23.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, March 22, 2023

Contact us: [email protected]

KAMATI YA KUCHUNGUZA VIGOGO 12 MBEYA YAANZA KAZI

KAMATI ya uchunguzi wa vigogo 12 akiwamo aliyekuwa Meya wa Jiji la Mbeya, Atanas Kapunga, kwa tuhuma za kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 63.448 kupitia mradi wa ujenzi wa Soko la Mwanjelwa, imeanza kazi.

Kamati hiyo ya uchunguzi, iliundwa na Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa Julai 31, mwaka huu alipokuwa jijini Mbeya, baada ya kupokea taarifa Maalumu ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali (CAG), iliyobainisha namna baadhi ya watendaji na viongozi wa halmashauri ya Jiji la Mbeya walivyoisababishia hasara serikali kupitia mradi huo.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla amesema timu hiyo imewasili na kuanza kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa agizo na maelezo yaliyotolewa na Waziri Mkuu, wakati wa ziara yake ya kikazi   aliyoifanya Mkoani hapa mwishoni mwa mwezi Julai.

“Kamati imewasili na tayari imeanza kuifanya kazi yake ambapo kazi kubwa itakayofanywa na kamati hiyo ni kuchunguza na kuwahoji watuhumiwa na kisha kufungua mashitaka dhidi yao,” amesema Makalla.

Pamoja na mambo mengine, kamati hiyo hiyo itafanya kazi yake sehemu mbalimbali Mbeya Mjini ndani ya siku sita na kisha kuelekea Wilayani Rungwe kwa ajili ya kuchunguza malalamiko ya wakulima wa chai yaliyotolewa kwa Waziri Mkuu ambapo wakulima hao kwa sasa wametishia kutolima zao la chai kwa madai ya kutonufaika nalo kutokana ukiritimba wa manunuzi unaofanywa na bodi ya chai hivyo kulazimika kuuza zao hilo kwa mnunuzi mmoja na kwa bei isiyo na tija.

Mbali na Kapunga, wengine watakaohojiwa na kamati hiyo ni waliowahi kuwa wakurugenzi wa Jiji la Mbeya kwa nyakati tofauti, Mussa Zungiza, Elizabeth Munuo, Juma Idd na Dk. Samwel Lazaro aliyekuwa akikaimu nafasi ya ukurugenzi.

Wengine ni aliyekuwa Mweka Hazina wa Jiji hilo, James Jorojik   na waliokuwa wajumbe wa bodi ya zabuni ambao ni Mussa Mapunda, Samweli Bubengwa, Davis Mbembela, Lydia Herbert na Bernard Nsolo ambao walipitisha nyongeza ya mradi huo bila kuzingatia maslahi ya jiji na mwingine ni Emily Maganga ambaye inasemekana hakuishauri vizuri bodi hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,020FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles