25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli: CCM tukubali matokeo umeya D’ salaam.

MagufuliManeno Selanyika na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

RAIS Dk. John Magufuli amebariki kufanyika kwa uchaguzi wa nafasi ya umeya katika Jiji la Dar es salaam inayogombewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Taarifa iliyotolewa na Ikulu jana iliziasa pande zote zinazovutana kuwa  tayari kupokea matokeo yoyote.

Taarifa hiyo iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa ilimkariri rais akisema.

“Upande wowote uwe tayari kupokea matokeo ya uchaguzi huo ili meya apatikane na jiji liweze kuendelea na mipango yake ya kuwahudumia wananchi bila vikwazo.

“Mahali tunapostahili kushinda kama tumeshinda tushinde kweli, lakini mahali tunaposhindwa kama tumeshindwa kweli napo tukubali kushindwa na hiyo ndio demokrasia ya kweli” ilieleza taarifa hiyo.

Kauli hiyo ya Rais Magufuli inahitimisha malumbano ya muda mrefu ambayo yalisababisha uchaguzi huo kuahirishwa zaidi ya mara tatu katika kile kilichodaiwa awali kwamba CCM wanafanya mbinu kuzuia Ukawa kushinda kiti hicho.

Awali, uchaguzi huo ulikuwa ukiahirishwa kutokana na mvutano kuhusu wajumbe halali wenye sifa za kushiriki upigaji kura, huku CCM ikitaka wabunge wa viti maalumu kutoka Zanzibar washiriki uchaguzi huo.

CCM wakwaa kisiki mahakamani

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana ilibariki uchaguzi wa meya na naibu meya wa Jiji la Dar es Salaam kufanyika kama ulivyopangwa leo baada ya kukataa maombi ya kuuzuia yaliyowasilishwa na wana CCM .

Uamuzi huo ulitolewa jana mahakamani hapo na Hakimu Mkazi Mkuu, Warialwande Lema, baada ya kusikiliza maombi yaliyokuwa yamewasilishwa na walalamikaji, Suzan Massawe na Kumjhi Mohammed kupitia Wakili wao, Elias Nawela dhidi ya Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam.

Hakimu Lema alisema hakuna sababu za msingi zilizotolewa na waleta maombi ya kulazimisha uchaguzi wa meya na naibu meya wa Jiji la Dar es Salaam usifanyike kesho (leo).

“Hakuna uthibitisho wowote kuonyesha kama hao waleta maombi si miongoni mwa wapiga kura, hivyo si busara kuendelea na sababu ambazo hazijathibitishwa,” alisema Hakimu Lema.

Akiendelea kusoma uamuzi huo, alisema kukosekana kwa orodha inayoonyesha majina ya wapiga kura kunasababisha haijulikani waleta maombi ni miongoni mwa wapiga kura au laa.

Alisema mahakama inataka lazima waonyeshe uthibitisho kitu ambao waleta maombi hawajakionyesha, hivyo hali hiyo inafanya hata mahakama kutofikiria kama kuna hasara watakayoipata kwa miaka mitano ijayo.

Akielezea historia ya shauri hilo, Hakimu Warialwande alisema waombaji hawakuwa makini tangu awali walipofungua kesi hiyo Februari 5, mwaka huu, ambapo hawakutokea mahakamani hadi Februari 14, mwaka huu, ndipo Wakili Nawela alipojitokeza na kuomba nakala ili awapelekee wajibu maombi.

Hakimu huyo alisema kutoonekana kwa waleta maombi hayo, kunaonyesha kwamba hawakuwa makini na hali hiyo inafanya washindwe kuishawishi mahakama iwape haki yoyote kwa kuwa hawakufuatilia shauri lao tangu awali.

Kutokana na mazingira hayo yote, mahakama inaona hakuna sababu zozote za msingi zilizowasilishwa na waleta maombi hayo kuzuia uchaguzi huo.

Awali, Wakili Nawela aliiomba mahakama  itoe zuio la kufanyika uchaguzi huo na kuamuru hali ibaki kama ilivyo, kwa madai ya kwamba waleta maombi hawajapewa haki yao ya kualikwa kushiriki katika uchaguzi huo.

Aliomba hali ibaki kama ilivyo hadi hapo kesi ya msingi itakaposikilizwa kwa kuwa iwapo uchaguzi utafanyika leo kesi yao ya msingi na maombi yao yatakuwa hayana maana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles