28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

WABUNGE CCM WAZIDI KUNYUKANA

Mbunge wa Geita, Joseph Kasheku, akichangia mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji ya Mwaka 2017/2018, bungeni jana. Picha na Deus Mhagale

Na MAREGESI PAUL-DODOMA

WABUNGE wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanazidi kunyukana hadharani, huku wengine wakipingana kutokana na kauli wanazotoa bungeni.

Mnyukano huo umekuja baada ya waliowahi kuwa mawaziri wa Rais Dk. John Magufuli, kupinga wazi wazi bajeti ya Wizara ya Maji kutokana na kutopewa kipaumbele miradi kwenye majimbo yao.

Wengine walionya ikiwa maji hayatapelekwa kwa wananchi majimboni mwao Chama Cha Mapinduzi (CCM) kina hatari ya kuondoshwa madarakani mwaka 2020.

Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma (CCM), amewashambulia kwa maneno wabunge wenzake wa CCM, Charles Kitwanga wa Misungwi na Nape Nnauye wa Mtama.

Tukio hilo lilitokea bungeni jana, wakati mbunge huyo alipokuwa akichangia bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa mwaka wa fedha 2017/18 iliyowasilishwa juzi na Waziri Gerson Lwenge.

Wakati akichangia wizara hiyo juzi, Kitwanga alilalamikia uhaba wa maji jimboni kwake na kutishia kwenda kuwahamasisha wananchi wapatao 10,000 wa jimbo lake wakazime mtambo wa maji ulioko jimboni humo kwa kuwa hauna faida kwa wananchi, kwani hawapati maji.

Kwa upande wake Nape alisema kama Serikali haitapeleka maji kwa wananchi kama ilivyoahidi katika ilani yake CCM inaweza isirudi madarakani 2020.

Katika tukio la jana, Musukuma alisema maneno waliyoyatoa wabunge hao hayawezi kukubaliwa kwa sababu hayana sababu za msingi.

“Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza mheshimiwa Rais na Waziri wa Maji na Umwagiliaji kwa kazi wanayofanya kwenye wizara hiyo kwa sababu sisi wengine ni waathirika wa ukosefu wa maji kwa miaka mingi na sasa tunaona mabadiliko yanavyokweda kwa spidi.

 “Suala jingine nataka kuwazungumzia wana CCM wenzangu ambao jana nilisikiliza mchango wa mheshimiwa Kitwanga akilalamika kwamba atamobilize wananchi 10,000 wa Misungwi ili wakazime mtambo wa maji pale Iherere.

“Nilisikitika sana na nataka niwaulize kwamba, nyinyi mawaziri wa Magufuli hivi vile viapo mnavyokula mnajua maana yake?

“Kama hamjui maana ya hivi viapo, basi sina hakika kama mko sawasawa na kama hamko sawaswa, Ndalichako (Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia), hebu pitisha operesheni ya vyeti feki huenda hapa penyewe kuna feki za kutosha.

“Hivi inawezekana vipi mtu uliyekuwa waziri unasimama hapa na kusema ulipokuwa waziri ulikuwa umebanwa kuzungumza na baada ya kufukuzwa sasa uko huru kuzungumza?

“Hebu ngoja niwakumbushe tukio la mwaka 2014 ambapo Mheshimiwa Kitwanga alipokuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini akisimamia madini, alikuja Geita mimi wakati huo nikiwa Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Geita.

“Niliwaambia wananchi pale mgodini wasitoke mpaka walipwe fedha zao na mzungu na baadaye Kitwanga akaja akamwambia mkuu wa mkoa, kwamba hata kama kuna mwenyekiti, wapigwe mabomu na kweli kesho yake tulipigwa mabomu.

“Kwa hiyo, nataka nimwambie Waziri wa Mambo ya Ndani, kwamba Kitwanga akienda kuhamasisha wananchi pale Misungwi, peleka mabomu naye aonje joto ya jiwe kwa sababu haiwezekani waziri uliyekula kiapo uje hapa na kutuchanganya baada ya kutimuliwa wakati sisi hatujui mliyokuwa mnazungumza kwenye kabineti,” alisema Msukuma.

Akimzungumzia Nape, Musukuma alisema kauli yake ya juzi, kwamba CCM isipopeleka maji kwa wananchi itaangushwa madarakani haiwezi kukubaliwa kwa sababu wananchi hawakipimi chama hicho kupitia sekta ya maji pekee.

Kwa mujibu wa Musukuma, hadi sasa wananchi wanaiamini CCM kwa sababu imewafanyia mambo mengi mazuri na pia hakuna awamu yoyote ya kiserikali iliyowahi kutimiza ahadi zote ilizojiwekea katika ilani ya uchaguzi.

“Jingine ni la Nape ambaye jana (juzi) alichangia hapa. Nape alikuwa Katibu Mwenezi wangu wa Taifa wa chama changu na jana alizungumza mambo mazuri, lakini kuna moja alisema tusipowatekelezea wananchi suala la maji hawataturudisha madarakani.

“Hilo haliwezekani kwa sbabu wananchi wanatutegemea kwa mambo mengi na siyo maji peke yake na tumewafanyia mengi mazuri.

“Pamoja na hayo, ilani hazijaanza kuandikwa kwenye awamu ya tano, ilani tumezipitisha awamu nyingi na hakuna hata ilani moja iliyowahi kutekelezwa kwa asilimia mia moja.

“Suala hapa siyo kulazimisha kila kitu kikamilike katika awamu hii, tusibebeshane mzigo kwa sbabu hakuna rais aliyewahi kutekeleza ahadi zote. Kwa hiyo tupeane nafasi kwani Rais wetu anafanya kazi nzuri tusianze kumchambachamba humu ndani.

“Lakini pia, kama Kangi Lugola anataka kuzunguka na sauti za wabunge watakaoiunga mkono bajeti ya maji kwa kusema ndiyo, basi ajiandae kuzunguka na sauti ya besi ambayo hajawahi kuisikia,”alisema Musukuma huku akishangiliwa.

KANGI LUGOLA

Awali, Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), alipokuwa akichangia hotuba ya bajeti hiyo, aliwataka wabunge washirikiane kuitaka Serikali iongeze fedha katika bajeti hiyo ili miradi mingi ya maji iliyokwama, iweze kutekelezwa.

“Waheshimiwa wabunge, mbunge yeyote atakayepitisha bajeti hii kwa kusema ndiyoooo wakati nchi haina maji, nitaanzisha mwenge wangu kwa kwenda kuchukua sauti zenu katika hansard ili nizipeleke kwa wananchi nikawaambie mnavyounga mkono bajeti ya maji wakati nchi haina maji,”alisema Lugola.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, maji ni muhimu katika maisha ya binadamu kwa sababu hata Yesu alipotaka kukata roho msalabani, alisema anaona kiu ya maji.

“Kwa hiyo, pamoja na umuhimu wa maji katika maisha yetu, huko vijijini wananchi hawana maji na wengine wanaoga kwa zamu na wanapooga, wanaoga katika maeneo muhimu ya miili yao,”alisema.

Katika siku za hivi karibuni wabunge hao wa CCM wamekuwa wakirushia maneno ndani ya Bunge ambapo Mbunge wa Viti Maalumu, Lucy Mayenga, alionya watu wanaompiga vita Rais Magufuli na kuwataka wamwache afanye kazi yake.

Naye Munde Tambwe, aliwataka wabunge kuacha kuishambulia Serikali pamoja na mawaziri kwani kazi inayofanywa na CCM katika nchi hii ni kubwa.

Wakati wabunge hao wakisema hayo Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Kessy, alishangazwa na baadhi ya wabunge kutaka wasanii wa muziki wa kizazi kipya waendelee kuimba hali ya kuwa wanamtukana Rais Dk. Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles