32.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 12, 2024

Contact us: [email protected]

PRECISION YATAFUTA KWA UVUMBA UHUSIANO THABITI ATCL

Na LEONARD MANG’OHA

TANGU kufufuliwa kwa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), kumesaidia kuimarisha utendaji wa shirika hilo lililopoteza mwelekeo kiasi cha kushindwa kujiendesha kutokana na ndege zake kuwa katika hali isiyoridhisha.

Kufufuliwa kwa ATCL kunaonekana kuibua ushindani kwa mashirika binafsi ya ndege ya hapa nchini.

Sauda Rajab ni Mkurugenzi Mkuu wa Precision Air, anasema ushindani wa bei mara zote huwa ni wenye hasara kwa watoa huduma husika yaani kwa suala hilo ni mashirika ya ndege.

Anasema kufufuliwa kwa ATCL kumeongeza ushindani katika soko la usafiri wa anga ambalo ni jambo zuri kwa abiria kwa kusaidia kupunguza gharama za tiketi.

“Ujio huo kwa upande mwingine umeleta msukumo wa ushindani kwenye nauli, jambo ambalo limesababisha mashirika kuweka nauli ambazo hazina tija sana katika uendeshaji.

“Ukifuatilia kwa karibu utagundua mashirika yote hapa nchini yanatengeneza hasara na sababu mojawapo kubwa ni kuwa na bei zisizo na tija sana kwenye uendeshaji wa mashirika,” anaeleza Sauda.

Hivi karibuni wakati wa ziara ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano katika mkutano na wafanyabiashara waliopanga katika majengo ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Precision Air, Sauda Rajab, alimweleza Waziri kuwa wapo tayari kushirikiana kibiashara na ATCL.

Katika kutaka kufahamu ni ushirikiano wa namna gani wangependa kushirikiana na shirika hilo la umma, Sauda anaeleza kuwa yako maeneo mengi yanayotoa fursa kwa wao kushirikiana na ATCL.

Anasema wanaweza kushirikiana katika kutengeneza mtandao wa safari kwa kuunganisha safari ‘code sharing’ kwa safari za ndani na zile za kimataifa.

Anasema kwa kuwa Precision Air ina mtandao mpana zaidi wa safari za ndani, basi wanaweza kukubaliana ATCL wao wakajikita katika kuanzisha safari za kikanda na kimataifa na huku wao wakabaki na jukumu la kuwaunganisha abiria wa ndani kutoka maeneo mbalimbali kujaza ndege za ATCL kwa safari za nje.

“Lakini pia Precision Air ipo tayari kuingia ubia na ATCL ili kutengeneza shirika moja lenye nguvu,” anasema Sauda.

Tija ya ushirikiano

Sauda anaeleza kuwa tija inayoweza kupatikana kupitia ushirikiano huo anafafanua kuwa wanaweza kutengeneza wenye tija kwa mashirika yetu yote na hata ikiwezekana kuwa na shirika moja litakaloweza kutoa ushindani wa kweli kwenye soko la kikanda na kimataifa.

Safari ya ufufuko wa ATCL ilianza baada ya kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli, aliyeamua kulifufua shirika hilo kwa kununua ndege mbili mpya aina ya Bombardier ambazo zimeisaidia ATCL walau kufanya safari za ndani ya nchi kwa uhakika na moja ya nje kwenda nchini Comoro.

Pia Serikali imeendelea na jitihada za kununua ndege nyingine moja ambayo ilitarajiwa kuwasili nchini mwezi Juni mwaka huu (haijawasili hadi sasa ikidaiwa kuzuiwa nchini Canada) sambamba na nyingine mbili zinazotarajiwa kununuliwa mwakani ikiwamo moja aina ya Boeing 787 yenye uwezo wa kubeba zaidi ya abiria 260.

Ladislaus Matindi ni Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL anasema kununuliwa kwa ndege hizo kumeongeza ufanisi wa utendaji wa shirika hilo na kutoa nafasi kwa wananchi kuchagua wasafiri na shirika gani tofauti na ilivyokuwa awali ambapo kulikuwa na mashirika binafsi pekee.

Matindi anasema kununuliwa kwa ndege hizo kumeifanya ATCL kuongeza safari katika mikoa mbalimbali kama vile Mbeya, Kagera, Kilimanjaro, Dodoma, Ruvuma na Mtwara ambapo mwanzo haikuwa ikifanya safari katika maeneo hayo.

