29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

UCHAGUZI EALA: CHADEMA, CCM WAUMIZANA

Fredy Azzah,

VYAMA vya CCM na Chadema vimeumizana, kutokana na misimamo yao wakati wa kuchagua wawakilishi tisa wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

Hali hiyo imejitokeza wakati CCM ikiwa na wabunge 275 na vyama vya upinzani vikiwa na wabunge 117.

Wakati chama kimoja kikiweka msimamo wa kuwakataa baadhi ya wagombea wa wenzao, athari ya moja kwa moja hutokea kwa sababu, ni vigumu chama husika kupeleka majina ya wagombea wake na hapohapo kikaweka msimamamo wa kuwachagua baadhi na kuwakataa wengine.

Kutokana na hali hiyo, kila upande una nafasi kubwa ya kukwamisha upande mwingine kwa misimamo itakayowekwa.

Aprili nne mwaka huu, awamu ya kwanza ya uchaguzi huo ilifanyika ambapo wagombea wawili wa Chadema walianguka baada ya kupigiwa kura nyingi za hapana.

Wagombea hao walikuwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani wa zamani, Lawrence Masha na Mbunge wa zamani wa Nyamagana, Ezekia Wenje.

Hali hiyo, ilisababisha malalamiko kwa upande wa Chadema, ambapo Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alipinga matokeo hayo akisema ni uminywaji wa demokrasia.

 “Hawawezi kueleza sababu za msingi za kuwakataa wagombea wetu, kwa sababu wagombea wetu wana sifa, lakini wenzetu wana mkakati wa ki-CCM na kiserikali, wanakataa wagombea wazuri washindani wa chama chetu kwa sababu ambazo hatuzielewi…

“Tutawarejesha tena wagombea hawahawa wawakatae tena, watuambie wanatumia sheria gani kuwakataa wagombea wa upinzani.

“Wanajipaje uhalali wakutuchagulia sisi wapinzani, ni nani wawe wawakilishi wetu, huo ni ujinga hakuna demokrasia kama hii duniani, ila kwa ujinga wa CCM kama ambavyo mmeuona.

“Uchaguzi huu umekuwa wa kijinga watu hawana masilahi ya Taifa, wanaangalia mambo ya chama lakini time will tell (muda utaongea) ndiyo kwanza vita inaanza,” alisema Mbowe.

Tofauti na alivyoahidi, katika marudio ya uchaguzi huo uliofanyika juzi, Chadema ilipeleka wagombea sita, ambapo baada ya kupigwa kura, wawili wasiokuwa na majina makubwa kwenye nyanja za siasa walishinda, huku wakiwaangusha vibaya viongozi wao wa kitaifa na wanasiasa waandamizi.

Katika kura 296 zilizopigwa juzi kujaza nafasi mbili za Chadema, Josephine Lemoyan alipata kura 219 na Pamela Maassay alipata kura 200, hivyo kutangazwa washindi.

Wakati sura hizo mpya kwenye ulingo wa siasa za kitaifa zikichomoza, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho,Profesa Abdallah Safari akipata kura 35, huku Naibu  Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu, akipata kura 59.

Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha, alipata kura 44 huku Wenje ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kanda ya Ziwa, Ezekia Wenje, akiambulia kura 43.

Matokeo hayo, licha ya kupongezwa na viongozi wa Chadema, yamezua mjadala kwa wapenzi na mashabiki wa chama hicho na dawau wengine wa siasa ambao wanasema CCM yenye wabunge wengi, wamefanya makusudi kuchagua majina yasiyojulikana ili kuikomoa Chadema.

Wanasema wakati nchi nyingine zikipeleka viongozi waandamizi EALA ili wakatetee maslahi ya nchi zao, CCM yenye wabunge wengi, wameikomoa Chadema badala ya kuangalia maslahi ya nchi.

Wakati hayo yakisemwa, hali kama hiyo ilitokea kwenye uchaguzi wa Aprili nne,mwaka huu ambapo kambi ya upinzani ilidaiwa pia kukaa na kukubaliana kuchagua baadhi ya watu wa kuwapigia kura kwa upande wa CCM na wengine kuwaacha.

Katika uchaguzi huo, Chadema ilidaiwa kuweka msimamo wa kuwapigia kura Happiness Lugigo na Fancy Nkuhi na kuwaacha Happiness Mgalula na Zainabu Kawawa kwa upande wa kundi la wanawake.

Baada ya kura, Lugigo alipata kura 196, Nkuhi  197, Mgalula 125 na   Kawawa 137.

Kwa upande wa kundi la wanaume bara, walidaiwa kuweka msimamo wa kumchagua Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa na Dk. Ngaru Maghembe na kuwaacha Makongoro Nyerere na Anamringo Macha.

Kimbisa alipata kura 266, Macha 23, Makongoro 81 na Dk.Maghembe 287.

Baadhi ya sababu zilizodaiwa kufanya upinzani ichaguwe baadhi ya watu wa kuwapigia kura na wa kuacha wengine, ni athari za vugu vugu la Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Chadema yanena

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, mbali na kupongeza walioshinda, alisema CCM ndiyo yenye wabunge wengi hivyo kwa kiasi kikubwa imechangia kupitisha wajumbe wawili wa chama chao na kuwaacha wengine wane.

Alisema wagombea sita waliopelekwa bungeni, walipatikana kutokana na maelekezo ya barua ya Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah iliyotaka nafasi mbili za Chadema, kila moja iwe na wagombea wasiopungua watatu na suala la jinsia lizingatiwe.

Kutokana na hali hiyo, alisema walipewa muda mfupi ili kuwasilisha orodha ya wagombea bungeni, ambapo walichukua majina 17 ya walioomba nafasi hizo awali ambapo ndani yake kulikuwa na wanawake wawili na wakafungua dirisha kwa wengine kuomba tena nafasi hizo ndani ya chama ambapo sita walituma maombi.

“Baada ya hapo, tulipata watu 23, walioongoza ni hao sita ambao ndiyo idadi ya chini ya wagombea tuliyoambiwa na Bunge tuwapeleke,” alisema Mrema.

Alisema baadhi ya hoja zinazotolewa sasa kwamba matokeo hayo yameonyesha kwamba viongozi wakuu wa chama hicho walioshiriki kwenye uchaguzi huo hawana mashiko, hazina maana kwani waliowakataa ni CCM na si Chadema.

“Kama hawakubaliki, ni CCM ndiyo hawawakubali kwa sababu wao ndiyo wengi, siyo wabunge wa Chadema,” alisema Mrema.

Hoja nyingine kupelekwa kwa majina hayo kumetokana na makovu yaliyotokea ndani ya chama hicho baada ya Wenje na Masha kuchaguliwa kwenye kundi la awali.

Mrema alisema. “Kwamba kuna makovu siyo kweli, mara ya kwanza wagombea walikuwa 17, Kamati Kuu ikachagua hao wawili ndio walikuwa na kura nyingi na nafasi zilikuwa mbili, lakini CCM wakawakataa, sasa ni vyema muwaulize watuambie kwanini mwanzo waliwakataa Masha na Wenje.”

CCM yajibu

Mbunge wa Bukoba Vijijini, ambaye pia ni Katibu wa Wabunge wa CCM, Jason Rweikiza, alisema hoja ya wao ndio waliowakataa Masha na Wenje awali na kwamba juzi ndio waliosababisha wabunge wawili wanawake wa chadema wapite hazina mashiko.

Alisema wabunge wa CCM wapo 275 na upinzani ni zaidi ya 116, lakini Profesa Safari alipata kura 35 ambazo siyo nusu hata ya wabunge wa Chadema.

“Kwa hiyo uchaguzi ulifanywa na wabunge wote, kama Profesa Safari alipata kura 35 kwanini ilaumiwe CCM? kama Chadema wote wangempa, si angekuwa na kura nyingi, sasa kwanini tu mbaya aonekane ni CCM?

“Lakini nafasi zilikuwa ni mbili, wameleta wagombea sita, lazima wawili washinde, wengine wabaki, kwa hiyo kuilaumu CCM ni ujinga na wakome mara moja,” alisema.

ZItto akerwa

Juzi mara baada ya kutangazwa kwa matokeo, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), alionekana kuchukizwa na matokeo hayo na kujutia hata kuwa raia wa Tanzania.

Jana tena akaandika “Jana (juzi) usiku, nilikuwa nimekwazika kufuatia matokeo ya uchaguzi wa wawakilishi wa Tanzania kwenye Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

“Kufuatia hasira hiyo, nikaandika wakati mwengine unajiuliza kama unastahili kuwa kwenye nchi ambayo umo kama raia.

“Haikuwa sahihi kabisa kwa kiongozi wa ngazi yangu kujutia uraia wangu kwa sababu tu ya kundi la watu wachache kuamua kuchagua wawakilishi wetu kwenye taasisi za kimataifa bila kujali uwezo, uzoefu na weledi wa wawakilishi husika.

“Ndiyo maana  mataifa mengine yamepeleka raia wao mahiri kabisa. Rwanda wamepeleka Waziri Mkuu mstaafu na mawaziri wawili, Burundi imepeleka waziri wake wa Afrika Mashariki.

“Uganda imepeleka mawaziri wastaafu. Kenya imepeleka wabunge wazoefu na wafanyabiashara wakubwa. Hata mwanachama mpya Sudani ya Kusini imepeleka waziri wa zamani, Spika wa Bunge wa zamani na jenerali wa jeshi.

“Hasira za kuipenda nchi yangu ndio zilinipelekea kuandika nilivyoandika. Naomba radhi kwa andiko lile na ninalifuta. Hata hivyo, wabunge wote wa vyama vyote wajue kuwa wameionea nchi yetu,” alisema.

Mahanga

Suala la uchaguzi huu pia, jana na juzi lilitawala kwenye mitandao ya kijamii, ambapo Kada wa Chadema, Makongoro Mahanga, alisema. “Wabunge wote sita walikuwa na sifa ya kuchaguliwa na hakukuwa na wagombea wa Mbowe.

“Sasa wabunge wa Chadema bungeni wako 72, ukichukua hata na CUF, nadhani, Ukawa wana wabunge kama 110.

“ Ina maana Ukawa walikuwa na jumla ya kura 220. Hizo kura 220 ukigawa kwa wagombea wetu sita (ambao wote walistahili kupata kura) ina maana kila mgombea wetu alikuwa na wastani wa kura 36 tu toka Ukawa. Kwa hiyo matokeo hayana nia yoyote ovu lililopangwa na wabunge wa Chadema au Ukawa, bali yanaonyesha mambo mawili

“Moja  CCM kupanga kutogawa kura zao kwa wagombea sita bali zote kuzipeleka kwa wawili tu (wanawake).
“Mbili Chadema ingepeleka majina matatu tu ili CCM wasipate wigo mpana sana wa kuacha wagombea wetu wengi. Tumejifunza, tusonge mbele tukijua CCM ni ile ile,”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles