Na ELIUD NGONDO
HALMASHAURI ya Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya imesimamisha ubomoaji wa nyumba zaidi ya 600 katika eneo la mbuga ya kilimo cha mpunga Tenende.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Hunter Mwakifuna alisma katika kikao cha Baraza la Madiwani alisema tangazo la halmashauri hiyo la mwaka 2015 kuwataka wananchi wabomoe nyumba walizojenga ndani ya mbuga sasa limesimamishwa.
Alisema hatua hiyo imesimamishwa hadi yatakapofanyika marejeo ya mpango wa uendelezaji wa eneo hilo mwaka 2018.
“Mpaka sasa kuna nyumba zaidi ya 900 ambazo zimejengwa katika eneo hilo la mbuga ya Tenende na baadhi ya madiwani wa halmashauri hii nao wana nyumba katika mbuga hiyo,” alisema Mwakifuna.
Alisema mbuga hiyo ina ukubwa wa hekta zaidi ya 970 lakini hekta zaidi ya 70 zimevamiwa na waliovamia sasa wanatakiwa wasiendeleze kujenga eneo hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Musa Mgata alisema ongezeko la uvamizi wa mbuga hiyo umetokana na baadhi ya watendeji wa idara ya ardhi kuuza maeneo kwa wananchi.
Alisema eneo hilo lilikatazwa kujengwa lakini kuna watendaji walioamua kukiuka na kuwauzia wananchi wengine nje ya wale waliokuwapo awali.
“Mbuga ya Tenende ilitengwa kwa mpango maalumu wa kuhifadhi maeneo kwa ajili ya uendelezwaji wa kilimo cha mpunga mwaka 2008 ikiwa ni kukabiliana na upungufu wa chakula katika wilaya hii,” alisema Mgata.
Mgata alisema mbuga hiyo imezungukwa na kata za Serengeti, Ikama, Mwanganyanga na Itumba.
Alisema wananchi hao walitakiwa kufidiwa na halmashauri lakini eneo hilo lilivamiwa na waliovamia wanatakiwa kutoendelea na ujenzi.
Veronica Kanyigila, diwani Kata ya Lusungo (CCM) alisema wananchi wamekuwa wakijichukulia uamuzi wa kujenga na kusababisha migogoro isiyokuwa na tija.
Alisema ulikuwapo mgogoro wa muda mrefu ambao umekuwa unarudisha nyuma mipango ya halmashauri kutokana na wananchi kudai fidia na kusimamishwa kwa hatua hiyo kutapunguza malalamiko hayo.