“Bado tunaendelea kufanya utafiti Pemba, Mpanda, Tanga na Mafia viwanja vingine kama vile vya Musoma, Shinyanga, Iringa vinafanyiwa marekebisho vikikamilika tutaanza safari za kwenda huko,” anasema.

Safari za nje ya nchi

Kwa sasa ATCL ina safari moja tu ya nje ya nchi kati ya Dar es Salaam na Visiwa vya Comoro ambayo imekuwapo kwa muda mrefu hata kabla ya shirika hilo kuanza kusuasua katika utoaji huduma.

Kwa mujibu wa Matindi, wako katika mikakati ya kujitanua katika soko la kimataifa wakilenga kuanza kwa kujiimarisha zaidi katika ukanda huu wa maziwa makuu unaojumuisha nchi za Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Malawi na Zambia.

Anasema safari hizo zitaanza mara moja baada ya kuwasili kwa ndege nyingine mpya aina ya Bombardier inayotarajiwa kufika nchini mwezi ujao.

Tayari shirika hilo limeanza mazungumzo na nchi mbalimbali ikiwamo China, India, baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya (EU), Afrika na Mashariki ya Kati ili kufanya makubaliano ya kufanya safari katika nchi hizo pale watakapopata ndege hizo zinazotarajiwa kununuliwa mwakani.

“Hatuwezi kusubiri tupate ndege ndiyo tuanze kutafuta wapi pakwenda, tumeanza mapema ili kufahamu namna ya kupata mafundi watakaozitengeneza ndege hizo katika nchi hizo, kujua upatikanaji wa chakula, mafuta na kupata watu watakaouza tiketi zetu huko.

Pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa abiria na kuangalia ushindani kama tutamudu, tutafanikisha hili kwa kutumia mpango kazi ambao uko hatua za mwisho kwa ajili ya utekelezaji wa makubaliano kati ya nchi na nchi,” anasema Matindi.

Kuongeza ufanisi wa shirika

Matindi anasema ili ATCL ijiendeshe kwa ufanisi ni lazima kuzingatia weledi katika uendeshaji ikiwa ni pamoja na kuwa na matumizi yenye uhalisia ikijumuisha kuajiri watumishi wenye sifa na kwa idadi inayostahili, kubana matumizi kwa kufanya manunuzi sahihi na si yanayolenga kujinufaisha hata kama si ya lazima.

Anasema kusiwe na safari zisizo za lazima kwa watumishi ambao wanasafiri kila mara pasi ya kuwa na sababu za msingi na kupewa posho zisizowastahili.

“Kama watumishi wanapewa safari za kila mara na wale wanaobaki watatekeleza kazi zote bila shida basi hao watumishi hawana sababu ya kuendelea kuwapo wanapaswa kupunguzwa,” anasema Matindi.

Anasema ili nauli ziwe za chini na kuwavutia abiria wengi zaidi ni lazima kuwe na mazingira ya kuwavutia abiria wengi zaidi ili kuongeza mapato, abiria wanapokuwa wengi mapato yatakuwa juu kwa hiyo hata nauli inaweza kupunguzwa.

“Pia tunapaswa kuhakikisha viongozi wa Serikali wanaokodi ndege wanalipa. Nitawadai, lazima nifanye hivyo kama wajibu wangu na si hofu ya kuulizwa na Rais aliyeagiza kufanya hivyo,” anasema.

Anasema wanatakiwa kujipanua zaidi katika soko la ndani ili kuongeza abiria na kuboresha huduma kwa wateja wao ili mtu akitumia ndege hizo awe na kiu ya kuzitumia tena, kwani mtu akitoka analalamika hatarudi.

Wakati Sauda akisema haya, ATCL iko katika mkakati wa ushirikiano na Shirika la Ndege la Ethiopia, Ethiopian Airways, ushirikiano uliofikiwa na Rais Dk. Magufuli na Waziri Mkuu wa nchi hiyo wakati wa ziara yake hapa nchini.

Kwa mujibu wa JPM, Ethiopian Airways ina jumla ya ndege 96 zinazofanya safari zake katika viwanja vipatavyo 72 huku shirika likitarajiwa kununua ndege nyingine mpya 40 hivi karibuni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles