33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

TWIGA CEMENT YAMILIKI SOKO LA SARUJI KWA KISHINDO

Na Shermarx Ngahemera

KUJIKWAA si kuanguka, ndio maelezo stahiki kuelezea hali ya soko la saruji baada ya wazoefu wa soko hilo Tanzania Portland Cement (TPCC) au Twiga Cement kama jina la chapa yao, kuzinduka usingizini na kupigania uongozi wake kwenye soko la bidhaa hiyo nchini.

Dude limezinduka  na sasa wamelishika soko ambalo lilianza kuponyoka kutokana na ujaji wa Kampuni ya Dangote  Cement kule Mtwara ambao wana uwezo mkubwa  wa uzalishaji kuliko viwanda vyote nchini vikiunganishwa  na kuja na dhana isiyozoeleka ya ugavi wa saruji kwa wateja  wake badala ya kuifuata wao wenyewe kiwandani na hivyo kutibua masoko ya wengine.

Dangote kiwanda chake kina uwezo wa kuzalisha saruji ya tani milioni tatu  kwa mwaka, ingawa hadi sasa imefikia tani laki saba tu kutokana na uzalishaji unaokatikakatika kwa sababu mbalimbali.

Dangote Cement ina matatizo ya nishati kwani umeme unaohitajika kuendesha mashine zote kiwandani upo kwa kiwango  kidogo, hivyo kufanya sehemu tu ya uwezo wake. Makaa ya mawe bado ni shida  pamoja na juhudi ya Rais Magufuli kuipa kampuni hiyo sehemu ya kuchimba makaa yake kule Mbinga. Gesi asilia bado haijafungwa kwa hiyo inakosa mbadala wa mambo mengi.

Awali Mwenyekiti wa kampuni hiyo, Alhaj Aliko Dangote, alisema anahitaji eneo la makaa ya mawe ili ajenge mitambo ya kuzalisha umeme wa megawati 75, ambapo angetumia kiwandani megawati (MW)  50 na angeuza  megawati  25 kwenye gridi ya Taifa kwa watumiaji wengine  wa nishati hiyo.

Upatikanaji wa eneo ulichukua muda mrefu sana na hivyo kiwanda kufunguliwa kabla hata suala la upatikanaji umeme  kutatuliwa na hivyo kufanya uzalishaji wa saruji katika kiwanda hicho kuwa ni mdogo na wa mashaka.

Kitendo cha Rais Magufuli kumpa Dangote eneo la makaa ya mawe,  halikupokelewa vizuri na wazalishaji wengine ambao walidai kuwa upendeleo huo wa rais ulikuwa unajenga uwanja usio sawa na hivyo kuleta manung’uniko kwa wale ambao hawana migodi.

Lakini Ikulu ilijibu kuwa hakuna kiwanda kilichoomba ila kile cha Dangote  na hivyo kikapewa  na kudai kuwa huwezi ukampa mtu rasilimali asiyoihitaji, kwani inapotolewa hutolewa na mashariti yake kwani nia na madhumuni huainishwa kwenye maombi hayo kama mtu akiomba na si vinginevyo.

Mkurugenzi wa Tanga Cement (Simba cement), Reinhardt  Schwartz ndiye aliyelalamika alipokutana na wahariri mjini Tanga, kuwa viwanda vingine vimeonewa kwa kutokupata sehemu ya kuchimba makaa ya mawe,  kitu ambacho kimezua majadiliano makali.

Hata hivyo, wataalamu  wa uchumi wanahoji  mwenendo unaoonekana kushamiri wa kiwanda kimoja kumiliki uchumi  wote, kwani wanahoji uchumi hauwezi ukamilikiwa na viwanda vichache ila wao wazalishe saruji kwa kuchukua malighafi kwa wazalishaji wengine  au wafanyabiashara wanaoshugulika na malighafi hizo ili kuleta urari katika soko na uchumi mpana.

Inasemekana Rais Magufuli  alifanya hivyo kutokana na ahadi za awali za Serikali kwa Dangote kumpunguzia gharama nyingi za uzalishaji  na kuwekeza katika eneo jipya la uwekezaji ambapo kila kitu kinabidi kijengwe na hivyo kupewa motisha huo lakini si bure bali atalipia ada  na tozo zote kama  mchimbaji  wa kawaida.

Baada ya uwekezaji mkubwa kukuza uzalishaji  na kupata sehemu ya kutumia gesi asilia, Kampuni ya Twiga Cement imekuja juu kiushindani na kibiashara kwa kuchukua mikataba yote mikubwa nchini itakayotumia saruji  na kokoto zake kutoka wilayani Chalinze.

TPCC ndio inatoa saruji kwa miradi ya Reli ya Kati (SGR) Dar hadi Morogoro, Mradi wa Upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Barabara ya Dar  hadi Chalinze na barabara za juu  (flyover) za Tazara na Ubungo na Bomba la Mafuta la kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga kwenye Kijiji cha Chongoleani.

“Dangote alitumia ushindani wa bei ya saruji kama kigezo chake  cha kupata masoko, lakini kigezo hicho peke yake hakitoshi kwa watu wenye miradi ambao wanataka uhakika na ubora wa bidhaa pamoja na ukaribu, vitu ambavyo Dangote hana,” alidai mfanyakazi mmoja katika idara ya Masoko ya Twiga na kutaka jina  lake lisitajwe kwani si msemaji wa kampuni hiyo.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles