23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Zitto, mawaziri Watoana jasho ukuaji wa uchumi

ARODIA PETER-DODOMA

BAADHI ya wabunge wa upinzani na mawaziri wamechuana kwa kuonyeshana umahiri wa nani anajua nini katika miradi ya ujenzi na uhalisia wa kiwango cha ukuaji wa uchumi hapa nchini.

Mchuano huo ulitokea bungeni jana, katika mjadala wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, baada ya Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe Zitto, kutoana jasho na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango pamoja na Naibu wake, Dk. Ashatu Kijaji, ambao kwa nyakati tofauti walisimama bungeni kutoa taarifa kuhusiana na hoja kuhusu ukuaji wa uchumi pamoja na taarifa ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwa Tanzania.

Katika hoja yake, Zitto alisema katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Wizara ya Ujenzi imechukua asilimia 46 ya bajeti yote ya maendeleo, lakini haijatoa matokeo ya kuridhisha katika ukuaji wa uchumi.

“Jumla ya fedha ambazo tumeziingiza kwenye wizara hii ni shilingi trilioni 18.7, sawa na jumla ya fedha za bajeti ya maendeleo ya nchi ambayo ni shilingi trilioni 40.6,” alisema Zitto na kuongeza:

“Kwa hiyo asilimia 46 ya bajeti ya maendeleo unaishika wewe Waziri wa Ujenzi, Kamwelwe na manaibu wako wawili.

“Wabunge wana haki ya kuuliza, kiasi hiki cha fedha ambacho tunakiingiza kwenye wizara hiyo hadi sasa kimezalisha viwanda vingapi, kwa sababu tunazungumza kuhusu namna ambavyo fedha tunaziingiza katika miradi kama reli, ndege zinachocheaje sekta nyingine za uchumi.

“Tungepata maelezo ya Serikali hapa, kwamba tumeingiza shilingi trilioni 18.7 na matokeo yake ni nini, Dk. Mpango analijua hili kwamba moja ya sekta zinazopaswa kuonyesha zilivyochangia uchumi ni ujenzi.

“Kwanini sisi ambao tunaingiza fedha nyingi kiasi hiki, na bado kasi ya ukuaji wa uchumi iwe ni ndogo, leo hii tunabishania makisio ambayo IMF wameyatoa ya asilimia nne nakadhalika, IMF na Waziri Mpango hawajakanusha makisio haya, wamekanusha ile ripoti, lakini makisio bado ni yale yale, hata ukichukua makisio ya Serikali ya asilimia sita lakini kabla Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani uchumi wetu ulikuwa unakua kwa asilimia saba kwa miaka kumi na tangu Serikali ya Awamu ya Tano imeingia madarakani, shilingi trilioni 18 zimeingizwa katika  ujenzi, lakini ukuaji wake uko chini.”

Alitolea mfano nchi ya Kenya kwamba wamejenga reli ya SGR kwa mkopo mkubwa, lakini sekta yao ya ujenzi imekua kwa asimilia 1.5.

“Hata mkiacha ile asilimia nne ya IMF twendeni na ile ya Serikali ya asilimia sita bado tuko chini, kwa sababu mipango yetu ya maendeleo ya miundombinu ni kutoa fedha kwenda nje na hatuingizi ndani na ndiyo maana mzunguko wa fedha ni mdogo, mmewapa kazi wakandarasi wa nje wanaagiza malighafi zote kutoka nje.

“Mnakusanya kodi kwa muuza nyanya kumlipa Mturuki, naye anapeleka Uturuki, ndiyo maana uchumi haukui, hata mjenge utetezi wa namna gani, nimeona ile ya Serikali kwenda IMF, kusema tuna makisio ya miradi mikubwa haya ni makosa, tuna SGR, Stigler’s Gauge, miradi yote hii haina maana, fedha zote zinaenda nje na huduma yetu ya deni la taifa ni kubwa,” alisema.

Baadaye Mpango alisimama kutoa ufafanuzi: “Nataka nimpe taarifa Zitto, hapa nimeshika ripoti rasmi ya pato la taifa na ukuaji wake wa mwaka 2018 ambayo iko bayana, gross late ya 2013 ilikuwa asilimia 6.8, 2014 ilikuwa asilimia 6.7, 2015 asilimia 6.2, 2016 asilimia 6.9, 2017 asilimia 6.8 na 2018 ilikuwa silimia 6.9, sasa hiyo gross late iliyoteremka ni ipi,” alihoji na kuongeza:

“Kwanini mnatumia taarifa za IMF ambazo hazina ukweli, na niliwaambia katika Bunge hili kwamba bado tunazungumza na AfDB wana project uchumi wa Tanzania mwaka huu 2019 utakua asilimia 6.8, makadirio ya Benki ya Dunia (WB) ni asilimia 6.6, sasa hiyo growth late iliyoteremka ni ipi?

Baada ya taarifa hiyo, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, alimuuliza Zitto kama anaipokea taarifa hiyo.

“Naipokea taarifa ya Mpango lakini ninachotaka kumwambia, kwanza anajua kwamba mamlaka ya Economic Surveillance ya dunia ni moja nayo ni IMF na anafahamu kwa sababu amefanya kazi huko, WB, AfDB na hata Wizara ya Fedha makisio wanayoyatumia ni ya IMF, si makisio mengine na anafahamu labda atakataa kwa sababu anaitetea Serikali hapa,” alisema Zitto.

Pia mjadala huo ulimwibua Dk. Kijaji, aliyetoa ufafanuzi kuwa kupeleka fedha katika sekta ya ujenzi kuwa athari yake ni ya muda mfupi.

Alipotakiwa kuendelea na hoja yake, Zitto aliendelea kusisitiza kuwa: “Kuna tofauti kubwa kati ya kasi ya ukuaji wa uchumi na uchumi. Sekta ya ujenzi ni ya pili katika kasi ya ukuaji, si ya pili katika uchangiaji kwenye sekta. Lakini pointi yangu hapa wastani wetu tuliokuwa nao ni asilimia saba.

“Mpango anajua panapokuwa na mdororo wowote wa uchumi Serikali inaingiza fedha katika mzunguko, na kwa miaka mitatu iliyopita tumeingiza shilingi 18.7 trilioni kwenye ujenzi, naomba nijibiwe, hii fedha ambayo tumeipampu imezalisha viwanda vingapi, ajira za kudumu ngapi, sekta ya kilimo imechochewa vipi,” alihoji.

Naye Naibu Waziri Kivuli wa Fedha, David Silinde (Chadema), alisema mradi SGR wenye thamani ya Dola bilioni saba za Marekani haujaleta mabadiliko yoyote katika ukuaji wa uchumi.

Alishauri Serikali kufanya uamuzi upya wa kuwekeza katika miradi ya kuzalisha chuma ya Mchuchuma na Liganga ili malighafi zinazotumika katika ujenzi huo wa reli ziweze kuzalishwa ndani ya nchi.

“Sisi hatuna shida na reli kujengwa, isipokuwa ni namna mambo yanavyofanyika, chuma zote zinazotumika zinatoka China na kidogo ndiyo wanapewa wa ndani tena wanapewa tenda za kudanganyia, tani 1,000 au 2,000 basi.

“Haya ni makosa tumekwishafanya na kama hatujawaza mapema mradi wa awamu ya pili kutoka Makutupora kwenda Mwanza watu wetu wataambulia patupu.

“Kikubwa ninachoshauri makosa yaliyofanyika yasiendelee kufanyika, Dola bilioni tatu za Marekani zikiwekezwa Mchuchuma, manufaa yake ni makubwa, umeme, madini na chuma kitakachotumika hata katika hiyo reli,” alisema Silinde.

Baada ya mjadala huo, Dk. Tulia, alitoa ufafanuzi kwa Mbunge wa Mbeya Vijijini,  Oran Njeza (CCM), aliyeitaka Serikali kulipa deni la Sh bilioni 433.9 inalodaiwa na wafanyakazi wa Reli ya Tazara na kuutafakari upya mkataba wa uendeshaji wa reli hiyo kati yake na Zambia, akieleza kuwa nchi jirani hiyo haiwekezi vya kutosha katika reli hiyo.

Mbunge huyo pia aliishauri Serikali kujenga bandari kavu mkoani Mbeya ili kuipa thamani Reli ya Tazara.

Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF), aliitaka serikali kutekeleza miradi ya ujenzi wa barabara zinazoziunganisha wilaya za Tabora na barabara kuu zinazouunganisha mkoa huo na mikoa mingine ili kurahisisha usafirishaji wa mazao, hasa tumbaku inayolimwa kwa wingi mkoani humo.

Alisema wakandarasi wa ndani waliopewa zabani za kutekeleza miradi hiyo wameonyesha udhaifu, hivyo kuna haja Serikali kuachana nao na kutoa kazi kwa wakandarasi kutoka nje.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles