London
BORIS Johnson ameahidi kumaliza kizungumkuti cha Brexit iwapo atachaguliwa tena baadae wiki hii. Lakini ikiwa siyo Johnson, basi ni Jeremy Corbyn ambaye amefanikiwa kuficha msimamo wake kuhusu suala la Brexit.
Boris ambaye ni Meya wa zamani wa London, amepunguza utani na mizaha yake iliyozoeleka wakati akijitayarisha kwa uchaguzi Alhamisi ijayo chini ya ahadi ya kukamilisha mchakato wa Brexit haraka iwezekanavyo.
Kura za maoni ya umma zinaashria juhudi zake za kujipigia upatu kuwa kiongozi imara na mwenye mitizamo ya kutia moyo zinafanya kazi na chama chake cha Conservative kinaweza kupata wingi wa viti bungeni.
Lakini Johnson bado amesalia kuwa kiongozi anayegawa maoni, kutokanana nafasi yake wakati wa kampeni ya kura ya maoni ya Brexit mwaka 2016 ambayo ilitawaliwa na madai yaliyotiwa chumvi kuhusu Umoja wa Ulaya na kadhia ya uhamiaji.
Matamshi yake ya kuudhi ikiwemo dhidi ya mashoga na kuwafananisha wanawake wa kiislam wanaovaa hijab kuwa sawa na masanduku ya barua, yameongezeka wakati wa kampeni.
Kimsingi wapiga kura wengi wanaamini Boris ni mwanasiasa bora kuliko kiongozi wa mrengo wa kushoto Jeremy Corbyn ambaye maoni ya umma yanamtaja kuwa kiongozi wa upinzani asiye mashuhuri katika kipindi cha miaka 45 iliyopita.
Tabia ya Boris ya kukosa umakini na kupungukiwa uzingatiaji wa mambo umesababisha ashutumiwe kwa kukosa uwezo wa kuwa kiongozi thabiti.
Akiwa Wazri Mkuu, Johnson amewaziba midomo wapinzani wake kwa kufanikiwa kuufanyia mabadiliko mkataba wa Brexit wa mtangulizi wake Theresa May.
”Wale ambao hawakumchukulia kuwa mtu makini walifanya makosa” alisema Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron pindi Johnson alipoufanikisha mkataba wa Brexit.
Juhudi zake zilikatishwa na uamuzi wa bunge wa kupitisha sheria ya kumzuia kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya bila mkataba na kusababisha kurefushwa kwa muda wa mchakato huo hadi Januari mwaka unaokuja.
Hivi sasa anatumai ikiwa atashinda wingi wa viti bungeni, anaweza kufanikiwa kupitisha makubaliano yake na Umoja wa Ulaya kabla ya muda wa mwisho wa Januri 31 kufikiwa.
Harakati za kisiasa za Johnson zimekuwa na kishindo wakati wote na hivi sasa amewekeza nguvu zote katika uchaguzi wa Desemba 12.
Ushindi wake utaacha alama muhimu miongoni mwa viongozi wenye ushawishi nchini Uingereza, ikiwemo shujaa wake Waziri Mkuu wa zama ni Winston Churchill.