23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Upande wa pili wa shilingi Jiji la Dubai

Vibarua kwa kawaida hufanya kazi kwa saa 14 ikiwamo wakati wa joto kali la nyuzi joto zaidi ya 50DUBAI ni moja ya majiji yenye sifa za kipekee duniani linapokuja suala la ubunifu, utajiri, uzuri, ubora, mvuto wa majengo na miradi yake ya maendeleo.

Jiji hilo la Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE), lililopo kusini mashariki mwa Pwani ya Persia lina wakazi zaidi ya milioni mbili.

Ijapokuwa msingi wa uchumi wake kihistoria umejengwa kupitia sekta ya mafuta, ufalme huo umefanikiwa kubadili hilo kwa kuuelekeza katika sekta za utalii, anga, mali zisizohamishika na huduma za kifedha.

Nembo inayolitambulisha jiji hilo ni majengo yake marefu yanayochungulia mbinguni (skyscrapers) ikiwamo refu kuliko yote duniani- Burj Khalifa.

Kwa maana hiyo, utakayoshuhudia humo hata kama umetokea katika mataifa ya magharibi, ziliko teknolojia za juu hukuacha mdomo wazi hasa mpangilio na aina ya ubunifu wa miradi ya maendeleo.

Hiyo ni pamoja na visiwa vilivyotengenezwa na binadamu, ikiwamo vilivyo mfano wa mti wa mchikichi na matawi yake, hoteli na maduka makubwa kabisa katika ukanda wa mashariki ya Kati na duniani.

Ni katika jiji hilo ndiko iliko inayoaminika kuwa hoteli pekee duniani ya nyota saba-.Burj Al Arab.

Hata hivyo, kuna upande mwingine wa shilingi wa jiji hilo tajiri na linaloonekana kuwa la matajiri, ambao wengi hawaufahamu.

Mbali ya wengi wakiwamo watalii kutoufahamu, mamlaka za UAE haziko tayari kuuanika, bali kuufuta kutoka katika ramani.

Hayo yaliweza kufichuliwa na mpiga picha wa Iran, Farhad Berahman, aliyeanika namna vibarua kutoka Asia Kusini wanavyoishi kimasikini katika sehemu nyingine ya jiji hilo.

Vibarua hao husafiri kutoka kwao kwenda Dubai kwa matumaini ya kutengeneza mustakabali sahihi wa familia zao kwa siku za usoni, lakini hujikuta wakiiishi kidhalili, mishahara midogo na kazi ngumu kwenye jua kali.

Picha za Farhad zilichukuliwa huko Sonapur, jina lisilo rasmi la kambi ya wafanyakazi, moja ya vitongoiji vya Dubai, vilivyotengwa mbali kabisa na ma-skyscrapers na kila aina ya kile ambacho jiji hilo tajiri la UAE limebarikiwa.

‘Sonapur’ – jina linalomaanisha ‘Jiji la Dhahabu’ kwa Kihindi – ni hifadhi ya wafanyakazi 150,000 wengi wao kutoka India, Pakistan, Bangladesh na China.

Miaka 30 iliyopita, karibu eneo zima la Dubai lilikuwa jangwa lakini likakua haraka hadi kuwa kitovu cha biashara na utalii ukanda wa Ghuba ya Persia na Mashariki ya Kati.

Mpiga picha huyo amekuwa akiitembelea Dubai mara kwa mara na aliweza kujionea jinsi jiji hilo lilivyokuwa na kubadilika haraka kufikia hapo lilipo leo hii.

Na hivyo anafahamu vilivyo uwapo matabaka matatu tofauti ya watu wanaoishi Dubai; raia wa ufalme huo, wataalamu wa kigeni na mwisho vibarua ambao ndio nguvu kazi inayoujenga mji huo.

Farhad anaeleza kuwa wafanyakazi kadhaa wamejikuta hati zao za kusafiria zikikamatwa uwanja wa ndege na kulazimishwa kufanya kazi kwa malipo madogo duni.

Hupelekwa Sonapur – ambayo haiko katika ramani inayojulikana ya Dubai ili waweze kudhibitiwa kirahisi na waajiri wao.

Mpiga picha huyo, alizungumza na kibarua mmoja aitwaye Jahangir kutoka Bangladesh, ambaye ana umri wa miaka 27 akiwa katika mwaka wake wa nne kama mfanyakazi wa usafi.

