26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Uchambuzi wa taarifa ya mafuta Zanzibar kukamilika Septemba

KHAMIS SHARIF-ZANZIBAR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amesema kazi ya uchambuzi wa taarifa za utafiti wa mafuta na gesi uliofanywa na Kampuni ya RAK GAS ya Ras Al Khaimah, inatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu.

Alisema katika mchakato huo, wataalamu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, wanashiriki ili kupata taarifa sahihi za rasilimali hiyo.

Akitoa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa mwaka wa fedha 2019/2020 katika kikao cha bajeti kinachoendelea katika ukumbi wa baraza la wawakilishi mjini Unguja, alisema Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019, imeandaa rasimu tatu za kanuni ambazo ni kanuni ya uchimbaji, ya ada na vibali na kanuni ya uwasilishaji wa taarifa za kila siku.

Alisema Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mafuta na Gesi (ZPRA), imejiandaa kufanya mazungumzo na kampuni nyingine zitakazohitaji kuwekeza katika sekta ya utafutaji wa mafuta na gesi baada ya kukamilika kwa hatua ya kuvigawa vitalu vingine vilivyopo Zanzibar.

Kuhusu Pato la Taifa, alisema kwa mwaka 2019 linatarajiwa kukua kwa kasi ya wastani wa asilimia 7.8 itakayosababisha kuimarika zaidi kwa uchumi kutokana na ongezeko la uwekezaji katika sekta ndogo ya usafirishaji na uvuvi.

Alisema hali hiyo imesababisha kuongezeka kwa pato la mwananchi kutoka shilingi milioni 2.1 sawa na Dola za Marekani 944 na kufikia shilingi milioni 2.3 sawa na dola 1,026.

“Zanzibar tayari imekaribia kufikia kiwango cha nchi ya kipato cha kati cha Dola za Marekani 1,030 kwa mujibu wa vigezo vya kimataifa,” alisema.

Alieleza kuwa pato la taifa kwa bei ya soko limefikia thamani ya shilingi bilioni 3.663 kwa mwaka wa fedha 2018 kutoka thamani ya shilingi bilioni 3.228  kwa mwaka 2017 kulikosababishwa na ongezeko la pato la mwananchi.

Alisema kasi ya mfumuko wa bei pia imeshuka hadi kufikia wastani wa asilimia 3.9 mwaka 2018 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 5.6 mwaka 2017 baada ya kuchukuliwa hatua za kuudhibiti.

Akizungumzia mwelekeo wa hali ya uchumi wa Zanzibar kwa mwaka 2019, alisema unategemewa kwenda sambamba na utekelezaji wa dira ya maendeleo ya 2020, mkakati wa kukuza uchumi Zanzibar (MKUZA III) na ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015/2020.

Alisema azma ya Serikali ni kuhakikisha inakamilisha miradi yote mikubwa ya maendeleo kama ilivyoahidi katika ilani ya uchaguzi ya chama ya mwaka 2015/2020.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles