33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

UCHAGUZI KENYA: MWANAFUNZI ASHINDA UBUNGE, MAMA AMSHINDA MWANAE

Mwanafunzi mwenye umri wa miaka 23, ambaye aligombea ubunge kama mgombea binafsi, anatarajia kuwakilisha Jimbo la Igembe South baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi huo jana asubuhi.

Igembe South ni moja ya majimbo ya Kaunti ya Meru, katika eneo la Mlima Kenya.

Mwanafunzi huyo, John Paul Mwirigi wa shahada ya kwanza ya elimu katika Chuo Kikuu cha Mlima Kenya, alishinda kwa kupata kura 18,867 dhidi ya mgombea wa chama tawala cha Jubilee, Rufus Miriti aliyepata kura 15,411.

Mwirigi pia aliwashinda wanasiasa wa siku nyingi wakiwamo Mwenda Mzalendo aliyepata kura 7,695, Kubai Mutuma (6,331) na Raphael Muriungi (2,278).

Mwirigi, ambaye anatarajia kuwa mbunge mdogo zaidi wa kuchaguliwa, hakuendesha kampeni yoyote ya maana.

Alisema kuwa aliendesha kampeni kwa mguu kwa kutembelea nyumba kabla ya kupata msaada wa waendesha bodaboda.

Wafuasi wake walianza kusherehekea ushindi juzi wakati matokeo ya awali yalipomuonyesha yuko mbele ya washindani wenzake.

Mwirigi alisema mara ya kwanza alivutiwa na siasa wakati akiwa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Kirindine.

“Nilikuwa na ndoto na ni hapo nikanza kuwaomba wanafunzi wenzangu kunikampenia kwa vile ningehitaji kura zao mwaka 2017.

“Nimeshikilia nyadhifa za uongozi shuleni na mahali ninakoishi,” alisema Mwirigi.

Mwirigi alisema ajenda yake ya kwanza itakuwa kusaidia shughuli za kilimo cha biashara kuhamasisha ujasiriamali na kukuza vipaji.

“Kwa vile natokea mazingira masikini, nafahamu masuala yanayowakabili wakazi. Ajenda yangu kuu itakuwa kubadili maisha ya watu,” alisema.

Akiwa mzaliwa wa sita katika familia ya watoto wanane, bado anaishi katika nyumba ya wazazi na hamiliki ardhi tofauti na madai yaliyoenea kuwa aliuza kipande chake cha ardhi ili apate fedha za kampeni.

Wakazi wa eneo hilo wanasema waliamua kumchagua kijana huyo licha ya kukosa rasilimali kwa sababu wana imani anajua matatizo yao na atayashughulikia.

 

MAMA AMSHINDA MWANAE

Katika eneo la Bomet Mashariki, katika kaunti ya Bomet kusini mwa uliokuwa Mkoa wa Bonde la Ufa, Mbunge wa zamani Beatrice Kones, ambaye ni mjane wa waziri wa zamani, Kipkalya Kones, aliyewania kupitia chama cha Jubilee alikabiliana na wagombea wengine wanane akiwamo mtoto wake wa kiume, Kipngetich Kones.

Kones aliwania kupitia chama kinachoegemea upande wa upinzani – Chama cha Mashinani (CCM).

Kulikuwa na ushindani mkali ulioiacha familia ikiwa imegawanyika, ambapo Kones alishinda kiti hicho mara ya kwanza kwenye uchaguzi mdogo, kufuatia kifo cha mumewe mwaka 2008 na akahudumu hadi mwaka 2013.

Wakati wa kampeni mtoto wake alimshutumu mara kwa mara mama yake kwa kukosa mipango mipya ya kuwanufaisha watu wa Bomet Mashariki.

Lakini wapigakura waliamua kumchagua kwa kumpa kura 22,796 ambazo ni sawa na asilimia 53.57 ya kura zilizopigwa.

Wa pili alikuwa mgombea wa kujitegemea, Bernard Bett aliyekuwa na kura 12,042 huku Kones akimaliza wa nne akiwa na kura 2,410, sawa na asilimia 5.66.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles