Na Hamisa Maganga, aliyekuwa Nairobi
KUKUA kwa teknolojia kumechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha maisha ya mtu mmoja mmoja na mataifa mbalimbali duniani.
Lakini wakati mwingine kunaweza kukaharibu biashara za watu ambao bado wanaishi ki-analogia jambo ambalo huchangia kudumaza maendeleo.
Kampuni ya Kimataifa ya magari ya teksi (Uber), hivi majuzi ilijikuta ikijizolea umaarufu mkubwa barani Afrika baada ya kusababisha mzozo mkali kati yao na madereva wa teksi jijini Nairobi, Kenya.
Nikiwa jijini humo kwa ziara ya kikazi iliyodhaminiwa na Shirika la Ndege la Fastjet, nilijikuta nikihamasika kufanya mahojiano na mahasimu wawili – madereva wa teksi za kawaida na wale wanaotumiwa na Uber.
Katika mahojiano hayo nilibaini mambo mengi lakini kubwa zaidi ni jinsi Uber wanavyokwepa kulipa kodi nchini humo.
Lingine ni jinsi wanavyowanyanyapaa madereva teksi wa kawaida wakidai kuwa ni wachafu na magari yao ni kuukuu.
Upinzani dhidi ya Uber na teksi za kawaida Kenya
Kampuni ya Uber imezidi kuimarika kutokana na kuwavutia wateja kwa kile wanachodai kuwa wanatoza nauli nafuu.
Suala hilo limewafanya madereva wa teksi za kawaida katika Mji Mkuu wa Kenya, Nairobi, kulalamika na kupinga vikali Uber kuingia kwenye soko.
Hatari ya kuendesha magari hayo imekuwa kubwa hadi polisi na Wizara ya Uchukuzi nchini humo ililazimika kuingilia kati mgogoro unaoendelea kati ya madereva wa Uber na teksi za kawaida.
Huku hayo yakiendelea, Uber inazidi kufungua matawi katika Mji wa Mombasa.
Hoja za madereva teksi za kawaida
Dereva wa teksi, Leornad Kurya, anasema hawawezi kusema kuwa Uber ni wabaya kwa sababu hawawezi kushindana na mabadiliko ya kidigitali.
Anasema biashara hiyo ni nzuri kwa kuwa walioajiriwa ni Wakenya, kwa hiyo kama kulikuwa na kijana ambaye hakuwa na kazi ya kufanya, Uber imempati fursa.
“Unajua mabadiliko ndani ya nchi ni mazuri, magari ya Uber yanazingatia usalama wa mteja na dereva pia.
“Kama watu wanaona Uber wanawawekea kauzibe, si vibaya wakabuni mbinu nyingine za kuwateka wateja, waanzishe wavuti zao ambazo zitawasaidia kupata wateja kwa urahisi, lakini kama tutaendelea kuwapiga basi tujue wazi kuwa tunazidi kuwatangazia biashara bila ya sisi kujua,” anasema Kurya.
Anasema kuwa Uber imekuja na nguvu kubwa kwani biashara yao ya siku nyingi imetupwa mbali na magari yao na imejulikana kwa haraka kuliko kampuni nyingine zilizopo nchini humo.
Anasema kuna kampuni nyingi Kenya zinazofanya kazi hiyo lakini hazijajizolea umaarufu kama ilivyo kwa Uber.
Anabainisha kuwa kutokana na ushindani wa biashara uliopo nchini humo, sasa hivi Kenya hakuna madereva ambao si waaminifu kwa kuwa akitokea ambaye anawaharibia biashara humchukulia hatua kali.
Akizungumzia kipato anachopata kwa siku kupitia kazi hiyo anasema ni kizuri japo si sana.
“Hii biashara ni nzuri na inalipa tofauti na kukaa kijiweni bila ya kazi. Naweza kwa wiki nikapata KSh 12,000 (sawa na Sh 240,000 ya Tanzania),” anasema.
Naye Joseph Wamarwa, anasema Uber wanafanya kazi bila ya kuwa na kituo maalumu jambo ambalo linaikosesha nchi mapato kwa kuwa hawatozwi kodi.
Anasema biashara hiyo pia imejenga matabaka nchini humo kwa kuwa inabagua walionacho na wasionacho.
“Hawa Uber ni wazuri isipokuwa wanachokosea ni kutubagua, wazee wanaotaka kufanya kazi hii wanashindwa kwa sababu hawawezi kutumia Smartphones (simu za kisasa).
“Lakini pia wanabagua magari, yaani gari kama hili (anaonyesha gari lake) haliwezi kufanya kazi na Uber kwa sababu namba zake ni A,” anasema Wamarwa.
Anasisitiza kuwa magari ya zamani hayatakiwi na kwamba wanataka magari mapya yenye namba C na D. Mfano magari yenye namba KCW, ndiyo yanayohitajika na yenye KAV hayatakiwi kufanya kazi na Uber.
Anasema asilimia 50 ya wamiliki wa magari hasa madereva teksi wamekopa magari yao, jambo ambalo linawawia vigumu wengine kukopa kwa kuwa vigezo na masharti yanayotakiwa ni magumu.
Kwa upande wake Morrison kamau, anasema kuwa wao ndio wanafanya kazi kwa haki kwa kuwa wanalipa ushuru tofauti na Uber ambao hawaingizi kitu serikalini.
Anasema Serikali inapaswa kuja na mikakati kabambe kuhakikisha kuwa inaboresha biashara hizi mbili.
“Kama Serikali inataka amani inapaswa kukaa na sisi sote ili tuzungumze lugha moja, la sivyo mambo lazima yaharibike na umaskini na uhalifu hautaisha.
“Sisi tunalipa ushuru wenzetu hawalipi, wanafanya kazi bila vikwazo vyovyote hivyo wanatuharibia biashara,” anasema Kamau.
“Anasema; “walipokuja kwa mara ya kwanza tuliwashtua kidogo, hawawezi kufanya biashara kiurahisi kama wanavyotarajia, lazima tuwashtue ili wajue kuwa wametuudhi, lakini wasihofu huu uhasama utaisha tu.
Anasisitiza kuwa kampuni zingine zinazofanya kazi kama Uber ikiwamo Mundo, Easy tax zenyewe zina stika za halmashauri kwenye magari yao tofauti na ilivyo kwa Uber.
Akizungumzia suala la unafuu anasema kuwa Uber hawana unafuu kwa kuwa wanatoza kwa umbali huku wakiangalia kilomita walizotumia, na kwamba kama barabarani kuna foleni ni lazima gharama ipande.
Anasema wao wanakubaliana na mteja kabla hawajaanza safari, hivyo kama ni mbali, karibu au barabara ina foleni, hasara huwa ni ya mteja.
“Hakuna urahisi wowote, tena unaweza kugundua kuwa wao wapo juu zaidi yetu. Mimi ninapopata mteja ni lazima nitatafuta njia za mkato ili niwahi kurudi nitafute mteja mwingine, lakini yeye anaweza kukupeleka taratibu tena kwa njia ya mbali ili mradi tu umlipe fedha nyingi, hiyo ndio tofauti yetu,” anasema Kamau.
Dereva wa Uber
Dereva wa Uber Geofrey Washira anasema huwezi kuufananisha usafiri huo na teksi za kawaida.
Anataja tofauti iliyopo kati ya Uber na teksi za kawaida kwamba madereva wao ni waongo wakati Uber ni wawazi hawezi kukudanganya kwamba yuko karibu wakati yuko mbali.
“Tofauti nyingine ni kwamba sisi tukikuendesha unakuwa na uhakika wa usalama wako binafsi na mali zako, ni wasafi ukilinganisha na madereva wengine, hii ni kwa sababu kabla ya kuanza kazi ni lazima uchunguzwe kuanzia mavazi, historia yako kama uliwahi kufanya uhalifu au la.
“Huwezi kuruhusiwa kufanya kazi na Uber kama una historia mbovu au ni mchafu. Pia sisi tunajali muda, tunamuhudumia mteja kwa haraka zaidi kuliko hao wengine,” anasema Washira.
Anasema sifa nyingine ya Uber ni kwamba hawawezi kuchukua abiria kama hajampigia simu hata kama amemsimamisha barabarani.
Madereva wake wapigwa
Wiki mbili zilizopita dereva wa Uber aliteketezwa kwa moto.
Polisi walisema kuwa gari hilo la Uber lilichomwa moto katika kitongoji cha Riruta jijini Nairobi na watu wanne waliokuwa wakilisubiri, lakini hata hivyo dereva alinusurika kifo.
Inasemekana watu hao waliungana na mteja wa Uber ambaye alikodisha teksi hiyo, lakini dereva aliruka kutoka ndani na kukimbia.
Hili ni tukio la pili la aina hii katika kipindi cha mwezi mmoja katika Jiji la Nairobi ambapo
Februari, madereva teksi za kawaida walifanya maandamano jijini Nairobi na kuipa siku saba kampuni ya Uber iwe imesitisha shughuli zake nchini Kenya, baada ya kuishutumu kuvunja sheria za nchi na kuhusika kuwa na ukoloni mamboleo.
Kuja Tanzania
Meneja wa Uber Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Alon Lits, anasema kampuni hiyo ipo mbioni kuja Tanzania.
Anasema wako vizuri na wana mpango wa kutanua biashara zao kwenda mbali zaidi.
Akizungumzia vitendo wanavyofanyiwa madereva wao nchini Kenya, Lits anasema tayari wamewasilisha malalamiko yao kwa serikali ili kudhibiti vitendo hivyo.
India iliharibu
Desemba mwaka juzi, kampuni hii ilishtakiwa nchini India baada ya dereva wake mmoja kushutumiwa kumbaka abiria wa kike.
Kutokana na tukio hilo, ilishutumiwa kwa kuwapotosha wateja kutokana na kushindwa kuwachunguza kwa ukaribu madereva wake.
Mwanamke aliyebakwa alikuwa na umri wa miaka 26, ambaye alitumia simu ya mkononi kuomba kupata huduma ya teksi kuelekea nyumbani badala yake alipelekwa mafichoni na kubakwa.
Dereva huyo baadaye alikamatwa na kufikishwa mahakamani.
Jinsi Uber inavyofanya kazi
Magari ya Uber ambayo yamejijengea umaarufu mkubwa nchini Kenya na India, yanafanya kazi kwa simu, ambapo mteja humlazimu kumwita dereva kupitia simu yake ya mkononi kupitia www.Uber.com.
Dereva anapowasili hakutajii gharama ya unakokwenda bali anakuchukua na kuseti simu yake baada ya hapo safari inaanza, ukifika unakokwenda simu ndio inakwambia unadaiwa kiasi gani cha fedha.
Uber hawana kituo maalumu na madereva wake kabla ya kuanza kazi wanapewa mafunzo.
Wanachaji abiria kulingana na kilomita, hivyo kadiri unavyochelewa kufika ndivyo gharama huongezeka. Kwa hiyo kama kuna foleni kubwa kama za hapa kwetu unaweza kujikuta ukilipia Sh 50,000 kwenye safari ambayo ingekugharimu Sh 20,000 za Kitanzania.