Amekuwa akilipwa Dirham ya UAE (AED) 800 sawa na Sh 380,000 kwa mwezi na kuitumia familia yake AED 500 sawa na Sh 240,000. Analazimika kuishi kwa tabu na kiasi kidogo kilichobakia.

Farhad anaeleza; “Watu huja katika nchi hii wakiwa na matumaini makubwa ya kutengeneza mustakabli wao ujao na kunufaika na uwekezaji mkubwa katika sekta ya ujenzi na mafuta.

“Kuna mahoteli mengi ya kifahari na miradi maarufu ya kidunia, ambayo vibarua hao wameijenga katika miaka ya hivi karibuni.

Mwajiri kwa kawaida huchukua hati zao za kusafiria mara tu wanapowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Dubai na wote hupelekwa Sonapur.

Vibarua kwa kawaida hufanya kazi kwa saa 14 ambapo wakati wa kiangazi hali joto hufikia zaidi ya nyuzi joto 50.

“Kwa kawaida hushauriwa watalii wa kimagharibi kutokaa nje kwa zaidi ya dakika tano wakati wa kiangazi.

Kwa mujibu wa sheria za serikali, maeneo ya kazi hutakiwa kusimamisha kazi wakati wa hali joto ya kiwango hicho ili kutoathiri vibarua na afya zao.

Lakini serikali yenyewe mara nyingi huwa haitangazi hali halisi ya hewa kwa makusudi kabisa.

Wakati Farhad alipowasili aliona wanaume wengi wamekaa uani kwenye fenicha mbovu, wakipika katika majiko machafu na huku wanyama wakizurura ovyo.

Aliongeza; “Vyumba wanavyoishi ni futi 12 kwa futi 12 vikiwa na vitanda sita na kuhifadhi watu sita hadi nane.

Chakula kwa kawaida hupikwa kwa kutumia gesi na katika hali na mazingira mabaya tena ya kutisha.

“Mmoja wa wafanyakazi wa Kichina alinipeleka katika chumba chake na kunionesha alama aliyoiandika katika baadhi ya mbao.

Inasomeka; “Mpendwa bosi ninafanya kazi katika kampuni yako mwaka mmoja sasa, mkataba wangu umeisha lakini sipati mishahara yangu kama ipasavyo kwa miezi minne. Napaswa kurudi nyumbani China karibuni, tafadhali nilipe fedha zangu.

Wataalamu wa kigeni, ambao wana vipato vikubwa kamwe hawakabiliani na upande huu giza wa Dubai, ambao vibarua wanaishi katika mateso na mbali na vyombo vya habari.

Farhad anasema alishtushwa wakati alipojionea hali halisi na kuamua kupiga picha mbalimbali.

Alisema; “Sikujaribu kupata ruhusa kwa sababu maeneo haya yamezuiwa kuonekana kwa umma na nilikuwa na hakika nisingefanikiwa kwa sababu UAE huwa haioneshi sehemu hii ya nchi yao.

“Hivyo nilichukua picha usiku wakati ambao ilikuwa rahisi kidogo kujificha kuwakwepa walinzi. Haikuchukua muda nikaanza kukutana na vibarua na kufahamiana, nilitambua kuwa walinihofia.

“Baadaye mmoja ya vibarua ambaye aliweza kuzungumza Kiingereza aliniambia kuwa waliogopa pengine nilitokea serikalini.

Aliongeza; “Muda mwingi nilishinda garini mwangu na kusubiri giza liingie ili niweze kuifanya kazi yangu iliyonipeleka hapo.

Pamoja na juhudi zake hizo mpiga picha huyo, alikamatwa na walinzi na kuhojiwa.

“Nilijifanya kuwa mtalii niliyepotea njia na walinzi walitaka kuniripoti polisi kwa sababu eneo la vibarua ni marufuku kupiga picha.’ Bahati nzuri kwa kudra za Mungu wakamwachia.

Mpiga picha huyo wa Iran ana matumaini kuwa picha zake hizo zitawafanya watu wafikirie mara mbili nini kinachoendelea katika upande huu mwingine wa nchi hiyo hasa maisha ya udhalili wanayoishi watu ili wapate msaada.

“Kuwatendea wanadamu wenzako ukatili ni kinyume cha haki za binadamu, siwezi kumwambia mtu yeyote nini cha kufikiria kuhusu picha hizo lakini naamini zinazungumza zenyewe,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles