hazina ukweli na kwamba nafsi yake ni safi kwa sababu hajapewa fedha na mtu wala taasisi yoyote.
Dk. Mwanjelwa alikiri yeye pamoja na baadhi ya wenyeviti wa kamati kuitwa ofisini kwa Spika ambao aliwaeleza kuwepo kwa maneno mitaani kuhusu baadhi ya wabunge wanavyotumia majina ya wevyeviti kuomba rushwa na kuwataka kuwasimamia vizuri pamoja na kuwafikishia ujumbe wa kubadilika.
“Ni kweli Spika alituita, mimi na wevyeviti wenzangu wa kamati sita ambazo huwa zinakumbwa na majaribu sana. Alitutaka kuwa makini kwa sababu ya unyeti wa kamati zetu lakini hakutuhumu kamati yoyote wala mwenyekiti wa kamati yoyote kupokea wala kuomba rushwa,” alisema Dk. Mwanjelwa.
Kwa upande Mbunge wa Mwibara, Kangi alipoulizwa kuhusu hilo, kwanza alieleza kushtushwa kwake na kuona habari inayohusu Bunge kutikiswa na rushwa kisha akakanusha Spika kuzungumzia jambo lolote kuhusu rushwa kwa wabunge.
“Mimi kwanza leo (jana) asubuhi nimeshtushwa sana na taarifa niliyoona kwenye gazeti lenu ikihusu Bunge la rushwa, kikao kweli Spika alituita lakini ni utaratibu wake wa kawaida kukutana na wabunge wake ila kwenye kikao hicho Spika hakuzungumza lolote kuhusu rushwa hata kama inatajwa mtaani hakuna ni uongo, kungekuwa na jambo kama hilo mimi ningekuambia,” alisema Lugola.
Naye Mwenyekiti wa Kamati wa Nishati na Madini, Martha Mlata, alipoulizwa alisema ni kweli Spika aliwaita baadhi ya wevyeviti wa Kamati za Bunge ambazo alizungumza nao mambo mengi ikiwamo suala la kuwataka na hata kuwaonya wajumbe wa kamati zao kuwa makini na kazi zao na kujiepusha na vitendo vya rushwa.
Alipoulizwa kuhusu tuhuma anazoelekezwa za kupokea Sh milioni nane akiwa na mbunge mwenzake alikanusha kwa kueleza kuwa tuhuma hizo ni za uongo zenye lengo la kumchafua.
Mbali na hao, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Dk. Raphael Chegeni naye alikanusha yeye mwenyewe na wajumbe wa kamati yake kujihusisha na rushwa na kueleza kuwa jambo hilo lina nia ya kupunguza makali yao ya kuwasulubu watendaji wa Serikali wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha.
“Hatujaitwa kwa Spika, hatujachukua rushwa kwa mtu yoyote. Hili lina lengo la kutupungumzia makali kwa sababu kamati yangu ina watu makini na imekuwa ikiwindwa sana, unajua sisi tunawasulubu kweli kweli watendaji wa Serikali ambao wanashindwa kutimiza wajibu wao sawasawa, sasa kama wameamua kutuchafua hilo litakuwa jambo jingine,” alisema Chegeni.
Alipoulizwa kuhusu kamati yake kutajwa kumtuma Katibu wake kufuata mzigo NHIF, Chegeni alisema jambo hilo halina ukweli wowote.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji (PIC), Richard Ndassa ametakiwa kufika leo makao makuu ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), baada ya kuitwa kwa ajili ya mahojiano.