Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati wakati akithibitisha kwamba kulikuwa na jaribio la kudukua mitambo ya tume hiyo, ambalo hata hivyo, halikufanikiwa, ametangaza uwezekano mkubwa wa kutangaza matokeo leo mchana.
“Tunazitaka pande zote kubakia watulivu hasa katika kipindi hiki muhimu,” alisema Chebukati.
“Tunafanya kila linalowezeklana kupata matokeo yote ndani ya kipindi kifupi kadiri iwezekanavyo. Tunategemea matokeo yote ya urais kupitia fomu halisi yatakifikia kituo cha taifa cha kujumuisha matokeo ifikapo saa 6 mchana kesho (leo).”
Alisema matokeo yatapitiwa na uamuzi wa mwisho kutangazwa baada ya muda kidogo.
Aidha kamishina mwingine wa IEBC, Yakub Guliye, ambaye anaongoza kamati ya makamishina wa Teknohama, aliwaambia wanahabari kuwa mfumo uko imara na hakuna aliyeweza kuingia baada ya majaribio kadhaa.
“Tumeona majaribio kadhaa ya watu fulani kudukua katika mfumo wetu, lakini hawakufanikiwa kwa sababu tumewekeza mno katika ulinzi,” alisema Profesa Guliye.
“Kuna majaribio lakini hakuna ushahidi wa kufanikiwa kuuingia. Tuhuma za kudukuliwa si katika mfumo wetu. Madai ya mfumo wetu ulidukuliwa si ya kweli.”
Ufafanuzi wa Profesa Guliye unapingana na ule wa Mtendaji Mkuu wa Tume, Ezra Chiloba alioutoa awali kuwa mfumo wao uko salama na hakukuwa na jaribio lolote la kuudukua.
JUBILEE YAONGOZA UGAVANA, SENETA, BUNGE
Chama tawala cha Jubilee kinatarajia kudhibiti Baraza la Seneta na Bunge kwa mara nyingine baada ya kutwaa viti vingi katika nyadhifa hizo na ugavana.
Chama hicho kilipata magavana 24 huku chama cha Rila, ODM kikipata magavana 13 na WDP cha mgombea mwenza wa Raila, Kalonzo Musyoka kikipata magavana wawili.
Kwa upande wa useneta, Jubilee ilitwaa viti 24, ODM 13 na WDP vitatu. Nafasi za ubunge Jubilee ilitwaa viti 113, ODM 41 huku wagombea binafsi wakipata viti 17.