MOSCOW, Urusi
MIAKA miwili iliyopita, timu ya Taifa ya Ufaransa ikiwa katika ardhi ya nyumbani, ilishindwa kutwaa taji lake la kwanza la michuano mikubwa.
Hizo zilikuwa ni fainali za Euro 2016, mashindano ambayo Ureno iliibuka kidedea, ikiitandika Ufaransa katika mchezo wa mwisho.
Ukiacha hilo, mashabiki wa soka nchini Ufaransa hawajashangilia utamu wa kulinyakua taji la Kombe la Dunia tangu walipofanya hivyo mwaka 1998.
Baada ya fainali hizo zilizofanyika nchini humo, wakishinda mabao 3-0 katika mtanange wa fainali dhidi ya Brazil, Ufaransa wamekuwa wasindikizaji licha ya mara nyingi kuwa na kikosi chenye mastaa.
Kama ilivyo kawaida yao, watakwenda Urusi kucheza michuano ya mwaka huu wakiwa na mastaa wengi kikosini.
Mapengo ya wakongwe Patrice Evra, Bacary Sagna, Andre-Pierre Gignac na Yohann Cabaye waliokuwa sehemu ya timu hiyo katika fainali za Euro za mwaka juzi, yamezibwa na nyota wanaotamba barani Ulaya.
Kwa kuanza na langoni, Wafaransa wanajivunia kipa tegemeo katika kikosi cha Tottenham, Hugo Lloris, ambaye hajaruhusu bao mara 73 katika mechi 203 alizoidakia timu hiyo ya Kaskazini mwa London.
Safu yake ya ulinzi itakuwa salama zaidi kwa kuwa Didier Deschamps ana Presnel Kimpembe ambaye amekuwa akiziba nafasi ya mkongwe Thiago Silva pale PSG, Raphael Varane (Real Madrid), Laurent Koscielny (Arsenal) na Samuel Umtiti (Barcelona).
Varane amekuwa na kiwango kizuri msimu huu, akicheza sambamba na mkongwe Sergio Ramos katika eneo la beki wa kati Real Madrid, ambapo asilimia 90 ya pasi zake msimu huu zimewafikia walengwa.
Pia, Deschamps anaweza kumuita beki wa Marseilla, Adil Rami, ambaye amekuwa msaada mkubwa kwa timu yake katika michuano ya Ligi ya Europa ambayo wameshatinga fainali, akiwa amefunga bao moja.
Wakati kocha huyo akiwa na uamuzi wa wawili atakaowatumia eneo la kati, mabeki wa pembeni wanaoweza kumsaidia ni Layvin Kurzawa wa PSG na Djibril Sidibe anayecheza Monaco.
Faida ya Kurzawa ni kwamba licha ya kwamba ni beki wa kulia, pia amekuwa mfungaji mzuri na hata PSG ilipoishia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, alikuwa amefunga mabao matatu.
Wafaransa watakwenda Urusi wakiwa wanajivunia ubora wa eneo lao la kiungo ambalo litakuwa na N’Golo Kante atakayecheza chini (kiungo wa ulinzi), nafasi ambayo pia Steven N’Zonzi anaicheza vizuri akiwa na kikosi cha Sevilla.
Juu ya mmoja kati yao, kutakuwa na Paul Pogba, licha ya kwamba kocha Deschamps atakuwa na Blaise Matuidi (Juventus), Corentin Tolisso (Bayern Munich), Adrien Rabiot (PSG) na Nabil Fekir (Lyon) na Dimitri Payet (Marseille).
Ufaransa inajivunia pia utitiri wa vipaji vya wachezaji wa pembeni (winga), kwani hapo kutakuwa na Kylian Mbappe, Ousmane Dembele, Anthony Martial, Thomas Lemar na Florian Thauvin na Kingsley Coman anayetarajiwa kurejea kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia.
Ni kama ilivyo kwa washambuliaji, ambako nako itakuwa ni juu ya Deschamps kuchangua atakayeingia ‘first eleven’ na atakayesubiri benchi.
Antoine Griezmann ameshaifungia Atletico Madrid mabao 19 na kutoa pasi za mabao ‘asisti’ nane msimu huu (kabla ya mechi za juzi). Ni wazi atampiku Oliver Giroud ambaye tangu ahamie Chelsea akitokea Arsenal, amekuwa akitokea benchi katika mechi nyingi.
Zaidi ya hao wawili, Wissam Ben Yedder anayeibeba safu ya ushambuliaji ya Sevilla na Alexandre Lacazette ambaye ameziona nyavu mara 13 pekee msimu huu, watakuwepo kusikilizia.
Mbali ya uzuri wa wachezaji wake, wachambuzi wa soka barani Ulaya wanaitazama Ufaransa kwa jicho la matumaini kuelekea fainali hizo, wakiamini kwa kiasi kikubwa hakiundwi na ‘wazee’. Wastani wa umri wa mastaa wa timu hiyo ni miaka 25.
Kwa upande mwingine, wamekuwa na mafanikio makubwa katika klabu zao kwani Kante, Pogba, Matuidi na Umtiti, wana rekodi ya kushinda mataji ya Ligi Kuu wakiwa na klabu mbalimbali.
Varane si tu taji la La Liga akiwa na Madrid, ameweza kubeba mara tatu lile la Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na wakali hao wa Santiago Bernabeu.