NA ELIZABETH HOMBO
DAR ES SALAAM
NUSU ya kaya za Tanzania sawa na asilimia 69 zinahofia kuishiwa chakula huku asilimia 51 ya kaya hizo zimeripoti kwamba hakukuwa na chakula cha kutosha kulisha kaya nzima.
Matokeo hayo yametolewa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze ambapo pamoja na mambo mengine asilimia 84 ya wananchi wanaoishi vijijini, wameripoti uhaba wa chakula katika maeneo wanayoishi ikilinganishwa na wale wanaoishi maeneo ya mijini ambapo asilimia 64 wameripoti tatizo hilo.
“Asilimia 51 ya kaya zimeripoti kutokuwa na chakula cha kulisha kaya nzima au mwanakaya kushinda na njaa kwa sababu hakuweza kupata chakula huku asilimia 78 ya wananchi waliohojiwa wameripoti hali ni mbaya katika maeneo wanayoishi.
Matokeo hayo yaliyotolewa na Twaweza katika muhtasari uitwao Uchungu wa Njaa, umetokana na takwimu za Sauti za Wananchi ambao ni utafiti wa kwanza barani Afrika unaotumia njia ya simu.
Takwimu za muhtasari huo wa ripoti kuhusu upungufu wa chakula, zimekusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,800 wa Tanzania Bara.